Kenya ya vifo na kumwaga damu mpaka lini?

    • Author, Yusuph Mazimu
    • Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

"Wakati mwingine naangalia kinachoendelea kwenye TV (maandamano), machozi hunidondoka," anasema Crispine Odawa, baba mzazi wa Rex Masai, mmoja wa vijana waliouawa kikatili kwenye mfululizo wa maandamano nchini Kenya. Kauli yake, iliyojaa uchungu usioelezeka, inawakilisha kilio cha wengi.

Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, maandamano nchini Kenya yamekuwa sehemu ya maisha ya kawaida ya wananchi, lakini sasa yamegeuka kuwa chemchemi ya machozi, huzuni isiyo na kikomo, na majonzi mazito. "Inauma sana... unapojaribu kupona, halafu linatokea bomu jipya," anasema Gillian Munya, mama wa Rex, akielezea jeraha lisilopona. Wazazi hawa walihojiwa na DW.

Kilio hiki cha kuumiza, na uchungu wa kupoteza mtoto, ndugu, na jamaa, kimetawala kwa mamia ya familia, na maelfu wakiomboleza majeruhi mabaya, wengine wakiwa wamejeruhiwa vibaya kwa risasi wakati wa maandamano.

Kila mara wananchi, hasa vijana, wanapoingia mitaani kuandamana, taifa huingia katika hali ya taharuki kubwa, huku taarifa za umwagaji damu kwa vifo vya kutisha, majeruhi ya kudumu, na uharibifu mkubwa wa mali zikiripotiwa.

Mwaka huu, maadhimisho ya kumbukumbu ya harakati za kupigania mageuzi ya kisiasa, Saba Saba, ya Julai 7, 2025, yamezidi kutonesha vidonda, wengi wa waandamanaji wakionyesha hali ya kutoridhika dhidi ya serikali ya Rais William Ruto.

Tangu kuingia madarakani kwa utawala wa Ruto mwaka 2022, kumekuwa na ukinzani mkubwa kutoka kwa vijana, ukinzani unaokwenda sambamba na maandamano ya kila mara yanayosababisha vifo na umwagaji wa damu usio na kikomo.

Swali hapa, Je, Kenya ya vifo na kumwaga damu mpaka lini?

Maandamano ya damu na kwanini?

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Kenya imeingia katika mzunguko wa maandamano yaliyojaa umwagaji damu, vifo, na ghasia za kila namna. Tangu mwaka 2023, kumekuwa na maandamano yanayoendana na makabiliano na Polisi, na kusababisha vifo na vitokanavyo na risasi.

Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binadamu la IMLU, watu 67 waliuawa kati ya Januari na Septemba 2023 pekee, katika maandamano 22 yaliyopinga gharama ya maisha.

Mnamo Juni 2024, hasira ya wananchi dhidi ya Mswada wa Fedha iliibuka tena. Tarehe 25 Juni 2024, siku ya kilele cha maandamano hayo, watu 60 waliuawa wengi wao kwa kupigwa risasi na vikosi vya usalama. Serikali baadaye ililazimika kuondoa mswada huo kufuatia shinikizo kubwa.

Lakini hata baada ya serikali kurudi nyuma, damu iliendelea kumwagika. Tarehe 8 Juni 2025, mwanablogu kijana Albert Ojwang aliuawa akiwa mikononi mwa polisi. Kifo chake kiliibua maandamano mengine tarehe 17 Juni, ambapo mtu mmoja aliuawa jijini Nairobi. Tarehe 25 Juni 2025, waandamanaji waliingia tena mitaani kuwakumbuka wale waliouawa mwaka mmoja kabla. Katika maandamano hayo, watu 16 walipoteza maisha.

Wiki chache baadaye, tarehe 7 Julai 2025, maadhimisho ya miaka 35 ya Sabasaba yakageuka kuwa siku ya damu tena. Vijana wa Gen-Z waliingia mitaani, wakifunga barabara na kushinikiza serikali kuondoka madarakani. Katika vurugu hizo, watu 11 waliuawa katika maandamano hayo yaliyofanyika katika maeneo kadhaa nchini humo.

Kwanini Polisi inatupiwa lawama?

"Maandamano kila wakati yanarudisha machungu. Tulidhani kifo cha Rex kingekuwa cha kwanza na cha mwisho. Bahati mbaya, Juni 25 serikali iliua watu wengi zaidi," anasema mwanaharakati Boniface Mwangi, mwanaharakati

Idadi ya wanaokufa kwenye maandamano inaendelea kuongezeka kila wakati huku polisi wakituhumiwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi.

Kauli ya Murkomen inazidi kuwaumiza familia ambazo tayari zimepoteza wapendwa wao kwa mikono ya polisi, huku polisi wanaeleza wanatekeleza majukumu yao ya kulinda watu na mali zao.

Mwezi Juni 2025, Waziri wa usalama wa ndani, Kipchumba Murkomen alitoa kauli iliyozua taharuki na ghadhabu mitaani. Akizungumza mbele ya waandishi wa habari, alisema: "Tunawaambia polisi kuwa mtu yeyote ambaye atakaribia kituo cha polisi, piga yeye risasi."

Licha ya kusema kauli hiyo imetafsiriwa tofauti, ilizua ghadhabu kubwa mitandaoni na mitaani. Baadhi ya wananchi wakimjibu mtu asiuawe bali akamatwe: "Ashikwe, asiuawawe wacha wewe!"

Wanaharakati na mashirika ya haki za binadamu walikemea kauli hiyo wakisema inawapa polisi ruhusa ya kutekeleza mauaji kiholela, jambo linalokiuka misingi ya katiba na haki za kibinadamu.

Kiongozi wa upinzani nchini humo, Raila Odinga, akizungumza kuhusu vifo vya vijana hasa waandamanaji anasema: "Tumerithi jeshi la polisi lenye mfumo wa kikoloni. Tunahitaji kulibadili jeshi hili liwe la kutoa huduma, si kutumia nguvu kwa wananchi. Haitoshi kubadili jina kutoka 'Force' kwenda 'Service'. Polisi wanapaswa kuwatendea watu kwa utu."

Mdahalo wa kitaifa suluhisho?

Katika kile kinachoonekana kama hatua ya kutafuta suluhu ya kitaifa, kiongozi wa upinzani aliyepoteza katika uchaguzi wa 2022, Odinga, anapendekeza kuwepo kwa mdahalo wa kitaifa na yeye yuko tayari kushiriki mdahao huo na Rais William Ruto.

Odinga amesema kuwa ni muhimu kwa taifa kuzungumza na kutafuta njia ya kuondokana na hali hii ya maumivu na vifo visivyokoma. Katika kauli yake ya karibuni, alisema: "Napendekeza kikao cha kitaifa kitakachowakutanisha Wakenya wa vizazi vyote, ili kusikiliza kilio cha watu wetu na kuja na mageuzi yasiyoweza kupingwa yatakayolifikisha taifa letu mbele."

Lakini kwa vijana waliopoteza marafiki, na ndugu, wazazi waliowapoteza watoto, na taifa lililoshuhudia damu ikimwagika kila mwaka, pendekezo hilo linaonekana kuchelewa.

Wengi wanasisitiza: "Ruto must go" (Ruto aachie madaraka) na si mdahalo, si maneno, bali hatua.

Msimamo wake huo pia umekosolewa na baadhi ya wafuasi wake na wanasiasa waliomwona kama sauti ya wanyonge. Wengi wanahisi kuwa amewasaliti kwa kukubali kushirikiana na serikali ambayo imekosa kusikiliza kilio cha wananchi.

Hoja hapa , je, mdahalo huu utazaa matunda ya kweli au ni njia nyingine ya kisiasa ya kunyamazisha harakati za wananchi? au itasalia swali lile lile: Kenya ya vifo mpaka lini?