Julius Malema: Mwanasiasa anayeiongoza EFF katika uchaguzi wa 2024 wa Afrika Kusini

FDC

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Julius Malema ana sifa ya kukiuka mipaka. Chama alichokijenga karibu miaka 11 iliyopita, kimekua na sasa ni chama cha tatu kwa ukubwa nchini Afrika Kusini.

Uhai wa chama chake, ulioambatana na itikadi kali, umewatia moyo Waafrika Kusini wengi waliokata tamaa.

Lakini kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 43 wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF), ana wakosoaji wengi wanaomtuhumu kwa chuki na kusema amehukumiwa mara mbili kwa kutumia matamshi ya chuki.

Baada ya Kufukuzwa ANC

EFD

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Wabunge wa EFF mara nyingi wametatiza shughuli katika bunge la Afrika Kusini

Alipofukuzwa kutoka chama tawala cha African National Congress (ANC) mwaka 2012, Malema, au "Juju" kama anavyoitwa wakati mwingine, amekiweka EFF kama mrithi wa ANC.

Mtazamo wake juu ya ukosefu wa usawa nchini Afrika Kusini, na kushindwa kwa ANC kugawa ardhi vya kutosha kutoka kwa Wazungu walio wachache na kuwapa weusi walio wengi, kulimgharimu na kufukuzwa chake cha zamani, ambacho kiliongoza vita dhidi ya ubaguzi wa rangi.

Katika uchaguzi mkuu wa 2019, EFF ilipata karibu 11% ya kura na viti 44 bungeni. Watafiti wa kura za maoni Ipsos wanasema chama hicho kinaweza kupata ushindi kama huo mwaka huu .

Wakati huo huo, kura nyingi za maoni zinatabiri ANC inaweza kupata chini ya 50% ya kura kwa mara ya kwanza katika miaka 30 na kupoteza wingi wake bungeni.

Licha ya kuwa kwa sasa ni chama cha wachache, Malema na wenzake bila shaka ndio wanasiasa wanaoonekana zaidi bungeni. Wanavaa suti nyekundu - zinazomaanisha kuwaunga mkono wafanyakazi wa Afrika Kusini - na mtindo wao wa siasa umesababisha mapigano ya ngumi na kutoka katika Bunge la Kitaifa.

Malema mwenye Utata

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Malema mwenyewe anajulikana kwa kuzua utata - katika maisha yake yote ya kisiasa amewaudhi watu mbalimbali, kuanzia vikundi vya kutetea haki za wanawake, wakulima wa kizungu, hadi wakuu wake wa kisiasa.

Amepatikana na hatia mara mbili ya kutumia matamshi ya chuki - mwaka 2010 na 2011 - kwanza kwa maoni aliyotoa kuhusu mwanamke ambaye alimshutumu Rais wa zamani Jacob Zuma kwa ubakaji na kisha kwa kuimba wimbo Shoot the Boer (piga risasi mkulima).

Mkuu huyo wa EFF alizua mzozo mwaka jana, alipouambia umati wa watu kwenye maandamano dhidi ya Israel kuhusu vita huko Gaza: "EFF, itakapochukua mamlaka mwaka ujao, itaipa silaha Hamas na kuhakikisha Hamas ina vifaa muhimu kupigania watu wao."

Kundi la Wapalestina la Hamas, linachukuliwa kuwa kundi la kigaidi na Israel, Marekani, Umoja wa Ulaya, Uingereza na taasisi mbalimbali.

Na mwaka 2016, alipozungumza na wafuasi wake kuhusu kasi ndogo ya ugawaji wa ardhi, Malema alionya:

"Ardhi itachukuliwa kwa njia yoyote ile. Hatutoi wito wa kuchinjwa kwa watu weupe. Kwa sasa. Tunachotaka ni kuchukua ardhi kwa amani na hatutoomba radhi kwa hilo."

Wafuasi wa Malema wanafurahia maneno haya, na anasalia kuwa mzungumzaji ambaye mtazamo wake mkali juu ya haki za watu maskini weusi wa Afrika Kusini umemfanya apendwe.

Ni maarufu hasa miongoni mwa vijana – katika nchi ambayo wastani wa umri ni miaka 28. Malema pia amezua gumzo wakati wa kuzuru nchi nyingine za Afrika, kama vile Ghana, Liberia na Kenya.

Prof PLO Lumumba, mwenyekiti wa Taasisi ya Pan-African ambayo ilimkaribisha Malema nchini Kenya, aliiambia BBC mwaka jana:

"Malema anawakilisha kizazi kipya cha Waafrika ambao sasa wanaanza kueleza masuala ya Afrika kwa njia ambayo inavutia umati mkubwa."

Hata hivyo, nchini mwake ‘Malema hana uwezo wa kushinda kura nyingi nje ya wafuasi wake," anasema mchambuzi wa siasa Richard Callland.

