Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jinsi kupungua kwa silaha kutaathiri vita Iran
Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa taifa lake lina "usambazaji wa kutosha" wa silaha muhimu.
Wizara ya ulinzi ya Iran nayo inasema kuwa wana "uwezo wa kupigana na adui" kwa muda mredu kuliko vile inadhaniwa na Marekani.
Hifadhi ya silaha pekee haitaamua jinsi vita hivyo vitamalizika.
Ukraine ina idadi ndogo ya wanajeshi na silaha chache ukilinganisha na Urusi, ila hilo si la muhimu sana katika vita hivyo.
Kasi ya operesheni za kijeshi imekuwa ya juu tangu mwanzo wa vita hivyo. Pande zote mbili tayari zinatumia silaha kwa kasi kubwa zaidi kuliko zinavyoweza kuzalishwa.
Taasisi ya mafunzo ya usalama wa taifa mjini Tel Aviv(INSS) inakadiria kwamba Marekani na Israel tayari wametekeleza zaidi ya mashambulizi 2000 kwa kutumia silaha tofauti.
INSS inasema Iran imetekeleza mashambulizi 571 kwa kutumia makombora na 1,391 kwa kutumia ndege zisizo na rubani, nyingi ambazo zimedunguliwa. Kwa pande zote, hawataweza kumudu kasi ya vita hivyo iwapo vitadumu kwa muda mrefu.
Iran
Maafisa kutoka mataifa ya magharibi wanasema kuwa Iran imepunguza idadi ya makombora wanayorusha, kutoka zaidi ya mia moja kwa siku ya kwanza ya vita hadi makombora machache tu kwa sasa.
Kabla ya vita, ilikadiriwa kuwa Iran ina makombora 2000.
Hakuna jeshi ambalo husema idadi kamili ya silaha walizo nazo, idadi hiyo ikibakia siri.
Mmoja wa makamanda wakuu wa Marekani, Gen Dan Caine,alisema siku ya Jumatano kuwa Iran imepunguza makombora wanayorusha kwa 86% kuanzia siku ya kwanza ya vita Jumamosi iliyopita.
Afisi kuu ya jeshi la Marekani (Centcom) inasema kumekuwa na kupungua kwa mashambulizi kutoka Iran kwa 23%.
Iran inaaminiwa kuwa ilikuwa imezalisha maelfu ya ndege zisizo na rubani kabla ya vita hivi na kuzipeleka Urusi, ambayo imekuwa ikitumia ndege hizo zisizo na rubani aina ya Shahed,kuishambulia Ukraine. Marekani pia imeiga muundo wa ndege hizo.
Ila Caine anasema mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kutoka Iran yamepungua kwa 73% tangu siku ya kwanza ya vita. Iran inaonekana kulemewa kudumisha kasi ya oparesheni zake.
Inaonekana kuwa Iran kupunguza kiwango cha mashambulizi ni njia moja ya kuhifadhi silaha walizonazo, ila pia kuzalisha silaha hizo kwa muda mfupi ni changamoto.
Ndege za kivita za Marekani na Israel sasa zina ubabe wa anga juu ya Iran. Sehemu kubwa ya mifumo ya ulinzi wa anga ya Iran imeharibiwa. Haina tena jeshi la anga linaloweza kudhibiti mashambulizi makali.
Centcom inasema kuwa awamu inayofuata ya vita inalenga kutafuta na kuharibu vifaa vya kurusha makombora na ndege zisizo na rubani za Iran, maghala yake ya silaha, pamoja na kuharibu viwanda vinavyozalisha silaha hizo.
Huenda sasa ikawa rahisi zaidi kwa Marekani na Israel kudhoofisha uwezo wa Iran wa kupigana. Lakini itakuwa vigumu kuharibu akiba yake yote ya silaha.
Iran ni nchi yenye ukubwa mara tatu ya Ufaransa. Silaha bado zinaweza kufichwa zisionekane kutoka angani.
