Uchambuzi: Matukio makuu ya makundi ya kigaidi mwaka 2022

Miezi 12 iliyopita imeshuhudia makundi ya wanajihadi yakipata hasara kubwa, hasa miongoni mwa uongozi wao, lakini pia kupata mafanikio ya kimaeneo katika Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambapo makundi hasimu yanapigania ushawishi na wanachama wapya.
Vita vya Ukraine na kuondolewa kwa wanajeshi wa nchi za Magharibi kutoka maeneo yenye wapiganaji wa jihadi, hasa katika eneo la Sahel barani Afrika, vimeonekana na wanajihadi kama fursa ya kupiga hatua wakati nchi za Magharibi "zimevurugika" barani Ulaya na kuondoka kutoka maeneo ya Waislamu yenye mizozo.
Kurejea kwa Taliban madarakani nchini Afghanistan mwaka 2021 ilikuwa wakati muhimu ambao makundi ya wanajihadi yanaonekana kutaka kuiga pengine, hata kama kwa kiwango kidogo.
Katika Sahel, kundi la Islamic State (IS) na al-Qaeda wanashindania ushawishi, na bila shaka wanapambana katika mchakato huo. Hasara iliyotokana na mapigano haya itakuwa kikwazo kwa matamanio yoyote ya upanuzi.
Uongozi wa wanajihadi na vikwazo vya kimaeneo vinaweza kuelezea kushindwa kwa kundi hili kupanga au kufanyamashambulizi katika nchi za Magharibi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, licha ya uchochezi unaoendelea - jambo ambalo uongozi wa IS ulitaja kwa masikitiko mwaka huu.
Wakati wa kuzingatia vitisho vikubwa vya wanajihadi mnamo 2023, mienendo ifuatayo ni muhimu:
- Juhudi za kuunganisha nguvu Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara.
- Ni matarajio ya IS kuwakomboa wanachama na familia zao walio kizuizini, haswa nchini Syria.
- IS hufanya mashambulia dhidi ya malengo rahisi nchini Afghanistan kama njia ya kudhoofisha mamlaka ya mpinzani wake, Taliban.
Kuwapoteza viongozi

Mwaka huu makundi mawili makuu ya wanajihadi duniani, IS na al-Qaeda, yalipoteza viongozi wao watatu kwa jumla - wawili katika operesheni za Marekani.
Viongozi wa IS Abu Ibrahim al-Hashimi al-Qurashi na Abu al-Hasan al-Hashimi al-Qurashi (hawana uhusiano) waliuawa nchini Syria mwezi wa Februari na labda mnamo Oktoba mtawalia.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kiongozi wa muda mrefu wa Al-Qaeda Ayman al-Zawahiri aliuawa katika shambulio la anga la Marekani katika mji mkuu wa Afghanistan Kabul tarehe 31 Julai.
Mauaji ya Abu Ibrahim na al-Zawahiri katika operesheni za Marekani yalizawadia utawala wa Biden mapinduzi ya sera za kigeni ambayo huenda yalisaidia kukabiliana na hali mbaya ya kujiondoa kwa ghasia nchini Afghanistan mwaka 2021.
Viongozi hao wasiojulikana wa IS Abu Ibrahim, ambaye aliteuliwa Oktoba 2019, na mrithi wake Abu al-Hasan, ambaye alitajwa kama mkuu mwezi Machi 2022, wote waliuawa bila kuwasilisha ujumbe wa aina yoyote wakati wa uongozi wao.
Kiongozi mpya aliyetangazwa na IS mnamo tarehe 30 Novemba, Abu al-Hussein al-Husseini al-Qurashi, anajiunga na safu hii ya viongozi wasio onekana.
Kiongozi wa kwanza wa IS Abu Bakr al-Baghdadi alikuwa mtu mashuhuri, licha ya kuonekana kwake kidogo. IS haijafichua habari zozote kuhusu utambulisho wa warithi wake watatu, kando na lakabu zao.
Ingawa IS na wafuasi wake wanaweza kudharau umuhimu wa sera hiyo, bila shaka ni changamoto kwa uaminifu wa kundi hilo.
Wanamgambo na wafuasi mara nyingi hupata kiburi na nguvu kutoka kwa sura ya viongozi - asili zao, mafanikio katika vita na sifa za kitaaluma. Bila hivyo, inaweza kuwa vigumu kuzalisha uaminifu na kujitolea.
