WARIDI WA BBC: Nilishauriwa ‘kuzaa’ mapema ili kupona ugonjwa wa Endometriosis

    • Author, Martha Saranga
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Ritha Mwambene, Mtanzania ambaye akiwa na umri wa miaka 18 alianza kupata dalili za maumivu yasiyo ya kawaida tangu alipopata hedhi kwa mara ya kwanza.

“Nimekuwa katika jamii ambayo unaambiwa kwamba ni kawaida mwanamke kupata maumivu anapokuwa katika hedhi’’

Kwa mara ya kwanza alipovunja ungo aliona ni hali ya kawaida hadi pale alipotimiza umri wa miaka 18 ndipo alianza kuona kwamba hilo halikuwa jambo la kawaida.

Alikuwa akiingia hedhi hadi siku 7 na huku akiwa mgonjwa sana na kupata damu nyingi.

Hali hii ilimsababishia kuwa mgonjwa haswa hali iliyomlazimu yeye pamoja na mama yake kuanza kwenda hospitali tofauti kutafuta majibu ya tatizo lake.

”Katika kipindi cha miaka 7 nilikuwa nikipatiwa majibu tofauti ambayo kila yalipotibiwa hayakuleta matokeo chanya’’

Ritha ambaye ni mtayarishaji wa filamu anasema hedhi haitakiwi kuwa kama ugonjwa kwa mwanamke, inapotokea hedhi ambayo haiwezekani kuidhibiti kiasi cha kushindwa kufanya shughuli za kila siku, hiyo si sawa.

Endometriosis ilivyoathiri elimu na maisha yake

Ritha anasimulia kwamba tatizo hilo lilimuathiri kwa sababu muda mwingi aliutumia kwenda hospitali takriban kila mwezi. Anasema: unaugulia maumivu makali sana na hata kurudishwa nyumbani mara kadhaa na kukosa masomo hasa ninapokuwa katika hedhi.

Anasema amesoma sana shule za bweni hivyo ilikuwa kila mara anarejeshwa hospitali au nyumbani kufanyiwa vipimo na matibabu hivyo kukosa masomo.

Anakumbuka aliwahi kupewa vipimo vilivyosema ana uvimbe kwenye kizazi, majibu ambayo yalimfanya aone ni mambo ya ajabu kabisa kwani hakutarajia kuwa na shida hiyo akizingatia umri aliokuwa não mdogo.

“Hilo wazo lilikuwa linapewa nguvu na jamii inayonizunguka, unakuta nimemwambia mtu changamoto yangu, basi wanajikuta tu wanahusisha ugonjwa huo na uvimbe”, anaelezea Ritha.

‘’Lakini wapo walionitazamana kwa jicho la kutonielewa kwamba kwa nini ninadeka’’ anaongeza

Aliwahi kuambiwa kuwa hana tatizo lolote bali ni ameiweka tu akilini kwamba kila akiingia hedhi lazima aumwe, “hivyo majibu kama hayo kuna wakati ukimwambia mtu anashindwa kunielewa na kuniona ninadeka”.

Anaeleza kuwa kuna wakati alikwenda hospitali akaambiwa yupo sawa hana tatizo

Alitambua vipi tatizo?

Ritha anasikitika sana kwa kuchelewa kupata vipimo sahihi kwani mara zote alizokwenda kutafuta matibabu alipatiwa majibu tofauti yaliyomkanganya.

Alikazana kutumia dawa za kupunguza maumivu ambazo wakati mwingine hazikumsaidia.

Anasema kwa wanafunzi wenzake, na watu wa karibu kama mama yake ndiyo waliomuona hali aliyokuwa nayo wakati akiwa hedhi, anasema hao waliweza kuelewa vizuri usumbufu na maumivu aliyokuwa anapitia..

Mnamo mwaka 2022 akiwa Nairobi kimasomo,anasema alikuwa anajificha kwa sababu alipata ufadhili wa masomo, hakutaka ijulikane kama anaumwa, hivyo alitumia dawa zaidi ili kuikabili hali hiyo.

“Niliumwa sana kiasi kwamba nilizidiwa nikachukuliwa katika hali ya dharura na nikalazwa hospitali na nilipata muda wa kumueleza ukweli daktari wa magonjwa ya wanawake kuhusu dalili na hali niliyokuwa ninapitia akanishauri na kunieleza baada ya kufanya vipimo vya laparoscopic surgery

Baada ya upasuaji alipatiwa majibu kwamba amekutwa na Endometriosis ambayo ilisambaa na kuathiri sehemu ya nyuma ya kizazi chake. Hivyo alishauriwa kufanyiwa upasuaji.

