Uamuzi mbaya unaathiri 'kazi na sifa' - Kocha wa Wolves Gary O'Neil baada ya kushindwa na Fulham

Kocha wa Wolves Gary O'Neil amesema maamuzi mabaya ya waamuzi yanaathiri "sifa" na "kazi" baada ya timu yake kupata kipigo cha 3-2 Jumatatu dhidi ya Fulham.

O'Neil alisema mwamuzi Michael Salisbury alisema uamuzi wa kutoa penalti ya kwanza kati ya mbili dhidi ya Wolves ulikuwa wa makosa, na anaamini maamuzi manne makubwa yalikwenda kinyume na wageni.

"Labda usiku wa leo hatimaye imenifanya niipinge VAR," O'Neil aliiambia Sky Sports.

"Athari mnazopata kuhusu sifa yangu, na klabu ni kubwa. Tunapaswa kuwa na uwezo wa kuzungumzia mchezo na sio maamuzi, lakini kwa bahati mbaya hatuwezi.

"Nafikiri ni [suala] tata sana. Nimekuwa nikiitumia mara kwa mara VAR lakini nadhani inaleta matatizo kwa sasa. Nafikiri VAR imetugharimu."

Adhabu tatu zilitolewa Jumatatu usiku. La kwanza lilisaidia Fulham kuongoza 2-1 baada ya Nelson Semedo kumshika Tom Cairney katika eneo hilo.

VAR ilidumisha uamuzi wa Salisbury kutoa mkwaju wa penalti, baada ya kuamua kuwa Semedo aligusa mpira alipokuwa akiwasiliana na Cairney.

La pili lilijiri dakika 15 baadaye huku Tim Ream akimshika Hwang Hee-chan wa Wolves ambaye alifunga na kufanya matokeo kuwa 2-2.

Fulham waliondoka na alama zote tatu kwenye dakika za nyongeza kupitia mkwaju wa penati ya pili ya Willian ambayo ilikuwa penati ya pili kati ya tatu zilizotolewa kwenye mchezo huo.

Hapo awali, Salisbury aliruhusu mchezo uendelee wakati Harry Wilson na Joao Gomes walipokutana kwenye eneo la hatari, lakini alibadili maamuzi yake na kutoa penalti baada ya VAR kumshauri aangalie skrini ya pembeni mwa uwanja.

Kwingineko, mchezaji wa Fulham Carlos Vinicius alioneshwa kadi ya njano baada ya kumgusa puani na kwenye paji la uso Max Kiliman wa Wolves kwa mguu wake.

"Tumejadili maamuzi mengi. Vinicius alipaswa kutolewa kwa kumpiga kichwa Max [Kilman]," aliongeza O'Neil. "Ream alipaswa kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la pili la adhabu. Ni maoni yangu.

"Nelson [Semedo] anacheza mpira na hakumgusa Cairney. Mwamuzi anasema alihisi hilo lilikuwa kosa.

"Kwa hiyo huyo amekiri kwamba lilikuwa kosa. Lile la Wilson hatukubaliani nalo. Ninahisi lilikuwa kosa dogo. Kwa maamuzi yote manne ya kwenda kinyume na sisi ni ngumu kukubaliana na hatukustahili hilo."

Wolves yaendelea kuathirika na maamuzi yenye utata

Ilipocheza na Manchester United katika mchezo wa kwanza wa ligi kuu Wolves walinyimwa penati katika dakika za mwisho licha ya mlinda lango wa United Andre Onana kumfanyia madhambi Sasa Kalajdzic. Timu hiyo ya magharibi mwa Midlands baadaye iliombwa radhi na Bodi ya wanataaluma wa uamuzi (PGMOL).

Mwezi Septemba kiungo wa zamani wa Ligi Kuu ya England, Danny Murphy alisema uamuzi wa wa kuipa Luton mkwaju wa penati wakati wa sare dhidi ya Wolves ulikuwa “mojawapo ya uamuzi mbaya zaidi msimu huu”.

O'Neil alisema mwezin Oktoba “ilikuwa ni kashfa” VAR haikuingilia kati wakat Hwang alipoadhibiwa kwa kumchezea madhambi Fabian Schar wakati was are ya 2-2 dhidi ya Newcastle.

Na kabla ya mapumziko kupisha michezo ya kimataifa Wolves iliadhibiwa kwa mkwaju wa penati katika dakika za lala salama ilipofungwa 2-1 na Sheffield United, tukio ambalo kocha O'Neil alilita "kosa kubwa" wakati akizungumza kwenye kipindi cha BBC cha Match of the Day.

"Ni bahati mbaya kwamba inaendelea kutokea dhdidi yetu," aliongeza O'Neil baada ya ya kikosi chake kupotea mbele ya Fulham. "Kuna maamuzi mabaya ya uamuzi, nilikuwa na mazungumzo ya kiutu uzima na yeye [mwamuzi Salisbury]. Sina hasira na na watu.

"Nina machaguo mawili – tuendelee kuwa na mwenendo kama inavyotupasa na kuheshimu maamuzi na kuwaambia wachezajia kufanya vivyo hivyo, au tuanze kusema kuwa hili si sawa kwetu na kupiga kelele. Ni bora niwe mtu muungwana pia mkweli, lakini haiwezekani hali hii iendelee dhidi yetu.

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Florian Kaijage.