Pia kuna suala la uhalali
IS inadai viongozi wake ni "makhalifa". Masharti mawili ya nafasi hii ni kwamba mwenye mamlaka anaweza kufuatilia nasaba yake hadi kwenye ukoo wa Mtume Muhammad - kwa hiyo jina "al-Qurashi", kwa kurejelea kabila la Quraish la Mtume; na kwamba hana ulemavu wowote wa kiakili au wa kimwili.
IS inawezaje kuthibitisha kuwa viongozi wake wanatimiza masharti haya wakati inakataa kuwatambua?
Al-Qaeda haijafanya vizuri zaidi.
Katika kipindi cha miezi minne tangu Marekani itangaze kifo cha al-Zawahiri, kundi hilo halijasema lolote kuhusu suala hilo. Lakini wakati huo, wafuasi wa ngazi za juu waliomboleza, wakionekana kuamini kifo chake, au angalau kuonyesha hivyo hadharani.
Kushindwa kwa Al-Qaeda kutaja mrithi - ucheleweshaji unachukizwa miongoni mwa wanajihadi kwani unaweza kusababisha "fitna" (migogoro ya ndani) - inaweza kuwa dalili ukosefu wa warithi wanaoaminika.
Naibu pekee wa Al-Zawahiri anayejulikana, Sayf al-Adl, anaaminika kuishi nchini Iran. Ikiwa ni hivyo, ni jambo lisilowazika kwamba kundi la wanajihadi wa Kisunni linaweza kuongozwa na mkazi wa nchi ya Kishia.
Wengi wa vigogo wa al-Qaeda wameuawa katika miaka ya hivi karibuni, na ndiyo maana al-Zawahiri mwenyewe alikuwa uso mkuu wa propaganda za al-Qaeda kabla ya kifo chake, mara nyingi kikiungwa mkono na kanda za kumbukumbu za watu waliofariki.
Sababu nyingine inayowezekana ya al-Qaeda kuchelewa kuthibitisha kifo cha al-Zawahiri ni uwezekano wa athari za kidiplomasia kwa Taliban, ambayo ilikanusha ufahamu awali.
Kwa ujumla, kushindwa kwa al-Qaeda kutaja mrithi na uteuzi wa mara kwa mara wa IS wa viongozi wasio onekana kunaashiria uhaba wa viongozi waliopo wa ngazi ya juu wa kijihadi wenye uwezo wa kutimiza majukumu haya ya juu.
Ushindani barani Afrika
Licha ya hasara zao za kimaeneo na uongozi katika Mashariki ya Kati na eneo la Afghanistan-Pakistani, IS na al-Qaeda zinaonekana kupata mafanikio katika Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambako wanatazamia maendeleo zaidi. Makundi hayo mawili ni maadui wakubwa katika maeneo haya na wamepania kutaka kuangamizana.
Wanajihadi wanatazamia kutumia machafuko ya kisiasa kwa mfano mapinduzi nchini Mali na Burkina Faso - na mivutano ya jumuiya kuimarisha uwepo wao, hasa katika maeneo ya mbali ambako serikali na huduma zake hazionekani sana.
Pia wanaangalia fursa zinazotokana na kupunguzwa au kuondolewa kikamilifu kwa wanajeshi wa kigeni wanaohusika katika oparesheni dhidi ya jihadi katika Sahel, haswa kuondoka kwa Wafaransa kutoka Mali mwaka huu.
Kubadilishwa kwa wanajeshi wa Operesheni ya Ufaransa ya Barkhane na mamluki wa Wagner wa Urusi nchini Mali huenda kuliongeza uwezo wa wanajihadi, ikizingatiwa sifa ya wapiganaji hao kwa mbinu katili dhidi ya wenyeji.
Ripoti kuu za vyombo vya habari kuhusu "mauaji" ya Wagner nchini Mali zinatumiwa sana katika propaganda za wanajihadi, haswa na al-Qaeda ambayo inadai kuwa inapigana kulinda raia kutoka kwa Wagner na jeshi.
