Jinsi Wahindi wawili walivyotoweka usiku wa Julai nchini Kenya

Khan

Watalii wawili wa Kihindi na dereva wao wa ndani walitoweka katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, usiku wa Julai.

Zaidi ya miezi miwili baada ya tukio hilo, polisi tisa wamekamatwa kuhusiana na kesi hiyo, ambayo India inasema "inaifuatilia kwa karibu".

BBC imeweka pamoja matukio yaliyojiri kuelekea kutoweka kwao na kujaribu kufumba fumbo hilo kwa kuangazia maswali mengi ambayo hayajajibiwa.

Katika moja ya machapisho yake ya mwisho kwenye mitandao ya kijamii kabla ya kutoweka, Zulfiqar Ahmad Khan alishirikisha video ya simba anayenguruma katika mbuga ya wanyama ya Maasai Mara nchini Kenya ambako alikuwa akipumzika.

"Asubuhi ya kichawi huko Maasai Mara. Hebu fikiria mara ya kwanza kukutana na Simba. Kiamsha kinywa cha mtu yeyote?" aliandika katika chapisho la kawaida la furaha.

Mtaalamu huyo wa masoko wa vyombo vya habari wa India mwenye umri wa miaka 48 alikuwa amefanya kazi mara ya mwisho kama afisa mkuu wa uendeshaji wa Balaji Telefilms, kampuni ya Televisheni yenye makao yake Mumbai.

Wasifu wa Bw Khan kwenye LinkedIn ulimtaja kama "kiongozi wa biashara anayezingatia ufanisi wa watu" na uzoefu wa zaidi ya miaka 19 katika kampuni za utangazaji na mawasiliano ya kidijiti; mwenye "uwezo mkubwa, kocha anayeendeshwa na utendaji, mshauri na meneja".

Marafiki zake walimtaja kama "mwanaspoti makini, mpenda vyakula, msafiri na mgunduzi" na mpenzi wa kriketi.

Baada ya kuacha kazi mwezi Juni, Bw Khan alikuwa amesafiri nchini Kenya kwa mwezi mmoja.

Machapisho yake ya Facebook na Instagram yalijaa picha na video za wakati wake nchini: kiamsha kinywa jijini Nairobi, alasiri zake katika mbuga za wanyama.

Bw Khan na Bw Kidwai (wa nyuma) wakiwa Nairobi siku mbili kabla ya kutoweka
Maelezo ya picha, Bw Khan na Bw Kidwai (wa nyuma) wakiwa Nairobi siku mbili kabla ya kutoweka
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Siku nne kabla ya kutoweka, aliwaita marafiki na alisikika kuwa na shauku ya kuzuru Kenya.

Mmoja wao alikuwa Rajiv Dubey, mtaalamu wa masoko wa Delhi, ambaye alikuwa amemfahamu kwa miaka 24.

"Alionekana mwenye furaha sana. Alikuwa amezungumza na baadhi ya marafiki zake siku chache zilizopita na alisema nao kwa kirefu kuhusu wanyamapori na kuwashauri watembelee eneo hili ni 'pazuri'," Bw Dubey alisema.

Bw Khan aliwaambia marafiki zake kwamba angerejea nyumbani tarehe 24 Julai na kwamba alitaka pia kurejea Kenya kushuhudia "Uhamiaji Mkubwa" wa kila mwaka - wakati zaidi ya nyumbu milioni moja na mifugo wanahamia kwenye mbuga za Maasai Mara.

Usiku wa tarehe 22 Julai, Bw Khan alitoweka, pamoja na Muhindi mwingine na dereva Mkenya.

Mhindi wa pili alikuwa Mohammad Zaid Sami Kidwai, 36, ambaye pia alizur8 Nairobi kwa visa ya kitalii.

Habari kuhusu Bw Kidwai, ambaye anatokea jiji la kaskazini mwa India la Lucknow na japo aliishi Dubai, bado ni za kutatanisha.

Ripoti za vyombo vya habari nchini Kenya zilimtaja kama "mtaalamu wa teknolojia ya habari na mawasiliano" ambaye aliishi "maisha ya kibinafsi".

Katika barua kwa Ubalozi wa India huko Nairobi mnamo Julai, mkewe Ambreen Kidwai alisema mumewe amekuwa akizuru Kenya tangu Februari kwa utalii.

Takriban polisi tisa wa Kenya wamekamatwa kuhusiana na kisa hicho
Maelezo ya picha, Takriban polisi tisa wa Kenya wamekamatwa kuhusiana na kisa hicho

Alimtaja Bw Khan kama rafiki wa mumewe, na kuongeza kuwa wote wawili walikuwa wametoka katika hoteli ya Nairobi waliyokuwa wakiishi na kuelekea kwenye baa saa tano karoro robo (22:45) usiku wa Julai 22.

