China inataka nini kutoka Afrika?

Muda wa kusoma: Dakika 6

Na Jeremy Howell

BBC

Katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, China imeongeza kwa kiasi kikubwa biashara na Afrika na kumwaga mabilioni ya dola katika ujenzi wa barabara, reli na bandari kote barani humo.

Hii imefanywa kupitia Jukwaa la Ushirikiano wa China na Afrika (FOCAC), mkutano wa miaka mitatu ambao unaelezea jinsi China na nchi za Afrika zinavyoweza kushirikiana kwa njia iliyo bora zaidi.

Mkutano wa mwaka huu uliofunguliwa mjini Beijing Jumatano, Septemba 4, na unamalizika Ijumaa, wakati Rais wa China Xi Jinping atakapotoa hotuba.

Hivi karibuni, China imebadilisha mkakati wake wa kuipa Afrika bidhaa zake za teknolojia za hali ya juu, pamoja na bidhaa rafiki kwa mazingira, au kile kinachojulikana kama "uchumi wa kijani."

China inafanya biashara ngapi na Afrika?

Katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, China imekuwa mshirika mkubwa wa kibiashara barani Afrika, mwekezaji mkubwa katika nchi za Afrika, na mkopeshaji mkubwa.

Biashara na nchi za Afrika mwaka 2022 (kulingana na rekodi zilizopo) ilizidi thamani ya dola bilioni 250. Hii ilihusisha China kuagiza malighafi nyingi kama vile mafuta na madini kutoka bara hilo, na kusafirisha bidhaa za viwandani kwa nchi za Afrika.

Mwaka huo huo, iliwekeza dola bilioni 5 katika uchumi wa Afrika, hasa kujenga viunganishi vipya vya usafiri, vifaa vya nishati, na kuendeleza migodi.

Mnamo mwaka 2022, kampuni za China zilipata faida kutokana na miradi hii yenye thamani ya karibu dola bilioni 40.

Kwa sasa kuna takriban makampuni 3,000 ya China barani Afrika, kwa mujibu wa Jukwaa la Uchumi Duniani (World Economic Forum).

Nchi za Afrika pia zinaidai China dola bilioni 134 kama mikopo kwa ajili ya maendeleo, na inashikilia asilimia 20, au yote, ya deni linalodaiwa na nchi za Afrika kwa dunia nzima.

Hata hivyo, kumekuwa na kupungua kwa mikopo ya China kwa nchi za Afrika na uwekezaji wake barani Afrika.

"China imekuwa na furaha kutoa mikopo kwa ajili ya miradi barani Afrika, kama vile reli, ambayo nchi za Magharibi na Benki ya Dunia haziwezi kuipatia fedha kwa sababu haina maana ya kibiashara," anasema Profesa Steve Tsang wa SOAS, kutoka Chuo Kikuu cha London.

"Sasa, nchi nyingi za Afrika zinaona kuwa hazipati mapato ya kutosha kutoka kwa miradi hii ili kulipa mikopo," anaongeza.

Leo, wakopeshaji wa Kichina kwa Afrika wanazidi kutambua kuhusu miradi. Wanatafuta miradi ambayo inaweza kuzalisha faida zaidi," anasema Dkt Alex Vines wa taasisi ya masuala ya kigeni ya Uingereza mjini London, Chatham House.

China pia imebadilisha mtazamo wake mbali na kuzipatia nchi za Afrika miradi mikubwa ya miundombinu - vitu kama barabara, reli na bandari - kuelekea kuwapa teknolojia ya hali ya juu kama vile mitandao ya simu ya 4G na 5G, satelaiti za anga, paneli za nishati ya jua na magari ya umeme.

"China inashutumiwa kwa kufurika soko la Afrika kwa magari ya umeme," anaongeza Dkt. Vines. "Hii ni njia moja ambayo China inaweza kuuza nje teknolojia yake mpya ya kijani."

Je, biashara na China imesaidia au kuiumiza Afrika?

China ilianzisha uhusiano mkubwa wa kibiashara na nchi za Afrika mwaka 1999, wakati Chama cha Kikomunisti cha China kilipozindua mkakati wake wa "kwenda nje".

Kongamano la Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) lilifanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2003 na sasa ni jukwaa la ushirikiano kati ya China na nchi 53 za Afrika.

Awali, lengo la China lilikuwa ni kuagiza malighafi nyingi iwezekanavyo kutoka Afrika, ili iweze kuzalisha bidhaa kwa ajili ya kuuza nje duniani kote, kwa mujibu wa Dk. Vines.

"China imetoa kiasi kikubwa cha fedha kwa Angola kujenga miundombinu ya msingi, badala ya usambazaji wa mafuta," anasema.

