Je, ushuru wa Trump kuathiri michezo duniani?

    • Author, Dan Roan
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Kuna athari ambazo zinaweza kutokea kwa Rais wa Marekani Donald Trump kuweka ushuru kwa sekta mbalimbali zinazohusishwa na michezo kupitia uwekezaji au ufadhili.

Masoko ya hisa yameanguka, huku kukiwa na hofu ya mfumuko wa bei, lakini mbali na msukosuko mkubwa wa kiuchumi. Je, vita vya kibiashara vinaweza kuathiri ulimwengu wa michezo?

Sarafu

Kama zilivyo klabu nyingi. Klabu ya Manchester United kutoka England, ina mkopo wa dola za kimarekani milioni 650 kutoka Marekani. Mtaalam wa fedha, Kieran Maguire anasema.

"Iwapo ushuru wa utawala wa Trump utakuwa na athari chanya kwa dola ya Marekani kwa kupanda thamani yake, hiyo ina maana kwamba thamani ya mikopo hiyo itaongezeka, na hii inaweza kuathiri akaunti za United."

Katika akaunti za 2022 kulikuwa na gharama ya pauni milioni 58 kutokana na kubadilisha fedha za kigeni kwenye mikopo hii. Kwa hivyo bodi ya United itakuwa ikiangalia riba na nini kinatokea katika soko kama athari za ushuru huu kwa vile viwango vya ubadilishaji wa kimataifa vinahusika.

Ufadhili

Marekani inatazamiwa kuandaa baadhi ya matukio makubwa ya michezo duniani katika miaka michache ijayo, ikiwa ni pamoja na Kombe la Dunia la 2026 na Olimpiki ya LA 2028 na Michezo ya Walemavu.

Matukio haya yanalenga kuwapa wafanyabiashara wa ng'ambo fursa muhimu ya kuongeza wasifu wao na kuongeza mauzo nchini Marekani.

Kampuni ya kutengeneza magari ya Korea ya Hyundai Group, kwa mfano, ina mkataba wa udhamini na shirikisho la soka duniani Fifa wakati wa Kombe la Dunia la Vilabu mwaka huu, na kisha Kombe la Dunia mwaka wa 2026. Je, sera kali za biashara za Trump zinaweza kufanya biashara kama hizo kuathirika?

"Naamini wafadhili wanatathmini upya mikataba kama hii, kutokana na vikwazo vya kibiashara ambavyo sasa vimewekwa," anasema John Zerafa, mwanamikakati wa zabuni za michezo.

"Kwa nini mfadhili atumie mamilioni ya pauni kufanya ufadhili usio na faida ya mauzo huko Marekani?"

Timu nyingi za michezo na wanariadha pia hufadhiliwa na kampuni za nguo za michezo.

Huku nyingi za kampuni hizo zikitegemea vifaa na utengenezaji wa bidhaa barani Asia - ambako Trump ameelekeza baadhi ya ushuru wa juu zaidi - haishangazi kwamba hisa katika kampuni kama za Nike, Adidas na Puma zote zimeshuka sana, huku kukiwa na hofu kwamba gharama za juu za kuagiza vifaa zitakwenda kwa watumiaji.

Mvutano wa nchi

Huku kukiwa n vita vya kibiashara, ushuru wa Trump pia umezua maswali katika hafla mbalimbali za michezo: Kombe la Ryder nchini Marekani baadaye mwaka huu, kisha kuna Kombe la Dunia la 2026, ambalo Marekani inashiriki pamoja na Mexico na Canada.

Mwezi Januari, Trump aliapa kutoza ushuru wa 25% kwa uagizaji kutoka nchi hizo jirani - washirika wawili wakubwa wa biashara wa Marekani. Lakini mwezi uliopita Trump alidai mvutano wa kisiasa na kiuchumi kati ya Marekani na waandaji wenza wa Kombe la Dunia una manufaa. "Nadhani itaifanya michezo iwe ya kusisimua zaidi. Mvutano ni jambo zuri," alisema.

Pia alitangaza kuunda kikosi kazi cha Kombe la Dunia, yeye atakuwa mwenyekiti ili kuhakikisha mashindano hayo yanakwenda vizuri. Fifa haijatoa maoni kuhusu kuhusu ushuru wa Rais wa Marekani.

Lakini sera za Trump zinazua maswali mazito juu ya utayari wa nchi hizo tatu na uwezo wa kufanya kazi pamoja, kuhakikisha mashabiki wanaweza kupata viza za kuingia, na kupita kwa urahisi kuvuka mipaka.

Kwa nyenzo zinazoagizwa kutoka nje kama vile chuma na alumini kuwa ghali, kunaweza pia kuleta wasiwasi kuhusu maendeleo ya miundombinu ya mashindano.

Trump pia amezungumza kuhusu kuifanya Canada kuwa 'jimbo la 51', na kusababisha wimbo wa Marekani kuzomewa na mashabiki wa Canada kwenye mechi za NBA na NHL.

Je, mvutano juu ya ushuru unaweza kusababisha matukio kama haya kujirudia kwenye Kombe la Dunia au hata Olimpiki?

Siyo ushuru tu. Kufukuzwa watu, mvutano na Umoja wa Ulaya na Nato, na uwezekano wa kuichukua Greenland na mvutano na mjirani zake. Haya yote yanaleta changamoto kubwa kwa Kombe la Dunia la 2026 na Michezo ya LA mnamo 2028.

Bidhaa na huduma za michezo

Huku ushuru wa kulipiza kisasi ukiwekwa na nchi nyingine, vita vya kibiashara vinaweza kuathiri mtu yeyote, mfano, timu au ligi kununua vifaa vya michezo vinavyotengenezwa Marekani, pamoja na watumiaji wa Marekani kununua bidhaa zinazotengenezwa ng'ambo.

Ligi Kuu ya Uingereza hupeleka matangazo ya mechi Marekani kupitia mkataba wake wa runinga wenye thamani ya pauni bilioni 2 na NBC, lakini kwa sababu hii inachukuliwa kuwa huduma badala ya bidhaa, ushuru huo hautumiki.

"Huenda kusiwe na athari, isipokuwa kama kuna aina fulani ya kuongezeka kwa uhusiano mbaya wa kibiashara kati ya Uingereza na Marekani," anasema Maguire.

"Kwa hivyo Ligi Kuu ya England haitalazimika kufikia maelewano ya aina fulani na mshirika wake wa utangazaji."

Wasiwasi mkubwa kwa soka ya Uingereza itakuwa ni wateja kuwa na pesa za kununua tiketi na usajili wa TV ikiwa kuma kushuka kwa uchumi.