Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mtakatifu Mary wa Misri: Aliishi uchi jangwani kwa miaka 47
- Author, Donna Ferguson
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Akiwa msichana, alikuwa mzinzi na alipenda ngono. Lakini baada ya kuukataa ulimwengu na kukaa uchi kwa miaka 47 jangwani, mwanamke huyo mwenye ngozi nyeusi akawa mwalimu mwenye hekima na mwadilifu wa maandiko ya Kikristo.
Hiyo ndiyo hadithi iliyowafikia wasomaji katika karne ya 11. Hadithi ya ajabu ya Mtakatifu Mary wa Misri ilipotafsiriwa kwa mara ya kwanza kutoka Kilatini hadi Kiingereza cha Kale zaidi ya milenia moja iliyopita.
Alexandra Zhirnova, mtafiti katika Chuo Kikuu cha Cambridge, Uingereza, anaeleza kwa nini hadithi ya mtakatifu huyu ilivutia sana.
Mary wa Misri au Mtakatifu Mary wa Misri, inasemekana aliishi Misri karne ya 4, alikuwa tayari amepata utakatifu katika baadhi ya sehemu za Ulaya baada ya kitabu cha maisha yake kutafsiriwa kwenda Kiingereza cha Kale.
Historia yake tukufu (hagiolojia) iliandikwa na Sophronius, Kiongozi wa kidini wa Jerusalem (634 - 638), ambaye alikusanya hadithi hiyo kupitia mapokeo ya mdomo kwa miongo kadhaa. Maisha yake yanasimuliwa na mtawa, Mtakatifu Zosimos wa Palestina, ambaye alidai alikutana naye jangwani, akizunguka peke yake akiwa uchi.
"Alikataa ulimwengu hadi kuacha kuvaa nguo, kwa sababu hakuzihitaji," anasema Zhirnova.
Alikuwa kahaba tangu ujana wake, alimwambia Zosimos, si kwa ajili ya pesa, bali kwa "tamaa isiyoweza kutoshelezwa na hamu isiyoweza kudhibitiwa."
Mtakatifu Mary wa Misri alikuwa kahaba kwa miaka 17. Alizaliwa mwaka 344 BK, alihamia mji wa Alexandria alipokuwa na umri wa miaka 12 na kufanya kazi kama kahaba. Kwa nia ya kuendelea na biashara yake, alijiunga na kundi kubwa lililokuwa likifanya safari ya kwenda Jerusalem kwa ajili ya Sikukuu ya Kuinuliwa kwa Msalaba Mtakatifu.
Katika sikukuu yenyewe, alijiunga na umati ulipokuwa ukielekea kanisani ili kuabudu, tena kwa nia ya kuwavuta wengine kutenda dhambi. Alipofika kwenye mlango wa kanisa, hakuweza kuingia. Mary wa Misri alikwenda kwenye kona ya uwanja wa kanisa na kuanza kulia machozi ya majuto.
Kisha akaona sanamu ya Bikira Mbarikiwa. Aliomba kwa Mama Mtakatifu ruhusa ya kuingia kanisani. Mary wa Misri aliingia kanisani. Kisha aliondoka jioni, kwenda Jordan kupokea ushirika katika kanisa lililowekwa wakfu kwa Mtakatifu Yohana Mbatizaji.
Siku iliyofuata, alivuka mto na kwenda jangwani, ambako aliishi peke yake kwa miaka 47. Kisha, alipokuwa akifunga Kwaresima, kasisi mmoja aitwaye Zosimus alimkuta mwanamke huyo.
Rangi yake
Ingawa haijulikani kwa hakika kama alikuwa mweusi wa kuzaliwa au la, Zhirnova anasema. Tafsiri ya Kiingereza cha Kale ya hadithi hiyo inasema alikuwa "mweusi kwa sababu ya joto la jua."
Mtafiti anaeleza wasomaji wa zama hizo hawakuelewa au kutambua tofauti za rangi kama tunavyofanya leo.