Bi Kidwai alisema "alimtumia ujumbe" mumewe karibu na usiku wa manane kuuilizia atarudi saa ngapi.

Alimjibu akisema ataondoka kwenye baa ndani ya "dakika 15".

Muda mfupi baadaye usingizi ulimbeba na alipoamka saa tisa usiku (03:00), alipata kwamba mumewe alikuwa hajarudi, Bi Kidwai alisema.

Alipiga simu ya mume wake - na ya dereva - lakini zote zilionekana kuwa zimezimwa.

Aliwasiliana na "marafiki wa pande zote" huko Nairobi, lakini wanaume hao wawili hawakuwa na yeyote kati yao.

Siku iliyofuata, Bi Kidwai alienda polisi na kuripoti kutoweka kwa mumewe na Bw Khan.

Pia alienda kwenye baa na kutafuta picha za CCTV - zilionyesha Wahindi hao wawili wakiondoka mahali hapo karibu na saa moja asubuhi na kuingia kwenye gari aiana ya Toyota sendan.

Pia alitambua gari lililoachwa nyuma ambalo polisi walibaini ndilo ambalo mumewe na Bw Khan walikuwa wakisafiria.

Huko Mumbai, marafiki wa Bw Khan walikuwa na wasiwasi kumhusu.

Walisema kulikuwa na "kimya kisichokuwa cha kawaida" baada ya Julai 21 - hakuna ujumbe wowote katika mitandao ya kijamii, hakuna simu - na "kilichowatia wasiwasi zaidi marafiki ni kwamba - [ujumbe] wetu wa WhatsApp haukuonyeshwa kama ilipokelewa".

Muonekano wa Mbuga ya Kitaifa ya Aberdare, Kenya.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Muonekano wa Mbuga ya Kitaifa ya Aberdare, Kenya.

Baada ya kusubiri kwa siku 70na maafisa wa polisi nchini Kenya kutoonyesha kupiga hatua yoyote katika uchunguzi wao, marafiki walianzisha kampeni mtandaoni kumshinikiza Waziri Mkuu Narendra Modi kuingilia kati ana kusaidia kumtafuta Bw. Khan - ombi hilo limetiwa saidi na zaidi ya watu 10,000 kufikia sasa.

"Zulfi hazuru tu nchi ya kigeni au mahali popote - bila kuchukua wiki kadhaa kutalii eneo hilo, nakujifunza mengi kuhusu hisoria na utamaduni wa eneo husika," marafiki zake waliandika katika ombi hilo.

Ziara yake ya Kenya , walisema ilikuwa ya alikuwa "mvumbuzi Zulfi huku akitaka kupata uzoefu wa nchi mpya ... mara Zulfi akatoweka na hajawahi kuonekana tena. Hakuna mawasiliano na familia na marafiki".

Nini kiliwakumba wanaume hao?

Vyombo vya habari vya ndani vikiwanukuu maafisa, viliripoti kwamba Wahindi hao wawili walikuwa Kenya kusaidia kampeni ya uchaguzi ya William Ruto, mwanasiasa mwenye haiba mwenye umri wa miaka 55 ambaye aliapishwa kama rais wa tano wa nchi hiyo mwezi Septemba, baada ya ushinda uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali.

Wahindi hao walitoweka pamoja na dereva wao raia wa Kenya Nicodemus Mwania punde tu baada ya kuchukuliwa na polisi jijini Nairobi, ripoti zilisema.

Takriban miezi mitatu baadaye, polisi wa Kenya walidai kuchukua hatua: polisi tisa wamekamatwa tangu tarehe 21 Oktoba kuhusiana na kile wanachoamini kuwa ni tukio la utekaji nyara na mauaji ya watu hao watatu.

Rais Ruto hivi majuzi alivunja kikosi cha polisi mashuhuri kilicholaumiwa kwa mauaji na kutoweka kinyume na sheria

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Rais Ruto hivi majuzi alivunja kikosi cha polisi mashuhuri kilicholaumiwa kwa mauaji na kutoweka kinyume na sheria

Polisi hao walikuwa sehemu ya kikosi maalum kinachofahamika kama Kitengo cha Huduma Maalum ambacho kilivunjwa na Rais Ruto hivi majuzi kwa madai ya kutekeleza mauaji ya kiholela na kutoweka kwa washukiwa kwa miaka kadhaa, kulingana na Kitengo cha Masuala ya Ndani cha Kenya, ambacho kinachunguza malalamiko dhidi ya polisi.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema uchunguzi wao huru umehusisha kikosi hicho na vitengo vingine vya polisi na vifo vya zaidi ya watu 600 katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Baadhi ya miili hiyo ilipatikana baadaye katika mito magharibi na kaskazini mwa Kenya.