Licha ya kuharibiwa kwa matawi yake huko Syria, Afrika Kaskazini (AQIM) na India" (AQIS), na mapambano ya kuendelea kuwepo kwa tawi lake la Yemen (AQAP), washirika wa al-Qaeda nchini Somalia (al-Shabab). na Sahel (JNIM) inaendelea kuwa tishio kubwa, kutokana na uhusiano wao wa ndani na jamii na makabila.

Chanzo cha picha, AFP
Mnamo Septemba, al-Qaeda ilitabiri kwamba al-Shabab, ambayo inadhibiti maeneo mengi katikati na kusini mwa Somalia, hivi karibuni itakuwa na nguvu za kutosha kuandamana Mogadishu na kuteka nchi nzima, katika hali iliyofananishwa na utekaji nyara wa Taliban nchini Afghanistan mwaka uliopita.
Wakati huo huo, tawi la Sahel la al-Qaeda, Jamaat Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM), ambalo viongozi wake wana mizizi katika jamii za Tuareg na Fulani nchini Mali, linaendelea kukua, likisaidiwa na msukosuko wa kisiasa katika eneo hilo na kuondolewa kwa wanajeshi wa Ufaransa.
Mwaka huu, JNIM imejaribu kutumia kuwasili kwa mamluki wa Kirusi Wagner nchini Mali kujionyesha kama "mtetezi" wa jumuiya za Kiislamu dhidi ya wavamizi wa kigeni, na imeongeza kwa kiasi kikubwa operesheni zake za kijeshi na vyombo vya habari.
Wakati huo huo, washirika wa IS wa Sahel, ambao walipewa hadhi ya kujitegemea kama tawi tofauti mwezi Machi, pia wamerekebisha operesheni yao nchini Mali na maeneo ya mpaka ya Burkina Faso.
Mwaka huu, IS ilidai mashambulizi yake ya kwanza katika Sahel huko Benin, ikitaja uvamizi wa Julai kama "upanuzi mpya" katika eneo hilo, ingawa shughuli zake huko zilitulia baadaye.
Lakini hadi sasa mnamo 2022, mashambulizi mengi ya IS katika Sahel yamekuwa yakilenga makundi hasimu, kama JNIM na wanamgambo wa Tuareg, huku kukiwa na mashambulizi machache tu dhidi ya Wagner na machache kwa vikosi vya kijeshi.
Mapigano ya wanajihadi katika Sahel yanatarajiwa kuendelea mwaka wa 2023, bila dalili za maelewano.
Hii hadi sasa imeepusha eneo hilo katika tishio lililoratibiwa zaidi na la kutisha la kijihadi, kwani vikundi vya wapiganaji vinatatizwa na juhudi za kumalizana.
Lakini ushindani huo hauwezi kusitisha ghasia, kwani makundi hayo mawili yanashindana mamlaka, picha na wanachama wapya, ambayo yanaweza kupatikana kupitia mashambulizi makali.
Kupanuka kwa IS barani Afrika
Mbali na Sahel, licha ya kushindwa kukuza uwepo wake nchini Somalia - hasa kutokana na uwepo wa mpinzani wake mwenye nguvu zaidi al-Shabab - IS mwaka huu imeongeza shughuli zake katika nchi kadhaa za Afrika.
Hasa, hii ilikuwa katika nchi ambazo al-Qaeda haina ngome, ambayo ni Nigeria, DR Congo na Msumbiji.
Mnamo mwaka wa 2022, tawi la IS la Jimbo la Afrika Magharibi (ISWAP) lilidai mashambulizi kwa mara ya kwanza katika maeneo ya Nigeria nje ya ngome yake ya jadi ya kaskazini-mashariki, ambayo IS ilidai kama kama "upanuzi wa ngome".
Pia mwaka huu, IS iliwapa washirika wake wa Msumbiji tawi huru, kama ilivyofanya Machi na washirika wake wa Sahel. Hii ilikuza wasifu wao kama matawi kwa haki yao wenyewe, na shughuli yao iliyoongezeka baadaye ilisisitiza hali hii mpya.
Miezi iliyopita ilishuhudia IS ikiongeza mashambulizi yake nchini Msumbiji, hasa dhidi ya Wakristo, na kudai "upanuzi" nje ya maeneo yake ya kitamaduni ya shughuli katika sehemu ya kaskazini ya jimbo la Cabo Delgado.
Kundi hilo pia limejigamba kuwa mashambulizi na vitisho vyake dhidi ya miradi ya nishati ya kigeni na uchimbaji madini na kulazimishwa kusimamishwa au kufungwa.
