Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwanini 2023 ulikuwa mwaka mgumu kwa nchi za Magharibi?
Katika uga wa kisiasa wa kimataifa, Marekani, Ulaya na nchi nyingine za magharibi zimekumbwa na pigo katika kipindi cha miezi 12 iliyopita. Pigo linaloashiria kuhama kwa ushawishi wa magharibi ambao umetawala kwa miaka mingi.
Licha ya mafanikio ya hivi karibuni katika Bahari Nyeusi, lakini matarajio ya Marekani na Ulaya kuhusu vita vya Ukraine hayajafikiwa linapokuja suala la vita. Na hayo ni matokeo mabaya kwa NATO na EU, ambazo zimetoa mabilioni ya dola Ukraine.
Wakati kama huu mwaka jana, NATO ilikuwa na matumaini makubwa kwamba jeshi la Ukraine lingeweza kufanikiwa kutokana na vifaa vya kisasa vya kijeshi na mafunzo.
Matumaini pia yalikuwa - wangeweza kuwafukuza wanajeshi wa Urusi katika maeneo waliyoyateka. Lakini hilo halikutokea.
Mashambulizi ya Ukraine yameshindwa
Katika nusu ya kwanza ya 2023, vikosi vya Ukraine vilivyofunzwa nchini Uingereza na maeneo mengine vilipopelekwa mashariki vikiwa na mizinga, Urusi ilizindua operesheni kubwa zaidi na ya kina ya ulinzi.
Mabomu ya ardhini ya kushambulia vifaru na wanajeshi, mitaro, mahandaki, ndege zisizo na rubani na mizinga - vyote vilitumika kuzuia mpango wa Ukraine. Na mashambulizi ya Ukraine ya kukomboa maeneo yanayokaliwa na Urusi hadi sasa yameshindwa.
Kuna uhaba mkubwa wa silaha kwa Ukraine. Bunge la Marekani limezuia juhudi za Ikulu ya White House kutoa dola bilioni 60 za msaada wa kijeshi. Wakati huo huo Hungary imesitisha msaada wa euro bilioni 50 katika Umoja wa Ulaya.
Urusi imeweka uchumi wake kwenye msingi wa vita. Inatenga theluthi moja ya bajeti yake ya kitaifa kwa ulinzi. Maeneo makubwa ya Ukraine yameshambuliwa kwa maelfu ya makombora.
Ni wazi, hali hii inaikatisha tamaa Ukraine - wakati Urusi inadhibiti takribani asilimia 18 ya ardhi ya Ukraine. NATO imetoa silaha nyingi na imejaribu kila iwezalo kuepuka kuingia vitani huko Ukraine.
Mashitaka dhidi ya Putin
Machi 2023, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu huko The Hague, Uholanzi, ilimfungulia mashtaka Putin. Nchi za Magharibi zilitarajia upinzani dhidi yake ungeongezeka katika nchi yake na ikiwa atakwenda nje ya nchi angekamatwa. Lakini hakuna hata moja limetokea.
Baada ya uamuzi huo wa mahakama, Rais Putin alitembelea Kyrgyzstan, China, Umoja wa Falme za Kiarabu na Saudi Arabia. Na alipewa mapokezi makubwa.
Ilitarajiwa vikwazo vya Umoja wa Ulaya vitaharibu uchumi wa Urusi na kumlazimisha Putin kupunguza mashambulizi yake. Lakini Urusi yaonekana kuhimili vikwazo hivi hadi sasa.
Bado inauza bidhaa nyingi ulimwenguni kupitia nchi kama China na Kazakhstan. Nchi za Magharibi zimekwepa kwa kiasi kikubwa kununua mafuta na gesi ya Urusi. Lakini Urusi inapata wateja wengine wa kuwauzia, ingawa kwa bei ya chini.
Nchi za Kiarabu na Iran
Wakati wa mkutano wa hivi karibuni mjini Riyadh, Saudi Arabia, Mawaziri kutoka nchi za Kiarabu walizikosoa nchi za Magharibi kwa kuwa na undumilakuwili.
"Unatarajia tuilaani Urusi kwa kuua raia nchini Ukraine wakati serikali hizi zinakataa usitishaji vita huko Gaza ambako maelfu ya raia wanauawa?" Nchi hizi zilihoji.
Vita vya Israel na Hamas ni wazi vimekuwa vya uharibifu kwa wakazi wote wa Gaza na Waisraeli walioathiriwa na shambulio baya la Hamas la Oktoba 7 kusini mwa Israel.
Vita hivyo vimegeuza macho ya walimwengu kutoka Ukraine, mshirika wa NATO na silaha za Marekani zimeelekezwa Israel. Lakini machoni mwa Waislamu wengi na watu wengine duniani; kuilinda Israel kwenye Umoja wa Mataifa, kumezifanya Marekani na Uingereza kuonekana kuwa washirika wa uharibifu wa Gaza.
Licha ya juhudi za Magharibi, Iran iko mbali na kutengwa. Imeeneza misimamo yake ya kijeshi kupitia wapiganaji nchini Iraq, Syria, Lebanon, Yemen na Gaza. Serikali inatoa pesa, mafunzo na silaha kwa wanamgambo hao.
Iran imeunda ushirikiano wa karibu na Urusi mwaka huu. Inaendelea kuipatia Urusi ndege zisizo na rubani za Shaheed kushambulia miji ya Ukraine.
Ingawa inachukuliwa kuwa tishio na nchi nyingi za Magharibi, Iran imefaidika na vita vya Gaza kwa kujiweka kama mfuasi wa Palestina katika Mashariki ya Kati.
Afrika na ushawishi wa mataifa makubwa
Nchi za eneo la Sahel la Afrika Magharibi zimeingia kwenye mkondo wa mapinduzi ya kijeshi.
Makoloni ya zamani ya Ufaransa; ya Mali, Burkina Faso na Jamhuri ya Afrika ya Kati yanapinga ushawishi wa mataifa ya Magharibi. Niger ilimpindua rais wake anayeungwa mkono Magharibi mwezi Julai .
Wanajeshi wa mwisho wa Ufaransa waliosalia wameondoka. Hata hivyo, wanajeshi 600 wa Marekani katika nchi hiyo katika kambi mbili wamebaki.
Maeneo yote ambayo majeshi ya Ufaransa na kimataifa yalikuwepo - nafasi zao zinachukuliwa na mamluki wa Urusi. Kundi la Wagner linaendelea na mikataba yao ya kibiashara yenye faida nyingi licha ya kifo cha kiongozi wao, Yevgeny Prigozhin, katika ajali ya ndege mwezi Agosti.
Wakati huo huo, Afrika Kusini, iliyowahi kuchukuliwa kuwa mshirika wa Magharibi, imekuwa ikifanya mazoezi ya pamoja ya majini na meli za kivita za Urusi na China.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea Kaskazini ni nch iliyowekewa vikwazo vikali kutokana na mradi wake wa silaha za nyuklia na programu ya makombora ya masafa marefu.
Licha ya hayo yote, imedumisha uhusiano wa karibu na Urusi. Mwaka jana, kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un alitembelea mji wa bandari wa Urusi.
Tangu wakati huo, Korea Kaskazini imeripotiwa kutuma makombora zaidi ya milioni moja kwa vikosi vya Urusi vinavyopigana nchini Ukraine.
Korea Kaskazini imefanyia majaribio makombora kadhaa ya masafa marefu. Sasa wanaaminika kuwa na uwezo wa kufikia miji mingi nchini Marekani.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Esther Namuhisa