Historia ya hivi karibuni pia inaonyesha mipaka ya vita vinavyopiganwa kutoka angani. Jeshi la Israel bado halijaangamiza Hamas huko Gaza baada ya zaidi ya miaka mitatu ya mabomu makali.
Waasi wa Houthi nchini Yemen walinusurika kurushiwa mabomu ya Marekani kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Marekani
Marekani bado ina jeshi lenye nguvu zaidi duniani. Akiba yake ya silaha za kawaida ni kubwa zaidi kuliko za nchi nyingine yoyote duniani.
Hata hivyo, jeshi la Marekani bado linategemea kwa kiasi kikubwa silaha ghali zinazotengenezwa kwa umakini, ambazo huzalishwa kwa idadi ndogo. Inaripotiwa kuwa Trump ameita mkutano na wakandarasi wa ulinzi baadaye wiki hii ili kuwahimiza kuharakisha uzalishaji wa silaha hizo. Hii ni ishara kwamba hata rasilimali za kijeshi za Marekani zinaweza kuwa zimepungua.
Caine anasema kuwa Marekani tayari imeacha kutumia "silaha za masafa marefu" silaha ghali na za hali ya juu kama makombora ya Tomahawk na sasa imeanza kutumia "silaha za masafa fupi" ambazo ni nafuu zaidi.
Jeshi la anga la Marekani sasa linatumia mabomu ya JDAM ambayo ni ya gharama ya chini zaidi na yanaweza kurushwa kutoka juu na kulenga eneo lililokusudiwa.
Mark Cancian, kanali mstaafu wa jeshi la wanamaji la Marekani katika kituo cha mafunzo ya kimkakati na kimataifa (CSIS) chenye makao yake Washington, anasema kwamba baada ya shambulio la awali la masafa marefu, Marekani "sasa inaweza kutumia makombora na mabomu ya gharama nafuu zaidi".
Anasema Marekani inaweza kuendeleza kiwango hicho cha mapigano "bila kikomo". Kadri vita vinavyoendelea ,orodha ya wanaolengwa hupungua, na kupunguza kasi ya vita.
Ulinzi wa anga
Mark Cancian anasema kuwa Marekani ina maelfu ya mabomu ya JDAM, lakini viwango vya mifumo ghali ya ulinzi wa anga imepungua. Katika hatua za awali za vita hivi, silaha hizo zimekuwa muhimu katika kukabiliana na tishio la mashambulizi ya kulipiza kisasi kutoka Iran.
Makombora aina ya Patriot yamekuwa yakihitajika sana si tu na Marekani, bali pia na washirika wake wa Kiarabu na Ukraine. Kila kombora la kuzuia shambulizi hugharimu dola milioni 4, na inaaminika kuwa Marekani kwa sasa huzalisha takribani makombora hayo 700 kila mwaka.
Ikiwa Iran bado ina uwezo wa kurusha makombora ya kibalistiki, hali hiyo huenda ikapunguza hifadhi ya Marekani.
Cancian, anakadiria kuwa Marekani inaweza kuwa na hifadhi ya karibu misururu ya makombora 1,600 ya Patriots, ambayo imekuwa ikitumika na huenda hifadhi yake imepungua.
Ingawa anasema Marekani inaweza kuendelea na vita vya anga kwa "muda mrefu", vita vya ulinzi wa anga ni "changamoto kubwa".
"Kama Rais Trump yuko tayari kupunguza idadi ya Patriots, basi nadhani tunaweza kudumu zaidi kuliko Iran lakini itakuja na hatari katika mgogoro unaowezetokea wa eneo la Pacifc."
Trump anatarajiwa kukutana na makampuni ya kutengeneza silaha za ulinzi nchini Marekani baadaye wiki hii , hii ikiwa ishara kuwa kuna wasiwasi kuhusu akiba ya silaha.
Hata hivyo, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth anasisitiza kwamba "Iran haiwezi kuhimili vita hivyo kwa muda mrefu", akieleza imani yake kwamba jeshi la Marekani lina uwezo wa kuendelea na mapigano kwa muda mrefu zaidi kuliko Iran licha ya hofu kuhusu akiba yao ya silaha