Jimbo la Afrika ya Kati (ISCAP) linalolengwa na IS nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (ISCAP) pia limekuwa mojawapo ya matawi hatari zaidi ya kundi hilo mwaka huu, na pia ni sehemu muhimu katika ujumbe wa IS kuhusu "upanuzi" wake wa Afrika pamoja na Msumbiji na Nigeria.
Mwezi Juni, IS ilitoa wito kwa msisitizo wa "Hijra" (uhamaji wa wanajihadi) hadi "Afrika Magharibi" - ujumbe ambao haijatoa kwa dharura yoyote tangu enzi zake za nchini Syria na Iraq.
Wito kama huo unasisitiza imani ya IS katika uwezo wake wa kuwakaribisha na kuwafunza wapiganaji wanaoingia na familia zao. Pia inapendekeza kwamba IS inaweza kuwa inaitazama Afrika kama msingi wa kujenga upya shughuli zake. Wito mwezi Juni kutoka kwa matawi ya IS nchini Syria Iraq – ngome za zamani za kundi hilo - kwa wafuasi kuelekea Afrika, uliimarisha mpango huu wa usajili wa IS.
Nchini Nigeria, DR Congo na Msumbiji, IS ina faida ambayo haifurahii katika Sahel na Somalia, ambapo inakabiliwa na wapinzani kama al-Qaeda.
Nchini Nigeria, kushindwa kwa mpinzani wake Boko Haram mwaka wa 2021 kunaonekana kuwa ni msukumo mkubwa kwa ISWAP katika suala la uandikishaji na ushawishi.
‘Kuvunja kuta'
Tangu 2019, wakati IS ilipopoteza ngome yake ya mwisho mashariki mwa Syria, uongozi wa IS umekuwa ukitoa wito kuvamia magereza ili kuwakomboa wafuasi wake.
Takriban jumbe zake zote za uongozi tangu wakati huo - ikiwa ni pamoja na jumbe mbili mwaka huu zimewaambia wanamgambo wa IS kwamba kuvamia magereza ni kipaumbele cha juu kwa kundi hilo.
Mnamo 2022, IS ilifanya uvamizi wa magereza mara tatu: moja huko Syria na mbili barani Afrika.
Wakati shambulio lake kali dhidi ya gereza la Ghuwayran, ambalo linawashikilia maelfu ya wafungwa wa IS, katika mkoa wa kaskazini-mashariki wa Hasaka nchini Syria mwezi Januari halikuweza kufikia lengo lake, ilikuwa ni mapinduzi ya propaganda muhimu kwa kundi la jihadi.
Uvamizi wa IS nchini Nigeria, karibu na mji mkuu Abuja, mwezi Julai na kaskazini-mashariki mwa DR Congo mwezi Agosti ulifanikiwa, na kuruhusu kundi hilo kuwakomboa mamia ya wafungwa katika kila tukio. Uongozi wa IS baadaye ungetaka wanachama wasiokuwa wa IS walioachiliwa katika uvamizi huu kujiunga na kundi hilo, kama njia ya kurudisha shukran.
Lakini zawadi halisi ambazo IS inazitarajia ni kambi za kizuizini zinazoendeshwa na Wakurdi kaskazini-mashariki mwa Syria, ambazo ni al-Hol na al-Roj, ambako maelfu ya wanawake na watoto wanaohusishwa na IS wanashikiliwa. Kuwepo katika kambi hizi za wanawake hasa wanaohusishwa na IS kunaendelea kuwa kidonda kwa heshima ya IS ambayo kundi hilo litakuwa na nia ya kuibadilisha.
Kundi hilo la kijihadi litakuwa likitazama kwa karibu matukio ya kisiasa kaskazini-mashariki mwa Syria, likitumai kutumia fursa yoyote kuvamia kambi na magereza, au angalau kuwatorosha baadhi ya wafungwa.
Operesheni za jeshi la Uturuki dhidi ya Wanajeshi wa Kidemokrasia wa Syria (SDF) wanaoongozwa na Wakurdi kaskazini mwa Syria ambapo kambi hizo zimejengwa zinaweza kutoa aina ya mapungufu ya usalama ambayo IS inatafuta.
