Godwin Asediba wa Ghana ashinda Tuzo ya BBC Komla Dumor ya 2025

Muda wa kusoma: Dakika 2

Mwanahabari wa Ghana Godwin Asediba ameshinda tuzo ya BBC News Komla Dumor ya 2025.

Mwanahabari wa habari za uchunguzi, mtayarishaji filamu na mtangazaji wa habari, ambaye ni mpokeaji wa 10 wa tuzo hiyo, anafanya kazi na TV3 na 3FM nchini Ghana. ripoti zake pia zimeonekana kwenye vyombo kadhaa vya kimataifa.

Mwandishi huyo mwenye umri wa miaka 29 mara nyingi huangazia masuala ya maslahi ya binadamu yanayolenga kufichua ukosefu wa haki na kupaza sauti za jamii zilizotengwa.

Tuzo hiyo, ambayo sasa ina muongo mmoja, ilianzishwa kwa heshima ya Dumor, mwandishi wa habari kutoka Ghana na mtangazaji wa BBC World News, ambaye aliaga dunia ghafla akiwa na umri wa miaka 41 mnamo 2014.

Alikuwa amefanya kazi bila kuchoka kuleta simulizi kuhusu masuala yenye utata zaidi ya Afrika duniani, akiwa mwenye kujiamini na mwenye ujuzi.

"Urithi wa Komla unatukumbusha kwamba simulizi za Kiafrika zinastahili kusimuliwa kwa kina, heshima na kujitolea bila woga kwa ukweli," Asediba alisema.

Kushinda tuzo hiyo haikuwa tu "hatua binafsi" kwa Mghana bali pia "wito wa kuendeleza moyo wa uandishi wa habari ambao unafahamisha, kuhamasisha na kubadilisha".

Majaji wa tuzo hiyo walisema walifurahishwa na kazi ya uchunguzi ya Asediba na imani yake isiyoyumba katika uadilifu wa wanahabari.

Makala moja ambayo alijivunia sana ilikuwa uchunguzi wake katika moja ya vyumba vikubwa zaidi vya kuhifadhia maiti vya Ghana ambavyo vilikuwa vimepuuzwa, na hivyo kusababisha hatari ya afya ya umma.

Asediba sasa anatazamiwa kusafiri hadi London ambako atatumia miezi mitatu kufanya kazi na timu za BBC News kwenye televisheni, redio na mtandaoni.

Pia atapata mafunzo na kuongozwa na wanahabari wakuu wa BBC.

"Katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, Tuzo ya Komla Dumor imesaidia kukuza baadhi ya wanahabari wenye kipaji barani Afrika.

Imekuwa fursa nzuri kuwatazama wakikua na kuleta athari chanya ya kudumu, katika BBC na kwingineko," mkurugenzi wa kanda ya Afrika wa BBC Juliet Njeri alisema.

"Maadhimisho haya ya 10 yanasimama kama ushuhuda wenye nguvu wa urithi wa kudumu wa Komla Dumor: shauku yake ya kusimulia simulizi za ujasiri, za kweli na sauti zinazotetea sauti za Kiafrika zinaendelea."

Asediba atasafiri barani Afrika kuripoti habari ambayo itatangazwa kwa hadhira ya kimataifa ya BBC.

Waliowahi kukabidhiwa tuzo hizo ni Rukia Bulle, Paa Kwesi Asare, Dingindaba Jonah Buyoya, Victoria Rubadiri, Solomon Serwanjja, Waihiga Mwaura, Amina Yuguda, Didi Akinyelure na Nancy Kacungira.

Mwaka jana, Bulle alisafiri hadi Senegal kuripoti kuhusu kuanguka kwa Baye - kikundi kidogo cha Waislamu ambao mwonekano wao mzuri unawafanya kuwa wa kipekee.