Shambulio la kombora lililotekelezwa na Urusi katika mji wa
Kryvyi Rih ulio katikati mwa Ukraine limeua takriban watu 18 na kujeruhi makumi, maafisa wa Ukraine wamethibitisha.
Tisa kati ya waliofariki ni watoto, alisema Rais Volodymyr
Zelensky, ambaye alikulia katika mji huo wa Kryvyi Rih.
Maafisa wa eneo hilo walisema kuwa kombora lilipiga eneo la
makazi ya watu.
Picha zilionyesha mtu mmoja akiwa amelala kwenye uwanja wa
michezo, huku video ikionyesha eneo kubwa la jengo la ghorofa 10 likiwa limeharibiwa
na waathiriwa wakiwa wamelala barabarani.
Wizara ya ulinzi ya Urusi baadaye ilidai "shambulio la
kombora lililotekelezwa kwa umahiri wa
hali ya juu" lililenga mkutano wa "makamanda wa vitengo na wakufunzi
wa mataifa ya Magharibi" katika mkahawa, na kukadiria kuwaua 85.
Hata hivyo haikutoa ushahidi wowote.
Jeshi la Ukraine lilijibu kwa kusema kuwa Urusi inaeneza
habari za uongo kwa kujaribu "kuficha uhalifu wake".
Ilisema kuwa
Moscow ilirusha kombora la aina ya Iskander-M ili kusababisha madhara na hasara.
Shambulio hilo,
mapema Ijumaa jioni, lilikuwa miongoni mwa mashambulizi mabaya zaidi kulenga
mji wa Kryvyi Rih tangu kuanza kwa uvamizi kamili wa Urusi mnamo 2022, na
linakuja wakati Rais wa Marekani, Donald Trump akishinikiza kusitishwa kwa
mapigano.
Zelensky
aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii kwamba takriban majengo matano
yameharibiwa katika shambulizi la ijumaa: "Kuna sababu moja tu kwa nini hali
hii inaendelea: Urusi haitaki usitishaji wa mapigano, na tunashuhudia."