“Wakati ninakwenda kufanyiwa upasuaji nilikuwa na hisia mchanganyiko sielewi natamani nikutwe naumwa au siumwi”, anasema.

“Nilifanyiwa upasuaji kwa saa tano muda ambao hatukutarajia, kesho yake asubuhi daktari aliyenifanyia upasuaji alikuja kuniona na kuniambia waliikuta na wakaichoma. Anasema alifurahi kwani alijua kilichomtokea.

Miaka miwili baada ya upasuaji amepata nafuu gani?

Kabla ya upasuaji aliambiwa uwezekano wa kupona kabisa ni mdogo, lakini inawezekana kupona na kwa muda mfupi na tatizo likarejea tena.

Anafafanua: Nilipata madaktari wazuri Nairobi na hapa nyumbani Tanzania, ambao walinishauri vizuri namna ya kuielewa hali yangu na kuikubali ili niweze kuendelea na maisha.

Ugonjwa umethiri vipi maisha yake?

”Imeniathiri sana kwani ninaona ninapoteza utambulisho wangu halisi. Kuumwa na kupata mitazamo mbalimbali ya watu ilikuwa inaniumiza na kunifanya kuwa kimya sana. Niliwaza sana na kujali maneno mabaya ambayo jamii inayonizunguka ilikuwa inasema kutokana na kutonielewa”.

Ritha anasema anakumbuka namna ambavyo amekuwa akipokea maneno kama ukizaa utapona.

Kuna wakati watu wa kawaida tu walikuwa wakimuambia azae ili apone, jambo ambalo lilimpa mawazo na maswali kwamba ni kwa vipi uponyaji wake unategemea kufanya uamuzi wa kuzaa, ambao hakuuona kuwa mwepesi.

‘’Nililia sana nikawaza yaani hiki si kitu ambacho nimekifikiria na kwa wakati huo mimi ni mwanafunzi, kwa hiyo muda wote huo nitaendelea kuteseka? ilinihuzunisha sana” anaeleza Ritha.

Madaktari walimishauri kama atapenda kupata watoto basi azae mapema. Lakini hakuwa tayari, anasema hajakubalina na kwamba Endometriosis na changamoto zake izuie kufanya mambo mengine yanayoweza kuwa na mchango chanya katika jamii.

Anasema aliamua kubadili tu mtazamo wake kwamba bado ana mambo mengi anayoyapenda anayoamini anaweza kufanya na kupata amani na furaha na kuisaidia jamii.

Aliamua kuandaa makala yenye uhalisia inayohusu changamoto ambazo wanawake wenye tatizo la Endometriosis wanakabiliana nazo hasa kabla ya kufahamu kuhusu tatizo linalowakabili.

Anakumbuka safari ya miaka saba ya kusumbuka na ugonjwa ambao hakuna aliyekuwa akiuelewa. Ameona ni vema watu wengine pia wajue.

Makala yake iko katika hatua za mwanzo za uandaaji.

Mbinu gani ulitumia kuyakabili maumivu?

Mara nyingi amekuwa akitumia dawa kali za kutuliza maumivu.Anakumbuka aliwahi kutumia dawa za kawaida ambazo zilikuwa zikishindwa kumsaidia.

Baada ya kujua hiyo hali ameikubali na hivyo inampunguzia sehemu ya msongo wa mawazo na wasiwasi.

‘Kwamba sasa nikianza kuumwa siogopi kusema kwamba watu watafikiria labda nimetoa mimba’.

Maumivu halisi ndani ya makala

Ritha anasema anarekodi kwa nyakati tofauti tofauti kwakuwa ni suala la kufikisha hisia zaidi ya kila alichopitia.

Si rahisi kurekodi wakati wa maumivu.

Kupitia makala hiyo kila mtu ataelewa na jamii nzima itajiona ina jukumu gani katika kumsaidia mwanamke huyu anayekabiliwa na Endometriosis.

‘’Nimeilenga jamii kwa upana wake,wanawake wanaume,wazazi wasimamizi wa ajira,wenzi ama wapenzi’’

Kuna uhitaji mkubwa kwa jamii yetu kuuelewa kuhusu matatizo kama haya ambayo hayajulikani kirahisi kama ilivyotokea kwangu kwenye ugonjwa huu wa Endometriosis.

Pia serikali inabidi kutia mkono katika kuisaidia jamii kuelewa vizuri kuhusu haya maradhi ambayo hayafahamiki kwa wepesi.

Jamii ikipewa elimu itajua namna ya kuwasaidia na kuwahudumia wagonjwa wa aina zote ikiwemo wa Endometriosis.