Matukio Mengine
Kumekuwa na matukio kadhaa ya wanajihadi mwaka huu ambayo pia yalijitokeza na yanafaa kuzingatiwa wakati wa kuchunguza vitisho vya siku zijazo.
Kuongezeka kwa AQAP kusini mwa Yemen baada ya muda wa kutofanya tukio kwa zaidi ya miaka miwili, kunasisitiza uwezo wa kikundi wa kujipanga upya na kuboresha ngome zake.
Ongezeko la "Mishale ya Ukweli" la AQAP lililoanza mwezi Septemba lilikuwa jibu kwa kampeni ya kijeshi ya kukabiliana na ugaidi iliyofanywa na vikosi vya kujitenga vya kusini vinavyoungwa mkono na UAE, vilivyopewa jina la "Mishale ya Mashariki", yenye lengo la kuwafukuza wanajihadi kutoka majimbo ya kusini ya Abyan na Shabwa.
Tangu wakati huo AQAP imekuwa ikitaka kuyashinda na kuyachokoza makabila ya Sunni na wafuasi wa Muslim Brotherhood dhidi ya vikosi vya kusini, ikionyesha "njama" inayoungwa mkono na Magharibi ya kuigawa Yemen na kudhoofisha maadili ya Waislamu.
AQAP ilibadilisha haraka vyombo vyake vya habari ili kuakisi ongezeko hili, na kuzindua kampeni ya "Mishale ya Ukweli" yenye chapa yake maalum ili kuonyesha shughuli zake za kusini.
Wakati huo huo, shambulio la Oktoba 28 katika eneo la madhabahu katika mji wa Shiraz kusini mwa Iran, ambalo lilidaiwa na IS, lilipongezwa na vyombo vya habari rasmi vya kundi hilo kama mfano wa hali yake kama "kikosi pekee" kilicho tayari kushambulia nguvu ya Shia nchini Iran.
Uandaaji wa Qatar wa Kombe la Dunia la Fifa mnamo Novemba ulivutia shutuma rasmi kutoka kwa al-Qaeda na IS. Vikundi hivyo vilionya kwamba tukio hilo lilileta "makafiri" ambao "waliichafua" "ardhi takatifu ya rasi ya Arabia" na kuendeleza maadili yasiyo ya Kiislamu.
Huko Afghanistan, vita vilivyotangazwa na IS dhidi ya Taliban huenda vikaendelea 2023.
"Mkoa wa Khorasan" unaolengwa na Afghanistan (ISKP) umelenga wanachama wa Taliban, dini ndogo, na shabaha za kigeni kama vile balozi za Urusi na Pakistani na hoteli inayotembelewa na raia wa China, kama njia ya kuwadharau watawala wa Afghanistan.
Pia mwaka huu, IS ilidai mashambulizi mawili ya kuvuka mpaka dhidi ya nchi jirani za Uzbekistan na Tajikistan, uwezekano wa kudhoofisha ahadi za Taliban za kuzuia wanajihadi kutumia ardhi ya Afghanistan kufanya mashambulizi.
Mwisho kabisa, kikundi cha wanajihadi chenye makao yake nchini Syria Hayat Tahrir al-Sham (HTS) kimeendelea kujaribu kujiunda upya kama mradi wa kisiasa wa wastani na halali ambao umetikisa uhusiano wake wa kihistoria na al-Qaeda.
Kiongozi wa kundi hilo Abu Muhammad al-Jawlani mwaka huu alikutana na waumini wa dini ndogo huko Idlib, ngome ya HTS, akitoa ujumbe wa kutia moyo kuhusu uhuru wa kidini. Pia alionekana akihudhuria hafla za umma, pamoja na maonyesho ya vitabu na sanaa.
HTS huenda ikaendeleza juhudi zake za upanuzi mwaka wa 2023, ambao mafanikio yake yatategemea sana hatua za kisiasa na kidiplomasia za Uturuki nchini Syria mwaka ujao. Kulikuwa na dalili za maelewano ya Uturuki na serikali ya Syria katika sehemu ya mwisho ya mwaka 2022.
Iwapo harakati hizo za kidiplomasia zitaunganishwa, kuna uwezekano wa kuwa na athari mbaya kwa hali ya makundi ya waasi, ikiwa ni pamoja na HTS, kaskazini mwa Syria.














