Wanasayansi wagundua ubongo wa mwanadamu uliogeuka kioo

Chanzo cha picha, Guido Giordano
Karibu miaka 2,000 baada ya kijana mmoja kufariki katika mlipuko wa volkano ya Vesuvius, wanasayansi wamegundua kwamba ubongo wake ulihifadhiwa baada ya kubadilika kuwa kioo kutokana na wingu la majivu lenye joto kali.
Watafiti waligundua vipande hivyo vya kioo mwaka 2020 na walidhani kuwa vilikuwa mabaki ya ubongo, lakini hawakuelewa jinsi yalivyoundwa.
Vipande hivyo vidogo, vyenye ukubwa wa kama punje ya harage vyenye rangi nyeusi, vilipatikana ndani ya fuvu la mtu huyo aliyekuwa na umri wa takriban miaka 20, ambaye alikufa wakati volkano ilipolipuka mwaka 79 (kabla ya kristo) karibu na eneo la Naples la sasa.
Wanasayansi sasa wanaamini kwamba wingu la majivu lenye joto la hadi 510°C lilifunika ubongo wake kisha kupoa kwa haraka, na kusababisha kiungo hicho kubadilika kuwa kioo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ni tukio la kipekee duniani ambapo tishu za binadamu, imebadilika na kuwa kioo kwa njia ya asili.
"Tunaamini kwamba hali mahususi ambazo tumerejesha kwa mchakato wa ubongo huu kubadilika kuwa kioo zinaufanya ugunduzi huu kuwa wa kipekee, ingawa si jambo lisilowezekana kutokea kwingine," alisema Profesa Guido Giordano kutoka Università Roma Tre alipoiambia BBC News.
"Hili ni jambo la kipekee," aliongeza.
Ubongo huo ulikuwa wa mtu aliyefariki akiwa kitandani ndani ya jengo lililojulikana kama Collegium, kwenye barabara kuu ya mji wa Kirumi wa Herculaneum.
Vipande vya kioo vilivyogunduliwa na wanasayansi vina ukubwa kati ya sentimita 1-2 hadi milimita chache tu.

Chanzo cha picha, Guido Giordano
Mlipuko mkubwa wa volkano ya Vesuvius ulifunika Herculaneum na mji jirani wa Pompeii, ambako watu wapatao 20,000 waliishi. Mabaki ya takriban watu 1,500 yamepatikana hadi sasa.
Wanasayansi sasa wanaamini kwamba wingu la majivu moto lilishuka kutoka Vesuvius kwanza, huenda likisababisha vifo vingi.
Mtiririko wa moto na vitu vya volkano unaofahamika kama pyroclastic flow, ulifuatia na kufunika eneo hilo.
Wataalamu wanaamini kwamba wingu la majivu ndilo lililosababisha ubongo wa mtu huyo kubadilika kuwa kioo kwa sababu pyroclastic flow haikufikia joto la kutosha au kupoa kwa kasi ya kutosha kufanya hivyo.
Mchakato wa kutengeneza kioo unahitaji mazingira mahususi za joto na hutokea kwa nadra katika mazingira ya asili.
Ili kitu kibadilike kuwa kioo, lazima kuwe na tofauti kubwa ya joto kati ya kitu hicho na mazingira yake.

Chanzo cha picha, Guido Giordano
Timu ya watafiti ilitumia teknolojia ya X-ray na darubini ya elektroni kuthibitisha kuwa ubongo huo ulipaswa kupashwa joto hadi angalau 510°C kabla ya kupoa kwa haraka.
Hakuna sehemu nyingine ya mwili wa mtu huyo inayoaminika kubadilika kuwa kioo.
Ni vitu vyenye unyevunyevu pekee vinavyoweza kubadilika kuwa kioo, jambo ambalo linamaanisha kuwa mifupa haikuweza kubadilika kwa njia hiyo.
Tishu zingine laini, kama viungo vya ndani, huenda viliharibiwa kabisa na joto kabla ya kupata fursa ya kupoa vya kutosha ili kubadilika kuwa kioo.
Wanasayansi wanaamini kuwa fuvu la kichwa lilitoa ulinzi fulani kwa ubongo wake, jambo lililosaidia mchakato wa ubadilishaji huo.
Utafiti huu umechapishwa katika jarida la kisayansi Scientific Reports, linalotumika na watafiti kuripoti kazi zao kwa wataalamu wenzao












