Rais wa Kenya avunja kikosi cha 'polisi wauaji'
Na Abdalla Seif Dzungu
BBC Swahili

Chanzo cha picha, Getty Images
''Tuna mpango wa kuimarisha usalama nchini Kenya ili kuzuia aibu ya Wakenya kuuawa na maafisa wa polisi na miili yao kutupwa katika Mto Yala na kwengine''.
Hayo ni matamshi ya rais wa Jamhuri ya Kenya William Ruto wakati alipovunjliia mbali kitengo maalum cha SSU kilichokuwa kikihudumu chini ya afisi ya Mkurugenzi mkuu wa Ujasusi DCi nchini Kenya.
Rais Ruto alisema hiyo ni sehemu ya mabadiliko ya uongozi huku utawala mpya ukipania kurekebisha usimamizi wa idara ya usalama nchini.
Alisema kwamba, kitengo hicho ndicho kilichohusika pakubwa na mauaji ya kiholela na kupotea kwa watu ambão miili yao baadaye ilipatikana maeneo tofauti nchini kama vila mto Yala.
Hatua hiyo inajiri baada ya kiongozi huyo kupokea ripoti ya uchunguzi kuhusu kutoweka kwa raia wawili wa India na mwenyeji wao aliyekuwa dereva wa gari walimokuwa.
Ripoti hiyo ilipendekeza kuvunjiliwa mbali kwa kitengo hicho ili kuruhusu uchunguzi kukamilika kabla ya faili hiyo kuwasilishwa kwa mkurugenzi mkuu wa mashtaka nchini kenya.
Je kitengo hicho kilikuwa na majukumu gani?
Kuvunjiliwa mbali kwa kitengo cha polisi cha Flying Squad – kilichohusisha maafisa wa polisi waliokuwa wakihusika na ujasusi mbali na kukabiliana na wahalifu nchini, kulisababisha kuundwa kwa kitengo maalum cha Sting Squad Headquarters SSH chenye maafisa hamsini waliopatiwa mafunzo ya hali ya juu.
Kitengo hicho kilipewa majukumu ya kushughulikia uhalifu wa hali ya juu kama vile wizi wa kutumia silaha, utekaji nyara na wizi wa magari katika jiji na kaunti zinazozunguka mji wa Nairobi , lakini majukumu yao mara kwa mara yaliongezeka zaidi ya mji wa Nairobi.
Walipewa jukumu la kufanya kazi kwa karibu na mashirika mengine ya usalama ili kuzuia uhalifu kutoa habari za kijasusi mbali na kushughulikia matukio ya uhalifu yanayohitaji dharura.
Kwanini kimevunjiliwa mbali?

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kumekuwa na tuhuma kwamba polisi wamekuwa wakihusika na vifo na kupotea kiholela kwa Wakenya ambapo wanaharakati wa haki za binadamu wametaka uchunguzi ufanyike.
Mnamo Aprili na Mei 2019, Shirika la haki za kibinadamu la Human Rights Watch ilihoji watu 35 wakiwemo mashahidi, wanafamilia wa waathiriwa, madaktari na wafanyakazi wa kijamii, wanaharakati, na wafanyakazi wa polisi akiwemo msemaji wa polisi jijini Nairobi.
Shirika hilo katika ripoti yake linasema lilifanya kazi kwa karibu na mashirika washirika huko Dandora na Mathare jijini Nairobi katika kutambua waathiriwa na familia.
Mfanyabiashara ambaye pia ni mtoaji habari wa polisi aliiambia Shirika hilo kwamba polisi wana orodha ya watu wanaopanga kuwaua, wakiwemo wezi mbali na wanaume na wanawake ambao wametofautiana na maafisa hao.
Human Rights Watch pia imeandika mauaji ya kiholela katika muktadha wa ghasia za uchaguzi na oparesheni za kukabiliana na ugaidi huko Nairobi na eneo la kaskazini mashariki, na pwani katika operesheni za kukabiliana na ugaidi.
Imedaiwa kwamba baadhi ya wanachama wa kitengo hicho pia walihusika katika uhalifu wa kutumia silaha katika eneo la matuu ambapo walivamia kampuni moja ya kusambaza gesi na kuiba zaidi ya ksh.370,000 miongoni mwa visa vingine chungu nzima. Maafisa hao baadaye walinyang'anywa silaha na kushtakiwa mahakamani.
Je makundi ya haki za Kibinadamu yanasemaje?
Shirika la haki za kibinadamu la Amnesty Kenya liliunga mkono kuvunjwa kwa kitengo hicho huku likiitaka idara ya polisi kukagua shughuli za SSU na kujibu hadharani madai ya kuwajibika kwa kutoweka na mauaji ya kiholela ya washukiwa wengi,” shirika hilo la kutetea haki za binadamu lilichapisha kwenye mtandao wake wa Twitter.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe
Mto wa Yala uliopo eneo la Nyanza umekuwa ukigonga vichwa vya habari mwaka uliopita baada ya miili ya watu kupatikana ndani yake ikiwa imetupwa
Kufuatia malalamishi ya Wakenya katika mitandao ya kijamii kuhusu kupatikana kwa miili ndani ya mto huo mashirika ya haki za kibinadamu ikiwemo Haki Afrika yalielekea katika kaunti ya Siaya nchini Kenya ili kufuatilia matukio hayo.
Shirika hilo lilidai kugundua miili 21 katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya kaunti , ambapo ilikuwa imefungwa kamba, mingine ikiwa katika magunia na mingine ikiwa na alama za kukatwa ..
Shirika hilo linasema kwamba lilithibitisha kupitia kituo hicho cha kuhifadhia maiti kwamba mnamo mwezi Oktoba mwaka uliopita kilizika miili tisa iliokiuwa imepatikana katika mto huo katika kaburi la pamoja.