"Wakati huo, waliamini watu wenye ngozi nyeusi walikuwa na ngozi nyeusi kwa sababu waliishi katika maeneo yenye jua sana."
Ikiwa Mtakatifu Mary alikuwa mweusi au ngozi yake ilibadilika kuwa nyeusi, hilo halikuwa jambo kubwa sana kwa wasomaji wa zama hizo.
Maisha ya Mary
Irina Dumitrescu, profesa wa Kiingereza cha Kale, katika chuo kikuu cha Bonn, anasema, sababu iliyofanya hadithi hiyo ya ajabu kuwa maarufu "ni binadamu kutaka kujua kwamba Mungu anapenda watu wasio wakamilifu pia."
"Hadithi ya Mary wa Misri ina somo muhimu sana ambalo halipatikani kwa wanawake mabikira watakatifu."
Tofauti na hadithi nyingine za watakatifu waliokwenda jangwani ili kujiweka wakfu kwa Mungu, Mary wa Misri hakukaa mahali pamoja. Alilizunguka jangwa kwa uhuru. Alichanganyika na asili. Alikuwa uchi.
"Kwa Wakristo wacha Mungu ambao waliishi maisha ya stara, wazo la mwanamke anayezurura uchi kwa uhuru katika jangwa na kuwasiliana na Mungu ni la kusisimua na kwa kiasi fulani la ajabu," anasema Dumitrescu.
Mtakatifu aliyeasi
Wakati huo huo ambapo hadithi hiyo ilitafsiriwa na kuanza kuenea, pambano la kuwania madaraka lilizuka ndani ya Kanisa na kutishia kuzuia uhuru wa wanawake Wakristo walioishi katika nyumba za watawa, ambao wamejiweka wakfu kwa Mungu.
Wanamageuzi wa Kibenediktini kama vile Mwingereza Ælric wa Eynsham walitetea kutenganishwa wanaume na wanawake ambao walifanya kazi bega kwa bega katika nyumba za watawa, mara nyingi chini ya uongozi wa mwanamke.
"Nchini Uingereza wakati huo kulikuwa na mila ya muda mrefu ya jumuiya za mchanganyiko. Lakini wanamageuzi walisema hili lisiruhusiwe, kwani liliunda vishawishi kwa wanaume na wanawake," anasema Zhironova.
Wanawake wazee, ambao walishikilia nyadhifa za mamlaka katika nyumba za watawa, wangeathirika haswa.
"Hili lingezuia shughuli nyingi ambazo wanawake wa kidini wangeweza kushiriki, kama vile kufundisha, kuandika, na kuhubiri kwa waumini."
Hadithi ya Mtakatifu Mary wa Misri, mtafiti anasema, labda ilitafsiriwa au kusambazwa na watu ambao hawakuunga mkono mageuzi kama hayo.
"Tunaona mwanamke ambaye anapinga dhana za kawaida za kanisa. Wanawake hawaruhusiwi kufundisha, lakini Mary anafundisha."
Mtakatifu Mary pia alibadilisha mawazo kuhusu uzuri na tabia ya ngono. Weupe ulihusishwa na urembo katika zama za kale Uingereza. Na wasomaji wengi wa watakatifu wa kike watakuwa wamesikia kuwa ngozi nyeupe, ujana na uzuri; sifa hizi zilienda sambamba," anasema Zhirnova.
"Moja ya sifa kuu za Mary ni kupinga hayo. Na ngozi yake inakataa matarajio yote ya wanawake watakatifu."
Zhirnova anatumai utafiti wake utakuwa na athari sawa na Maisha ya Mary wa Misri kama yalivyokuwa katika Uingereza ya karne ya 11.
Vile vile, Zhirnova anatumai utafiti wake utatoa changamoto kwa baadhi ya fikra potofu zinazoendelezwa.
"Yeye ni mtakatifu aliyeasi."
Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi