Alien Enemies Act: Ifahamu sheria ya mwaka 1798 anayoitumia Trump kuwafukuza wahamiaji

    • Author, Sofia Ferreira Santos
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Zaidi ya raia 200 wa Venezuela, ambao Ikulu ya Marekani inadai ni wanachama wa magenge, wamefukuzwa Marekani na kupelekwa katika jela kubwa maarufu nchini El Salvador.

Kati ya watu 261 waliofukuzwa, 137 walifukuzwa chini ya Sheria ya dharura ya Maadui Wageni, amesema afisa wa ngazi ya juu wa Marekani kwa CBS News.

Sheria hii iliopo kwa karne nyingi ndio imetumiwa na Rais Donald Trump. Amelishutumu genge la Venezuela la Tren de Aragua (TdA) kwa "kujaribu, kutishia na kufanya uvamizi katika ardhi ya Marekani.

Mahakama ya chini ilizuia kwa muda uhamishaji huu tarehe 15 Machi, ikisema hatua hizi za utawala zinahitaji kuchunguzwa zaidi chini ya sheria.

Lakini katika uamuzi wa tarehe 7 Aprili, Mahakama ya Juu iliondoa kizuizi hicho, ikiegemea upande wa Trump huku pia ikiamuru kuheshimiwa haki za watu.

Pia unaweza kusoma

Sheria inasemaje na imetumika?

Sheria ya Maadui Wageni inampa rais wa Marekani mamlaka makubwa ya kuamuru kuwekwa kizuizini na kufukuzwa kwa wenyeji au raia wa taifa "adui" bila kufuata taratibu za kawaida.

Ilipitishwa kama sehemu ya msururu wa sheria mwaka 1798 wakati Marekani, ilipoona itaingia vitani na nchi ya Ufaransa.

Sheria hiyo inasema "wakati wowote vita vikitangazwa [...] au kukiwa na jaribio, tishio au kufanyika uvamizi wowote" dhidi ya Marekani, "watu wote wa taifa au serikali yenye uadui" wanaweza "kukamatwa, kuzuiwa, na kuondolewa, kama maadui wageni."

Sheria hiyo imetumika mara tatu pekee – nyakati tatu za mzozo unaohusisha Marekani.

Ilitumiwa mara ya mwisho wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, pale watu wa asili ya Japan - wanaoripotiwa kufikia 120,000 - walipofungwa gerezani bila kesi. Maelfu walipelekwa kwenye kambi za wafungwa.

Watu wa asili ya Ujerumani na Italia pia waliwekwa ndani wakati huo.

Kabla ya hapo, sheria hiyo ilitumika wakati wa Vita vya mwaka 1812 na Vita vya Kwanza vya Dunia.

Madai ya Trump

Ingawa hii ni mara ya kwanza kwa sheria hii kutumiwa na Trump, lakini si mara ya kwanza kuitaja.

Katika hotuba yake ya kuapishwa mwezi Januari, alisema atatumia sheria hiyo "kuondoa magenge yote ya kigeni na mitandao ya uhalifu inayoleta uhalifu katika ardhi ya Marekani."

Katika tangazo lake siku ya Jumamosi, Trump alitumia maneno ya sheria hiyo kwa kulishutumu genge la TdA kwa kutishia "kuivamia" Marekani. Alitangaza wanachama wake "wanastahili kukamatwa, kuzuiwa, na kuondolewa kama maadui wageni."

Uamuzi huo wa Trump umekosolewa na makundi ya kutetea haki za binadamu. Muungano wa Uhuru wa Kiraia (ACLU), ulipeleka kesi mahakamani kuzuia kufukuzwa watu kwa misingi kwamba Marekani haiko vitani.

Akizungumza na BBC News Jumapili, Lee Gelernt, wakili wa ACLU, alisema: "Hakuna shaka akilini mwetu kwamba sheria hii inatumika vibaya."

Venezuela imekosoa matumizi ya sheria hiyo, ikisema "inaharamisha uhamiaji wa Wavenezuela isivyo haki" na "inakumbushia matukio mabaya katika historia ya binadamu, kutoka utumwa hadi kambi za mateso za Nazi."

Katherine Yon Ebright, wakili katika Kituo cha Haki cha Brennan, alisema katika taarifa kwamba matumizi ya Trump ya Sheria hii ni kinyume cha sheria.

"Sababu pekee ya kuchukua hatua kama hayo ni kujaribu kuwaweka kizuizini na kuwafukuza Wavenezuela kwa kuzingatia asili yao, sio kwa shughuli zozote za magenge ambazo zinaweza kuthibitishwa katika kesi za uhamiaji," aliongeza.