Miili iliyoopolewa katika Mto Yala Kenya: Je ni nini tunachokijua kufikia sasa?

Chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Yala

Chanzo cha picha, Twitter

Maelezo ya picha, Chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Yala
Muda wa kusoma: Dakika 2

Wasimamizi wa hospitali katika eneo la magharibi mwa Kenya wamethibitisha kwa BBC kuhusu uwepo wa miili isiyopungua 20 iliooza katika chumba kimoja cha kuhifadhia maiti karibu na mto ambapo miili hiyo inadaiwa kuopolewa katika wiki za hivi karibuni.

Je mashirika ya haki za kibinadamu yanasemaje?

Kufuatia malalamishi ya Wakenya katika mitandao ya kijamii , shirika la haki za kibinadamu la Haki Afrika lilielekea katika kaunti ya siaya ili kufuatilia tukio hilo.

Linasema kwamba liligundua miili 21 katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya kaunti , ambapo miili mingi ilikuwa imefungwa kamba na mingine kupatikana katika magunia, mingine ikiwa na alama za kukatwa na mingine ikiwa imefungwa na nailoni katika vichwa.

Shirika hilo linasema kwamba lilithibitisha na kituo hicho cha kuhifadhia maiti kwamba mnamo mwezi Oktoba kilizika miili tisa katika kaburi la pamoja.

Katika mto Yala , Haki Afrika imesema kwamba muogeleaji ambaye amekuwa akiopoa miili hiyo amesema kwamba tangu mwezi Julai 2021, aliopoa miili 31 - miili kumi ikiwa ndani ya gunia.

Katika mto huo wanaharakati hao walithibitisha miili miwili iliokuwa ikiolea katika maji ya mto huo ambayo pia hutumika kwa matumizi ya nyumbani na jamii za eneo hilo.

Shirika hilo la haki za kibinadamu hivi sasa limetoa wito wa kutaka kubaini miili hiyop. Vievile limeitaka serikali kufichua ni nani anayehusika na mauaji hayo na kutupwa kwa miili hiyo katika mto huo ili kuchukuliwa hatua kali.

Je waakazi wanasemaje?

Muogeleaji mmoja ambaye amekuwa akihusika katika kuiopoa miili hiyo amesema kwamba baadhi ya miili ilikuwa imekatwakatwa, imefungwa kwa kutumia Kamba na kutiwa katika ,magunia.

Muogeleaji huyo ameaongezea kwamba tangu katikati ya mwaka uliopita amekuwa akiiopoa miili na anaamini kwamba huenda kuna miili zaidi inayooza katika mto huo.

'Maji hayo hutumika kwa matumizi ya binadamu'

Maji ya mto huo yamekuwa yakitumiwa na Wakenya katika eneo hilo kwa matumizi ya nyumbani

Tayari mkuu wa hospitali ya kaunti ya Yala iliopo kilomita 40 kaskazini magharibi mwa mji wa Kisumu , amethibitishia BBC kwamba chumba cha kuhifadhia maiti katika hopsitali hiyo kinamiliki miili 21 ambayo haijapata wenyewe.

Kufikia sasa haijulikani ni nani anayehusika na mauaji hayo ama miili hiyo inatoka wapi .

Je maafisa wa polisi wamesema nini kufikia sasa

Katika taarifa iliyoandikwa Jumatano, Januari 19, na kutiwa saini na msemaji wa polisi, Bruno Shioso, ilibainika kuwa kitengo maalum kilikuwa kimeundwa kuchunguza suala hilo.

Polisi walisema kuwa timu ya maafisa kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) imeanza uchunguzi wao na itafumbua kitendawili cha idadi kubwa ya miili hiyo.

"Kikosi kutoka afisi ya mKurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai kiliteuliwa na kupewa jukumu la uchunguzi ambao umekuwa ukiendelea kuhusu matukio hayo," ilisema taarifa hiyo.

Zaidi ya hayo, Idara ya polisi ilisema kuwa timu nyingine ya wataalam wa uchunguzi walikuwa wametumwa katika eneo hilo kusaidia katika uchunguzi.

Shioso alisema kuwa kikosi hicho kitasaidia katika utambuzi wa miili ambayo haijadaiwa na kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Yala Sub County Level IV.

"Ili kuharakisha utambuzi wa waathiriwa na uchunguzi mwingine wa kisayansi, timu maalum ya uchunguzi wa kisayansi kutoka makao makuu ya DCI imetumwa katika eneo la tukio huko River Yala na hospitali ya Tala Sub County Level IV kusaidia uchunguzi zaidi," ilisema taarifa hiyo.