Operesheni ya siri ya "Ghadhabu ya Mungu" ambayo Israeli ililipiza kisasi vifo vya wanariadha wake Munich

Kwa kuandaa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya joto ya 1972, Ujerumani ilitaka kuuonyesha ulimwengu kuwa ilikuwa nchi tofauti sana na ile ya 1936, wakati Adolf Hitler alipofungua Olimpiki yenye utata huko Berlin ambapo alitaka kuonyesha "ubabe wa Ujerumani."

Hata hivyo, miaka 50 baadaye, wengi wanakumbuka zaidi michezo iliyofanyika Munich kwa janga lililowakumba, kuliko matukio ya michezo.

Mnamo Septemba 5 mwaka huo, saa 4 asubuhi, watu wanane wenye silaha, wanachama wa kundi la Palestina la Black September, waliruka uzio wa senyenge wenye urefu wa futi sita na kuingia ndani ya vyumba vya wanariadha wa Israeli katika Kijiji cha Olimpiki huko Munich.

Saa 4:25 asubuhi, washambuliaji hao walitumia ufunguo 'inayoweza kufungua sehemu nyingi kufungua kufuli la mlango na kutumia ushoroba wa kuelekea kwenye vyumba vya wachezaji.

Baada yakuingia kukawa na makabiliano kati yao na baadhi ya wanariadha, ambapo wanamgambo hao wa Kipalestina waliwaua wawili na kuwateka wanamichezo tisa wa Israel na makocha.

Ili kuwaachilia wanamichezo hao, washambuliaji hao walitaka kuachiliwa kwa zaidi ya wafungwa 200 wa Kipalestina waliokuwa wametekwa na Israel na kuwahamisha mateka hao hadi kwenye uwanja wa ndege mjini humo, ambapo vikosi vya usalama vya Ujerumani Magharibi vilijaribu kuwaokoa.

Lakini mpango wa uokoaji haukufaulu na mauaji yakatokea, wanamichezo hao tisa wa kamati ya Olimpiki ya Israeli na afisa mmoja wa polisi wa Ujerumani Magharibi, pamoja na washambuliaji watano kati ya wanane waliokuwa na bunduki.

Wengine watatu, waliotambuliwa kwa jina la Adnan Al-Gashey, Jamal Al-Gashey, na Mohammed Safady, walikamatwa na polisi wa Ujerumani, ambao waliwaachilia baada ya ndege ya shirika la ndege la Ujerumani Lufthansa kutekwa nyara katika mabadilishano ya kuokoa maisha.

Baada ya kuachiliwa, watu hao watatu walihamishiwa Libya, ambako walipokelewa na Muammar Gaddafi kama mashujaa, kwa mujibu wataalamu.

Katika miezi kadhaa iliyofuata, wengi wa wanachama wa kundi la Black September walioshiriki katika kuandaa mauaji ya Munich waliuawa.

Idara ya ujasusi ya Israel inadaiwa kuhusika na mauaji hayo, katika kile ambacho kingekuwa sehemu ya operesheni ya siri inayojulikana kama "Ghadhabu ya Mungu".

Ni mmoja tu wa washambuliaji, Jamal Al-Gashey, aliyenusurika na hadi mwishoni mwa miaka ya 1990 bado alidhaniwa kuwa anaishi mafichoni.

Israel pia imeshutumu mamlaka za Ujerumani Magharibi kwa kushindwa kutoa usalama wa kutosha katika Michezo hiyo, kulingana na nyaraka rasmi za Israel ambazo zilifichuliwa miaka kumi iliyopita.

Michezo iliendelea siku moja baada ya shambulio hilo. Mwaka huo, jedwali la medali lilitawaliwa na Muungano wa Kisovieti, ambao ulikuwa na medali 50 za dhahabu, huku Marekani ikimaliza ya pili kwa 33 na Ujerumani Mashariki ya tatu kwa kuwa na medali 20.

"Ghadhabu ya Mungu"

Muda mfupi baada ya mkasa huo, Waziri Mkuu wa wakati huo wa Israel, Golda Meir, alitangaza kupitia bunge "vita dhidi ya ugaidi". Aliunda kamati ya siri kubaini waliohusika na shambulio hilo na kuagiza Mossad, moja ya mashirika ya kijasusi ya Israel, kuwatafuta na kuwaua, kulingana na mwandishi wa BBC Fergal Keane katika makala yake kuhusu shirika la Israel iliyochapishwa mwaka wa 2014.

Mike Harari, mmoja wa majasusi mashuhuri wa Israel, alisimamia "kampeni hii ya kulipiza kisasi" ambapo zaidi ya Wapalestina kumi waliuawa.

Katika moja ya mashambulizi ya Israel, kundi la mawakala wa Mossad, ambao baadhi yao walikuwa wamevalia kama wanawake, waliingia kwa boti za torpedo kwenye ukingo wa bahari wa Beirut, mji mkuu wa Lebanon, na kuwaua viongozi watatu wa Shirika la Ukombozi wa Palestina (OLP), na wanachama wengine wa kundi la wanamgambo.

Katika uingiliaji kati huu, sehemu ya kampeni ya 'Ghadhabu ya Mungu', raia kadhaa wa Lebanon na Palestina na mawakala wawili wa Israeli pia waliuawa.

Malengo makuu ya Operesheni ya 'Ghadhabu ya Mungu' yalikuwa kuleta haki kwa familia zilizoathiriwa na kuuonyesha ulimwengu kwamba Israeli haingeruhusu kuadhibiwa kwa uhalifu dhidi ya raia wake, anasema Michael Brenner, profesa wa Historia na Utamaduni wa Kiyahudi katika Chuo Kikuu wa Israeli.

Munich, katika mahojiano na BBC Mundo. "Mambo mawili yalijitokeza kwa pamoja: asili ya uhalifu wakati wa Michezo ya Olimpiki na ukweli kwamba mamlaka ya Ujerumani iliwaachilia magaidi watatu walionusurika wiki chache tu baada ya kukamatwa," anaongeza mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Israeli katika Chuo Kikuu cha Amerika. (Washington DC).

"Maangamizi 50"

Akiwa ziarani nchini Ujerumani mwezi Agosti, Rais wa Palestina Mahmoud Abbas alikataa kuomba radhi kwa mauaji ya Munich na badala yake aliishutumu Israel kwa kufanya "maangamizi 50 ya mauaji" katika mkutano na waandishi wa habari mjini Berlin pamoja na kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz.

"Ikiwa tunataka kuingia ndani zaidi katika siku za nyuma, nina orodha ya mauaji 50 yaliyofanywa na Israeli," kiongozi wa Palestina alijibu baada ya kuulizwa na mwandishi wa habari wa Ujerumani ikiwa alipanga kuomba msamaha kwa shambulio la Munich lililotokea miaka 50 iliyopita.

"Mauaji ya halaiki 50 na hadi leo, kila siku, tuna watu waliouawa na jeshi la Israeli," Abbas aliongeza.

Hisia ya ukosefu wa haki

Mwanahistoria Michael Brenner anabainisha kuwa kumekuwa na mijadala mingi kuhusu jinsi ya kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 50 ya mauaji ya Munich kwa sababu, baada ya mauaji hayo, Ujerumani ilienda kinyume na "inacyhopaswa kitaalamu" katika kujaribu kutatua mgogoro huo.

"Na bado kuna hisia ya ukosefu wa haki kati ya familia za walioathiriwa," anaongeza Brenner.

Ndugu wa wanariadha wa Israel waliouawa mjini Munich mwaka 1972 walitangaza mapema mwezi Agosti kwamba watasusia sherehe za kuadhimisha miaka 50 ya janga hilo kutokana na mzozo na serikali ya Ujerumani kuhusu fidia, ambayo kiasi chake hakikuwekwa wazi.

"Hatutaenda kwenye ibada ya kumbukumbu hadi Ujerumani ichukue jukumu la kweli, sio maneno tu," Ankie Spitzer, ambaye mume wake aliuawa katika shambulio hilo, aliiambia Reuters.

Kwa mujibu wa ripoti katika gazeti la The Times of Israel, Ujerumani ilizipa familia hizo takriban dola milioni 2 mara tu baada ya mauaji hayo na kwamba mnamo 2002 iliwapa euro milioni 3 zaidi.

Baada ya wiki kadhaa za mazungumzo yenye mvutano, hatimaye Ujerumani ilikubali Jumatano iliyopita, siku tano tu kabla ya maadhimisho ya miaka 50 ya mauaji hayo, kutoa euro nyingine milioni 28 kama dola milioni 28 kwa familia za wanariadha kama fidia.

Rais wa Israel Isaac Herzog mara moja alikaribisha mpango huo, na kuuita "hatua muhimu ya serikali ya Ujerumani."