"Nadhani chapa ya Malema, ambayo ni ya uvunjifu wa amani, siasa za mapigano, hata siasa za vurugu wakati mwingine - sidhani kama zinaungwa mkono na umma."

Historia ya Malema

Malema alizaliwa mwaka 1981 na kulelewa na mfanyakazi wa ndani mama Flora. Alikulia Seshego, kitongoji katika jimbo la kaskazini la Limpopo.

Matokeo yake ya shule ya mwaka wa mwisho yaliyovuja yalikuwa mabaya. Amepata digrii mbili za chuo kikuu huku akiiongoza EFF.

Malema anasema alijiunga na vuguvugu la vijana la ANC akiwa na umri wa miaka tisa, ambapo alifunzwa upinzani wa kutumia silaha, na ilimchukua miaka mitano tu kuwa mkuu wa kikanda wa Umoja wa Vijana wa ANC.

Kuchaguliwa kwake kama kiongozi wa Umoja wa Vijana wa ANC mwaka 2008 - kulimfanya kuwa mhusika mkuu katika siasa za kitaifa.

Hatua zake za mwanzo kama kiongozi zilikuwa kumpigia kampeni Zuma kuchukua wadhifa - kama kiongozi wa ANC na baadaye kama rais – alikuwa akiwaambia wafuasi "uwa kwa ajili ya Zuma."

Lakini uhusiano wa Malema na BZuma ulidorora mara tu baada ya Rais huyo kuwa rais mwaka 2009. Malema alimshutumu mshirika wake wa zamani kwa kuwapuuza wapiga kura maskini ambao walimweka madarakani. Baada ya kufukuzwa ANC, aliunda EFF 2013.

Katika utangulizi wa manifesto ya EFF ya 2024, Malema alisema ANC "imezalisha tena ukosefu wa usawa wa kiuchumi na ubaguzi wa rangi."

Ilani hiyo iliahidi kuunda nafasi za kazi kwa mamilioni ya watu ambao hawana ajira, kumaliza kukatika kwa umeme na kutaifisha sehemu muhimu za uchumi, kama vile migodi na benki.

Shutuma dhidi yake

FDVC

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Takriban watu 56,000 walijitokeza kuzindua kampeni za Malema

Hata hivyo, Malema hapo awali ameshutumiwa kwa kusaliti itikadi ya mrengo wa kushoto.

2013, mamlaka ya mapato ya Afrika Kusini ilisema kiongozi huyo wa chama anadaiwa zaidi ya dola za kimarekani milioni 1 ya kodi ambayo haijalipwa.

Ili kulipa malimbikizo ya kodi, Malema alilazimika kuuza jumba ambalo halijakamilika katika kitongoji cha Sandton cha Johannesburg, ambalo lilijumuisha chumba cha sinema na baa.

Pia alikabiliwa na mashtaka ya ulaghai na ufisadi kuhusiana na kandarasi ya serikali. Baada ya miaka mitatu, mashtaka yalitupiliwa mbali na mahakama mwaka 2015 kwa sababu ya ucheleweshaji wa muda wa kumfikisha mahakamani, hakimu aliamua.

Daima alikanusha mashtaka hayo na kusema yamechochewa kisiasa.

Mwaka 2018, Malema alikuwa miongoni mwa kundi linalodaiwa kupora takribani rand bilioni 2 (dola milioni 108) kutoka kwa benki iitwayo VBS. Malema alipuuzilia mbali madai hayo na uchunguzi wa bunge kuhusu suala hilo ulifungwa bila hitimisho kwani wachunguzi walisema hawakuwa na "taarifa za kutosha."

Mbio za uchaguzi mkuu

"Malema anaingia kwenye uchaguzi akiwa imara, lakini sio imara kama alivyokuwa," anasema Paddy Harper, mwandishi wa habari wa gazeti la Mail & Guardian la Afrika Kusini.

Anaashiria mvutano ulioripo kati ya Malema na naibu wake, Floyd Shivambu, pamoja na kufanya vibaya EFF katika uchaguzi mdogo wa hivi karibuni.

EFF pia inakabiliwa na ushindani kutoka uMkhonto we Sizwe (MK), chama kilichoanzishwa mwaka jana tu na kinachoongozwa na Rais wa zamani Jacob Zuma.

Kulingana na Ipsos, MK imekusanya wafuasi wengine wa EFF, haswa katika jimbo analotoka Zuma la KwaZulu-Nata.

Tunachojua ni kwamba kiongozi huyo mwenye itikadi kali ameanzisha harakati za kuikomboa nchi kutoka mikononi mwa ANC na nguvu yake imemfanya kuwa na kundi la wafuasi waliojitolea.

Mwezi Februari, maelfu ya wafuasi waliokuwa wamevalia mavazi mekundu walilipuka kwa shangwe wakati Malema alipowasili kwenye uzinduzi wa manifesto ya EFF.

Akitoa nakala ya waraka, aliutangazia umati huo: "Hii ndiyo silaha itakayotumika dhidi ya adui wa mapinduzi yetu!"

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah