Jinsi mpango wa kiuchumi na msukosuko wa kisiasa ulivyommaliza Liz Truss kisiasa

Liz Truss aliingia madarakani akiahidi enzi mpya ya kiuchumi na kisiasa.

Ni siku 45 tu tangu awe waziri mkuu – na kuhudumu kwa mfupi zaidi katika historia ya Uingereza.

Na pia kipindi hicho kilishuhudia ubahatishaji mkubwa katika kihistoria ya kiuchumi, kilishuhudia kwenda mbele na kurejea nyuma mara nyingi tu na kufutwa kabisa kwa mpango mzima wa kisiasa.

Imekuwa muda mfupi.

Lakini haijawa rahisi kabisa.

Katika msimu wa joto, kila kitu kilihisi tofauti sana.

Tulipokuwa tukizunguka Uingereza kwa ajili ya kampeni, ilikuwa wazi kwamba Bi Truss alikuwa maarufu sana kwa wanachama wa Conservative.

Ahadi zake za kupunguza ushuru na kutawala kama mhafidhina ndio hasa walitaka kusikia.

Hakuwa mwigizaji wa vyombo vya habari asiye na dosari, lakini alijua jinsi ya kushirikiana na umati wa watu kwa urafiki.

Kulikuwa na maonyo kutoka kwa Kansela wa zamani Rishi Sunak na wafuasi wake kwamba mipango yake ya kiuchumi ilikuwa hatari na inaweza isifaulu.

 Wengine walisema itakuwa ni kama kujimaliza kisiasa.

Lakini walishindwa katika mazungumzo ndani ya Chama cha Conservative.

Huku ushindi ukiwa umekaribia, pamoja na rafiki yake wa karibu na mshirika wake wa kisiasa Kwasi Kwarteng, Bi Truss alipata kazi ya kuunda mpango wa mamlaka ambao ungekuwa wenye kuleta mabadiliko na wa ujasiri.

Waliamua kuwa wangevunja sheria, ambazo zilikuwa zimefuatwa na mawaziri wakuu wa zamani wa chama hicho.

Utamaduni uliozoeleka katika suala la ‘kiuchumi’ ulitupiliwa mbali.

Walitayarisha kile wasaidizi walichoita ‘’mipango mikubwa’’ yenye kuleta mafanikio kwa haraka.

‘’Hatutakuwa tukibahatisha’’, mkuu mmoja katika Timu ya Truss alijigamba.

Bi Truss alijifananisha na Waziri Mkuu wa zamani Margaret Thatcher.

Washirika wake walisema kwamba kama waziri mkuu wa zamani, Bi Truss angekuwa na uthabiti madarakani.

Mwanamke huyo hakuwa wa kurejea nyuma.

Waliweka wazi kuwa angefanya maamuzi ambayo hayakupendwa na watu wengi na kushikamana nayo, liwe liwalo.

Bi Truss alitaka kuwa mwanamke mpya shupavu.

Ndani ya saa 48 ikaja mfululizo wa kwanza wa kubahatisha katika suala la kiuchumi, na kwenda mbali zaidi kuliko karibu kila mtu alivyotarajia.

Kwanza kulikuwa na kifurushi cha msaada wa nishati, ambacho kiliahidi kupunguza bei kwa miaka miwili.

Kwa mgombea ambaye alisema hakutakuwa na cha kufurahisha umma kiuchumi, ukweli wa kisiasa ukawa umeanza kujitokeza na ufuatiliaji wa kinachoendelea kwa makini ikawa umeanza.

Lakini ndani ya masaa machache, siasa bungeni ilibidi zitulie kidogo.

Bi Truss aliambiwa katika Bunge la Wawakilishi kwamba Malkia alikuwa mgonjwa.

Mwisho wa siku, waziri mkuu aliyekuwa ofisini kwa siku mbili alikuwa tena bungeni akitoa heshima kwa malkia aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi katika historia ya Uingereza.

Katika siku chache zilizofuata, lengo la serikali lilikuwa maombolezo ya kitaifa.

Baadaya mazishi ya Malkia, Bi Truss alilazimika kurudisha wakati uliopotea.

Aliendelea na safari yake ya kwanza na ya pekee ya kidiplomasia katika Umoja wa Mataifa mjini New York, ambako aliwaambia watangazaji kuwa yuko tayari kufanya maamuzi magumu katika kutafuta ukuaji wa uchumi.

Aliporudi ikawa sasa wakati umewadia wa ‘’mabadiliko yake makubwa kiuchumi’’ ambayo alikuwa akifikiria kwa miaka.

Bajeti yake ndogo - ambayo haikuwa ndogo - ilikuwa mabadiliko makali zaidi katika historia ya hivi karibuni.

Kodi zilipunguzwa, haswa kwa waliolipwa zaidi.

Ingefadhiliwa kwa kukopa, licha ya maonyo kwamba hilo lingeweza kusababisha mfumuko wa bei kuwa mbaya zaidi.

Wakuu bungeni waliamini kuwa walikuwa karibu kuzindua enzi mpya nzuri kwa uchumi wa Uingereza.

Waliopendelea uhuru wa kiuchumi walikuwa na nafasi yao na walikuwa wamedhamiria kuichukua.

Mmoja aliniambia: ‘’Kitu tofauti na cha ujasiri kinahitajika kufanywa.’’

Timu ya Truss iliamini kuwa masoko yangeipa nchi nafasi ya kurekebisha uchumi.

Lakini ndani ya siku chache - ikawa wazi kwamba walikuwa wamekosea na mpango wao wa kiuchumi ukaanza kufeli.

Kulikuwa na maelezo machache kuhusu jinsi serikali ingefadhili kifurushi hicho, na kucha masoko ya fedha yakiyumba, na kusababisha pauni kuporomoka, na kuilazimisha Benki ya Uingereza kuokoa fedha za pensheni.

Wabunge wa chama walianza kuwa na wasiwasi.

Ndani ya saa 72 za bajeti ndogo, wengi walikuwa wakiweka wazi kwamba hawakuwa wamefurahia.

Wabunge wa chama cha kihafidhina walizungumza kwa faragha kuhusu serikali ambayo tayari inazusha mzozo wa kisiasa.

Katika wiki ijayo, hiyo ingeongezeka hadi mzozo kamili utokee kwenye mkutano wa Chama cha Conservative huko Birmingham.

Kufikia wakati Bi Truss aliwasili, ilikuwa wazi kulikuwa na uasi mkubwa juu ya uamuzi wa kufuta kiwango cha juu cha ushuru.

Chini ya shinikizo kutoka kwa wabunge wa kawaida tu, Bi Truss akajimaliza kisiasa.

Siku hiyo hiyo, aliiambia BBC kuwa hatabadili mawazo yake.

Alimtuma kansela kueleza uamuzi huo.

Mpango huo ulitakiwa kuonyesha kuwa Bi Truss alikuwa akisikiliza.

Wabunge waliamini kuwa ungeruhusu wabunge waasi kuendelea.

Badala yake, ilifanya kinyume kabisa.

Waasi wakatumia fursa hiyo kwa faida yao.

“Inahisi kama siku za mwisho za Roma,” akasema waziri mmoja wa zamani.

Katika muda wa wiki chache zilizofuata, mamlaka ya Bi Truss yaliporomoka kabisa.

Alimfukuza kazi kansela wake na akafutilia mbali mpango wa kupunguza ushuru wa shirika.

Alimteua Jeremy Hunt kusimamia Hazina - mtu ambaye alikuwa amemuunga mkono Bw Sunak.

Bw Hunt aliamua Jumamosi kwamba mkakati mzima wa kiuchumi unapaswa kufutwa na kumwambia waziri mkuu siku iliyofuata.

Akiwa amedhoofishwa na matukio, hakuwa na chaguo ila kukubali.

‘’Jeremy Hunt ni Waziri Mkuu,’’ alisema mbunge mmoja, akizungumza na wengi.

‘’Sioni maana yake,’’ aliongeza mwingine.

Kufikia Jumapili, hali ilikuwa inaelekea kuunga mkono kuhitimisha mwisho wa uwaziri mkuu wa Bi Truss.

BBC iliwasiliana na wabunge wengi na hali ilikuwa giza.

Hakuna mtu aliyekuwa akipendekeza mamlaka ya Bi Truss yangepona.

Mwaminifu mmoja wa Bi Truss aliniambia: ‘’Tumepoteza’’.

Mbunge mmoja mwandamizi wa chama aliongezea huku hali ikiendelea kubadilika: ‘’Watu wanajua kuwa uongozi wake umekwisha. Ni swali la jinsi gani na lini’’.

Hata hivyo, bado kulikuwa na mwanga wa matumaini kwa Bi Truss.

Baadhi ya wabunge walikuwa na hofu ya kumwangusha waziri mkuu bila kuwa na mgombea wanaemuunga mkono kuchukua nafasi yake.

Waliogopa ingemaanisha machafuko zaidi, ambayo hakuna mtu angeweza kudhibiti.

Baadhi ya wakosoaji wa ndani wa Waziri Mkuu walihimiza tahadhari.

Kama mtu mmoja mkuu alivyonieleza: Mustakabali wa Bi Truss unaweza kuamuliwa na kile ambacho wapinzani wake hawawezi kufanya katika hatua hii.

Lakini kilichofuata ni unyonge zaidi.

Siku ya Jumatatu, Bw Hunt alichukua udhibiti na kufutilia mbali mpango wa kiuchumi.

Waziri Mkuu alikejeliwa sana kwa kutozungumza mwenyewe Bungeni.

Alikwepa swali la dharura kutoka kwa kiongozi wa chama cha Labour, kisha akaketi kando ya kansela kwa muda mfupi alipokuwa akivuruga mpango wake wa kiuchumi katika Bunge la Wawakilishi.

Siku chache baadaye, katibu wa mambo ya ndani alijiuzulu kwa kukiuka kanuni za mawaziri - lakini alianzisha mashambulizi makali dhidi ya waziri mkuu na mpango wake.

Kulikuwa na matatizo katika upande wa kulia wa chama, ambacho kilikuwa kimemfanyia kampeni Bi Truss kweli kweli.

Fimbo ya mwisho kwa Wabunge wa Conservative yalikuwa machafuko juu ya kura ya kupiga marufuku mfumo fulani wa kuongeza mafuta na gesi.

Wabunge waliambiwa ni kura ya kutokuwa na imani - kwamba kwa kutopiga kura na serikali, walikuwa wanasema hawataki iendelee.

Kisha wakaambiwa haikuwa suala la kutokuwa na imani.

Kisha wakaambiwa huo ndio ukweli - na wale walioasi wataadhibiwa.

Yote ilimaanisha kuwa kufikia Alhamisi asubuhi, Chama cha Conservative kilikuwa kimebadilika.

Waziri mkuu alipomwita Sir Graham Brady, mwenyekiti wa kamati ya 1922, ili kupima hali ya chama, ilikuwa mchezo umekwisha.

Enzi mpya ya uchumi ilikuwa imekwisha.

Saa ishirini na nne baada ya kusema yeye ni mpiganaji, alijiuzulu.

Bi Truss alishindwa, ‘mpango wake wa kuleta ‘’mabadiliko makubwa kiuchumi’’ ulikuwa umeporomoka.

Machafuko yakafafanua muda wa Bi Truss kuwa ofisini.

Katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja, kumekuwa na makansela wanne, na kufikia wiki ijayo kutakuwa na mawaziri wakuu watatu wamehudumu.

Chama cha Conservatives sasa kinapaswa kumchagua kiongozi wanayefikiri anaweza kuleta uthabiti.

Yeyote atakayekuwa, atataka kudumu kwa muda mrefu zaidi kuliko Bi Truss.

Tazama safari fupi na ngumu ya Waziri Mkuu wa Uingereza ndani ya sekunde 90