Washukiwa wa kesi ya Wahindi waliotoweka ni pamoja na inspekta mkuu wa polisi, koplo na madereva wa polisi."Bado hawajashtakiwa ili tuweze kukanusha rasmi madai hayo," Danstan Omari, wakili wa washukiwa, alisema.

Kulingana na hati ya kiapo iliyowasilishwa na polisi katika mahakama hiyo siku ya Jumatatu, teksi iliyowabeba Wahindi hao ilisimamishwa kwa nguvu na kundi la wanaume waliokuwa wakisafiri kwa gari la Subaru kwenye barabara ya Nairobi.

Wahindi hao na dereva wao walitekwa nyara na kuendeshwa kwa gari lingine hadi msitu wa Aberdare, kilomita 150 kutoka mjini, ambapo inadaiwa waliuawa na "miili yao kutupwa".

Hati hiyo ya kiapo inazungumzia takriban washukiwa wanne, akiwemo mwanamume mmoja ambaye alikuwa amepanga utekaji nyara sawia wa watu wengine watatu jijini Nairobi.

Wanaharakati wa Kenya wamekuwa wakiandamana kupinga mauaji ya kiholela yanayofanywa na polisi

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Wanaharakati wa Kenya wamekuwa wakiandamana kupinga mauaji ya kiholela yanayofanywa na polisi

Upekuzi katika msitu huo wiki iliyopita haukupata chochote isipokuwa "nguo na vitu vingine" vichache ambavyo vingetumwa kwa uchunguzi wa DNA, polisi waliambia mahakama.

Gazeti moja nchini humo la liliripoti kwamba "mifupa na mikanda" pia ilipatikana mahali hapo, lakini haikuweza kuthibitishwa.

Polisi walisema kutekwa nyara kwa Wahindi hao na dereva wao ni "operesheni ya mashirika mengi kati ya Kurugenzi ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na vyombo vingine vya usalama".

Wahindi hao wawili walikuwa nchini Kenya kwa "madhumuni ya kibiashara," kulingana na polisi.

Lakini familia na marafiki wa Bw Khan wanapinga vikali kwamba alikuwa nchini Kenya kwa shughuli za kibiashara.

Bi Kidwai pia alisema katika barua yake kwamba mumewe alikuwa huko kama mtalii.

"Zulfi hakuwahi kuniambia wala marafiki zake kuhusu kazi yoyote aliyokuwa akifanya kwa ajili ya kampeni ya uchaguzi huko. Daima angenipigia simu ikiwa anafanya jambo jipya," Bw Dubey alisema.

Lakini Dennis Itumbi, mshauri aliyeendesha kampeni ya kidijitali ya Rais Ruto, alisema Wahindi hao wawili "wamesaidia" katika kampeni ya mitandao ya kijamii.

Dennis Itumbi
Maelezo ya picha, Dennis Itumbi

“Nilikutana na wawili hao mara kadhaa jijini Nairobi, nilijua wanakaa wapi, nilikuwa nao kwenye kundi la Telegram, hawakuajiriwa kwenye kampeni, lakini walitupatia mawazo, mengine tuliyatumia,” Bw Itumbi aliniambia kwa simu kutoka Nairobi.

Ahmednassir Abdullah, mwanasheria wa familia za Wahindi, aliniambia: "Walikuwa wakimsaidia mmoja wa wagombea urais katika baadhi ya vyombo vya habari vidogo [ya kijamii].

Nadhani walikuwa wataalamu wa jinsi ya kutengeneza video fupi za mikutano ya kisiasa. Nadhani wote wawili walikuwa wakifanya jakumu dogo, la pembeni sana [kwenye kampeni]."

Maswali yasiyo na majibu

Polisi wanasema wanahitaji kufanya "uchunguzi zaidi na kukusanya ushahidi zaidi" ili kuwahusisha washukiwa hao na kutoweka kwa watu hao watatu.

Ni wazi kuna maswali mengi ambayo hayajajibiwa.

Je, hao Wahindi wawili walijuana tangu awali? Je, walifanya kazi kwa ajili ya kampeni ya uchaguzi wa urais wa Kenya na kushikwa na mizozo ya kisiasa? Kwa nini walidaiwa kutekwa? Polisi wamepata mabaki ya nani?

Hakuna anayejua kabisa.