Treni ilivyotekwa na abiria wake 400, wenyewe wasilimulia

    • Author, BBC Urdu & Kelly Ng
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Kwa kawaida tumezoea kusikia ndege zikitekwa, au mabasi yakitekwa na majambazi, magaidi na wahalifu wengine, lakini matukio ya treni kutekwa ni nadra sana kuyasikia.

Hii inatokana na ukweli kuwa ni jambo gumu mtekaji kumuamuru dereva wa treni aipeleke treni kwenye eneo jingine au nchi nyingine anayotaka yeye, ni tofauti na ndege ambayo rubani anaweza kulazimishwa kuipeleka katika nchi nyingine.

Lakini huko Pakistan treni ya Jaffar Express imetekwa na wanamgambo waliojihami kwa silaha wakati inapita katika handaki karibu na mji wa Sibi siku ya Jumanne, ikitokea mji wa Quetta katika jimbo la kusini-magharibi la Balochistan na kuelekea mji wa Peshawar katika jimbo la Kaskani -magharibi la Pakhtunkhwa.

Kulikuwa na zaidi ya abiria 400 waliokuwa wakisafiri, pale wanamgambo wajiitao Jeshi la Ukombozi la Balochistan (BLA), liliposhambulia treni na kuwachukua mateka abiri. Dereva wa treni ni miongoni mwa watu walioripotiwa kujeruhiwa.

Duru za kijeshi zinasema abiria 155 wameachiliwa na wanamgambo 27 wameuawa. Hakuna uthibitisho huru juu ya takwimu hizo, na shughuli za uokoaji zinaendelea.

Serikali inasema imepeleka mamia ya wanajeshi kuwaokoa abiria waliosalia, pia imetuma helikopta na vikosi maalumu vya kijeshi.

BLA imeonya kuwa kutakuwa na madhara makubwa, ikiwa kutafanyika jaribio kuwaokoa mateka. Zaidi ya abiria kumi na wawili walioachiliwa walipelekwa hospitalini kwa matibabu.

Ripoti zilizonukuu maafisa wa usalama zinasema, baadhi ya wanamgambo hao huenda waliondoka kwenye treni hiyo, na kuchukua idadi isiyojulikana ya abiria kwenda nao katika eneo la milima jirani.

Takribani watu 100 kati ya waliokuwa kwenye treni hiyo walikuwa ni maafisa wa vikosi vya usalama, maafisa wamesema.

Wanamgambo hao wametishia kuwaua mateka ikiwa serikali haitawaachilia wafungwa wa kisiasa wa Baloch ndani ya saa 48, kulingana na ripoti za ndani.

Pia unaweza kusoma

Abiria wasimulia

Muhammad Ashraf, aliyekuwa akisafiri kutoka Quetta kwenda Lahore kuitembelea familia yake, alikuwa miongoni mwa kundi la abiria waliofanikiwa kushuka kwenye treni Jumanne jioni. Anasema, "abiria walikuwa na hofu."

Kundi hilo la watu lilitembea kwa karibu saa nne hadi kituo kingine cha treni. Wanaume kadhaa walibeba abiria waliokuwa dhaifu mabegani mwao.

"Tulifika kituoni kwa shida sana, kwa sababu tulikuwa tumechoka na tulikuwa na watoto na wanawake," anasema.

Ishaq Noor, ni abiria mwingine aliyekuwa akisafiri na mke wake na watoto wawili, anasema mlipuko wa kwanza kwenye treni ulikuwa "mkubwa sana" kiasi cha kumfanya mtoto wake mmoja kuanguka kutoka kwenye kiti.

Yeye na mkewe kila mmoja alijaribu kumkinga mtoto mmoja katikati ya milio ya risasi. "Ikitokea risasi itakuja upande wetu, itatupiga sisi na sio watoto," anasema.

Mushtaq Muhammad, alikuwa kwenye behewa la tatu la treni hiyo. Anasema, "washambuliaji walikuwa wakizungumza wao kwa wao kwa lugha ya ki-Balochi, na kiongozi wao aliwaambia mara kwa mara wawachunge maafisa wa usalama ili kuhakikisha hawatoroki."

Washambuliaji walianza kuwaachilia baadhi ya wakazi wa Balochistan, pamoja na wanawake, watoto na abiria wazee, Jumanne jioni, anasema Ishaq.

Naye walimwachilia alipowaambia kuwa ni mkazi wa jiji la Turbat huko Balochistan, na wakaona ana watoto na wanawake pamoja naye.

Bado haijafahamika ni abiria wangapi wanashikiliwa. Vikosi vya usalama vinasema vimeanzisha operesheni kubwa ya kuokoa abiria waliosalia, na kupeleka mamia ya wanajeshi.

Siku ya Jumatano, BBC iliona makumi ya majeneza ya mbao yakipakiwa katika kituo cha reli cha Quetta. Afisa wa reli alisema ni matupu na yanasafirishwa kukusanya maiti yoyote atakae kuweko.

Waasi wa BLA

Wanamgambo wa BLA wamefanya uasi wa miongo mingi ili kupata uhuru na wamefanya mashambulizi mengi mabaya, mara nyingi yakilenga vituo vya polisi, njia za reli na barabara kuu.

Operesheni za kukabiliana na waasi hao katika eneo maskini la Balochistan zinazofanywa na jeshi la Pakistan na vikosi vya usalama zimesababisha maelfu ya watu kutoweka tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Vikosi vya usalama na Jeshi la Pakistan vinashutumiwa kwa uhalifu ikiwa ni pamoja na mateso na mauaji ya kiholela, tuhuma ambazo wanazikanusha.

Serikali ya Pakistani - pamoja na nchi kadhaa za Magharibi, ikiwa ni pamoja na Uingereza na Marekani - wameliorodhesha kundi hilo kuwa shirika la kigaidi.

Afisa wa ngazi ya juu wa polisi amesema, "treni bado imekwama nje kidogo tu ya handaki lililozungukwa na milima," kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.

Maafisa wanasema bado hawajawasiliana na mtu yeyote kwenye treni hiyo. Eneo hilo halina mtandao wa simu, maafisa wameiambia BBC.

Balochistan ni jimbo kubwa zaidi la Pakistani na lenye utajiri mkubwa wa maliasili, lakini ni moja ya majimbo masikini nchini Pakistan.

Tume ya Haki za Binadamu ya Pakistan inasema "ina wasiwasi mkubwa" juu ya utekaji nyara huo.

"Tunawaomba wahusika wote kusaka maelewano ya haraka juu ya masuala ya watu wa Balochistan na kutafuta suluhu la amani na kisiasa," imesema katika taarifa yake katika X.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres "amelaani vikali" kutekwa kwa treni na pia ametoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa abiria waliosalia.