"Miradi hii pia ilitoa fursa za ajira kwa watu wa China. Wakati mmoja, idadi ya wafanyakazi wa Kichina nchini Angola ilifikia zaidi ya 170,000," aliongeza.

China imeelezea uwekezaji wake barani Afrika kama "faida kwa kila upande".

Hata hivyo, miradi ya ujenzi ya China barani Afrika imeleta manufaa kidogo kwa wenyeji, anasema Profesa Tsang, na hii imezua chuki. "Makampuni ya Kichina kwa kiasi kikubwa huleta wafanyakazi wao wenyewe na hayatengenezi ajira nyingi za ndani. Pia kuna hisia barani Afrika kwamba China inawatumia wafanyakazi wa ndani katika ajira zenye mazingira magumu ya kazi," anasema.

Ukopeshaji wa China kwa nchi za Afrika uliongezeka kwa kasi katika miaka baada ya 2013, china kuzindua mpango wake wa Belt and Road ili kuboresha mitandao ya biashara kote Afrika na Asia, na kufikia zaidi ya dola bilioni 28 katika 2016.

China imekuwa ikishutumiwa kwa kutoa mikopo kwa Afrika, kwa kushawishi serikali kukopa kiasi kikubwa cha fedha na kisha kuzidai pesa wakati wanapoanza kuwa na matatizo ya kulipa.

Baadhi ya nchi za Afrika zinadaiwa madeni na China: Angola inaidaiwa na China dola bilioni 18, Zambia zaidi ya dola bilioni 10, na Kenya dola bilioni 6, kwa mujibu wa takwimu za Chatham House. Nchi hizi zote zimeona kuwa ni vigumu sana kulipa kiasi hiki.

Mara nyingi, China ingekopesha fedha kwa nchi za Afrika na kuzifunga kwa ulipaji wa faida kutokana na mauzo ya malighafi. Mikataba hii iliisaidia China kupata udhibiti wa migodi mingi ya madini katika nchi kama Kongo.

Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Akinwumi Adesina ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba serikali zinapaswa kuepuka mikopo kama hiyo.

" Kwanza kabisa ni mibaya, kwa sababu huwezi kuweka bei ya mali kwa usahihi," aliongeza.

"Kama una madini au mafuta chini ya ardhi, unapataje bei nzuri kwa mkataba wa muda mrefu? Hii ni changamoto kubwa," aliongeza.

Hata hivyo, Dkt Vines anasema, "Mtego wa madeni ya China haupo kabisa."

"China wakati mwingine hufanya kwa njia ya unyonyaji wakati wa inapofanya biashara na nchi dhaifu, lakini serikali zenye nguvu zinaweza kukabiliana na China bila kukusanya madeni makubwa," anaongeza.

Je, mipango ya China kwa Afrika katika siku za usoni ni ipi?

Rais Xi Jinping wa China amefanya ziara tano katika nchi za Afrika tangu mwaka 2013.

Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika, ambalo linaanza Beijing siku ya Jumatano, ni jukwaa pana na lililoanzishwa la ushirikiano kati ya nchi za Afrika na nguvu yoyote ya ulimwengu, anasema Dk Shirley Zhi Yu wa Shule ya Uchumi ya London.

Kila baada ya miaka mitatu, Baraza linaweka malengo mapya na vipaumbele.

"Ni mkakati mzuri wa kuishirikisha China kama mshirika wa nje wa Afrika," anaongeza.

"Kufikia mwisho wa karne, asilimia 40 ya watu duniani wataishi Afrika," anaeleza Dkt. Shirley. "Si vigumu kufikiria kwamba Afrika inashikilia mustakabali wa uchumi wa dunia."

Hata hivyo, maslahi ya China barani Afrika sio tu ya kibiashara bali pia ya kisiasa, anasema Dkt Vines.

"Kuna zaidi ya nchi 50 za Afrika katika Umoja wa Mataifa. China imeshawishi karibu kila mmoja wao kutoitambua Taiwan kama taifa," aliongeza.

"Sasa tunaona picha ya wazi ya kile China inataka kutoka Afrika," anasema Profesa Tsang.

"Inataka kuwa bingwa wa Kusini mwa Dunia, na kutumia nafasi hiyo kujenga ushawishi katika Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa," anaongeza. China inataka nchi za Afrika ziwe "zinaunga mkono" suala hilo. Mkutano wa ushirikiano kati ya China na Afrika sio mkutano wa usawa, anasema.

"Kuna tofauti kubwa ya nguvu," Tsang anasema. "Ikiwa unakubaliana na China, unakaribishwa. Kwa hivyo hakuna mtu atakayesema hawakubaliani na kile unachopanga."

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi