Vinicius jr: Mfahamu mchezaji wa Real Madrid aliyezua mjadala wa ubaguzi wa rangi Uhispania

Na Abdalla Seif Dzungu

BBC Swahili

Ubaguzi wa rangi katika soka ni suala la aibu ambalo limeathiri mchezo huo mzuri kwa miaka mingi na, ingawa kumekuwa na dalili za kuimarika, wanasoka katika ligi kote ulimwenguni na katika kandanda ya kimataifa wamekuwa wakikabiliwa na unyanyasaji wa kuchukiza.

Lakini picha za kutisha za nyota mwenye kipawa wa Brazil Vinicius Jr akibubijikwa na machozi zimesisitiza umuhimu wa kupambana na jinamizi hilo katika ligi ya LaLiga na ligi nyengine nyingi duniani.

Mshambuliaji huyo wa Real Madrid alikejeliwa na kelele za 'nyani' za udhalilishaji na za kibaguzi kutoka katika uwanja wa soka wa Mestalla Stadium huko Valencia Jumapili jioni katika tukio ambalo linapaswa kuwashtua wakuu wa LaLiga.

Vinicius ni mwanasoka mwenye kipawa cha hali ya juu ambaye amekuwa akikabiliwa na kampeni ya muda mrefu ya unyanyasaji wa ubaguzi wa rangi ambayo imekuwa ikitanda katika viwanja vya soka vya Uhispania. Lakini mechi ya Jumapili usiku ilikuwa kilele cha unyanyasaji huo wa muda mrefu wa mechi za ugenini za Real Madrid ambapo LaLiga wamelazimika kuripoti uhalifu wa chuki dhidi ya fowadi huyo kwa mahakama za Uhispania.

Unyanyasaji huo kutoka kwa mashabiki wa Valencia uligonga vichwa vya habari kwa sababu mchezaji huyo alimuonesha refa mashabiki ambao aliwaona na kusikia wakitoa dhihaka hizo.

Mechi hiyo ililazimika kusitishwa katika kipindi cha pili huku Vinicius aliyekasirishwa akiwaripoti mashabiki wa upinzani kwa mwamuzi.

Na baada ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 kutolewa kwa kadi nyekundu kwa kuzua ghasia, alisema: "La Liga ni ya wabaguzi."

Uwanja mzima ulikuwa ukipiga kelele za kibaguzi -Ancelotti

Ancelotti alisema: "Tulichoona leo hakikubaliki - uwanja mzima uliimba maneno ya kibaguzi.

“Sitaki kuzungumzia soka leo, hakuna maana kuzungumzia soka leo, nilimwambia mwamuzi alipaswa kusimamisha mechi.

"La Liga ina tatizo. Kwangu mimi Vinicius ndiye mchezaji muhimu zaidi duniani. Vipindi hivi vya ubaguzi wa rangi lazima visimamishe mechi.

"Ni uwanja mzima ambao unamtusi mchezaji kwa nyimbo za kibaguzi na mechi lazima ikome. Ningesema vivyo hivyo kama tungekuwa tunashinda 3-0. Hakuna njia nyingine."

Lakini rais wa La Liga, Javier Tebas alijibu kwenye mtandao wa Twitter kwa kusema Vinicius hakufika mara mbili katika mkutano wa kujadili kile "inachoweza kufanya katika kesi za ubaguzi wa rangi", na kuongeza: "Kabla ya kuikosoa na kukashifu La Liga, unahitaji kujijulisha ipasavyo. "

Lakini mkuu wa shirikisho la kandanda Luis Rubiales alisema soka la Uhispania lilikuwa na "tatizo kubwa ambalo pia linatia doa timu nzima, kundi zima la mashabiki, klabu nzima na nchi nzima".

Lakini Vinicius Jr ni nani?

Wakati kocha wa Real Madrid wakati huo Zinedine Zidane alipotakiwa kuwapatia nafasi wachezaji chipukizi katika klabu ya Real Madrid wengi walijiuliza kuhusu wachezaji ambao walikua na umahiri wa kuchkua nafasi hizo na jina la Vinicius Junior halikuwachwa nyuma.

Akilinganishwa na wachezaji wengine bora wa kandanda, Vinicius ni miongoni mwa nyota wa mchezo huo akifananishwa na Neymar na Kylian Mbape.

Vinícius José Paixão de Oliveira Júnior kama anavyoitwa alizaliwa tarehe 12 Julai 2000). Ni mchezaji wa soka la kulipwa ambaye anacheza kama winga katika klabu ya Liga ya Real Madrid na timu ya taifa ya Brazil .

Anajulikana kwa kasi yake, uwezo mkubwa wa kuchenga, na ustadi wa kucheza.

Kulingana na mtandao wa Wikipedia ,akiwa mzaliwa wa huko São Gonçalo, Vinícius alianza taaluma yake ya kusakata soka katika klabu ya Flamengo, ambapo alicheza mwaka wa 2017, akiwa na umri wa miaka 16.

Wiki chache baadaye, Vinícius alikuwa alihamia katika klabu ya La Liga Real Madrid, ambapo aliweka mkataba wa pauni milioni 38, ikiwa rekodi ya kitaifa kwa mchezaji wa chini ya umri wa miaka 18.

Kufikia msimu wake wa nne, Vinícius alikuwa amejiimarisha kama mshiriki mashuhuri katika kikosi cha kwanza cha Real Madrid, akiisaidia klabu hiyo kushinda taji la La Liga la 2021-22 na kufunga bao la ushindi katika ushindi wa Real Madrid katika fainali ya UEFA 2022.

Katika hatua yake ya ujana kwa Brazil, alikuwa mchezaji muhimu katika ushindi wa Mashindano ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 15 wa Amerika ya kusini ya ya 2015 na Mashindano ya wachezaji wasiozii umri wa miaka 17 ya Amerika Kusini ya 2017, akimaliza kama mfungaji bora katika mashindano ya mwisho.

Alianzishwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 2021 na alisaidia taifa lake kumaliza katika nafasi ya pili kwenye kombe la Copa América la 2021 na akawawakilisha kwenye Kombe la Dunia la FIFA la 2022 nchini Qatar.

Mtindo wake wa kucheza

Muda mfupi baada ya kuwasili Real Madrid mnamo Julai 2018, mwandishi wa habari wa ESPN Dermot Corrigan alimuelezea Vinícius kama "winga wa kushoto au mshambuliaji wa pili".

Mchezaji hodari, ambaye ingawa mara nyingi hupangwa upande wa kushoto, ana uwezo wa kucheza popote kwenye mstari wa mbele, na pia amekuwa akitumika kulia au katikati.

Ana kasi, ni mwepesi, ana ustadi wa kuteleza, na udhibiti wa karibu kwa kasi, na vile vile nguvu kubwa licha ya umbo lake dogo.