Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mapungufu ya mifumo ya intaneti barani Afrika na jinsi ya kuyarekebisha
Na Jewel Kiriungi ,
BBC News, Nairobi
Kukatika kwa intaneti kwa kiasi kikubwa ambako kumekumba mataifa kadhaa ya Afrika - ikiwa ni hitilafu ya tatu kushuhudiwa katika kipindi cha miezi minne - ni ukumbusho wa jinsi huduma hiyo ilivyo hatarini katika bara hili.
Maswali yanaulizwa kuhusu jinsi kutegemewa kwa kile ambacho kimekuwa chombo muhimu katika karibu kila nyanja ya maisha na jinsi uboreshaji unavyoweza kufanywa .
Kukatwa kwa nyaya mbili za chini ya bahari, ambazo husafirisha data kote barani, mapema Jumapili asubuhi, kumesababisha usumbufu wa hivi karibuni.
Mwezi Machi, uharibifu wa nyaya nne katika pwani ya Afrika Magharibi ulisababisha matatizo kama hayo.
Na mnamo Februari, viungo muhimu viliharibiwa katika Bahari ya Shamu baada ya nanga ya meli iliyopigwa kukokotana kuzivuruga nyaya tatu.
Uchunguzi unaendelea kuhusu kisa cha wikendi hii.
Lakini pia huenda ilisababishwa na "kuburutwa kwa nanga" kutoka kwa meli, Prenesh Padayachee, afisa mkuu wa kitengo cha dijitali na uendeshaji katika Seacom, ambayo inamiliki moja ya nyaya mbili zilizoathirika, aliiambia BBC.
Kebo ya pili, inayojulikana kama Eassy, iliathiriwa kwa wakati mmoja na mahali pamoja.
Tukio hilo lilitokea katika pwani ya Afrika Kusini, kaskazini mwa mji wa bandari wa Durban, kulingana na Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya (CAK).
Uwezo wa miundombinu inayounganisha Afrika na dunia nzima umeimarika katika miaka ya hivi karibuni na makampuni ya mawasiliano yanabadilisha nyaya nyingine ili kudumisha huduma hiyo.
Nchini Kenya, kwa mfano, CAK ilisema kwamba trafiki ya ndani ya mtandao kwa sasa ilikuwa ikitumia kebo ya Mfumo wa Baharini wa Afrika Mashariki (Teams) ambayo haikuathirika.
Wakati Kenya ina njia mbadala, nchi nyingine, kama vile Tanzania ambako viwango vya uunganisho vilifikia 30% ya kile walichotarajiwa kuwa, hawana mbadala.
Data inapaswa kuwa na uwezo wa kupata njia zingine, lakini kunapokuwa na idadi ndogo ya njia huduma hukwama na kupungua.
Visa vya uharibifu wa kebo vinaongezeka lakini hiyo ni kwa sababu idadi ya viunganisho pia imeongezeka.
"Watu wengi hawatambui kuwa mtandao umeshikiliwa na nyaya hizi ambazo ni kama mabomba ya bustani isipokuwa ni moja ambayo ina urefu wa kilomita 10,000, na hiyo ina maana kwamba ni tete," Dk Jess Auerbach Jahajeeah, mtafiti wa kidijitali katika Chuo Kikuu cha Cape Town, aliambia kipindi cha BBC Focus on Africa.
Kukokotwa kwa nanga kutoka kwa meli karibu na ufuo ni mojawapo ya sababu za kawaida za uharibifu, lakini maporomoko ya mawe chini ya maji, kama ilivyoaminika kuwa katika kisa cha Afrika Magharibi mwezi Machi, na shughuli za tetemeko pia zinaweza kuathiri nyaya.
Kwa kuwa "kebo nyingi za chini ya bahari mara nyingi huwa karibu sana, basi shughuli moja kwenye sakafu ya bahari au meli moja inaweza kuharibu nyaya nyingi kwa wakati mmoja", mtaalam wa tasnia hii Ben Roberts anasema.
Marekebisho wa uharibifu unaohitaji vifaa maalum na utaalamu, unaweza kuchukua siku au wiki kadhaa kulingana na hali ya hewa, hali ya bahari na ukubwa wa tatizo.
Ilichukua zaidi ya mwezi mmoja, kwa mfano, kwa nyaya nne za mtandao za Afrika Magharibi zilizokatwa kukarabatiwa na kurejeshwa kutumika.
"Tunashughulikia suluhisho la muda la uwezo ili kuhakikisha muunganisho umerejeshwa kwa maeneo yaliyoathiriwa," alisema Bw Padayachee kutoka Seacom.
Aliongeza kuwa "wanashirikiana kikamilifu na wadau mbalimbali ili kuharakisha mchakato wa ukarabati".
Meli ya kutengeneza kebo ya Léon Thévenin, iliyokuwa imetia nanga mjini Cape Town, inatumwa kwenye eneo la uharibifu na inapaswa kuwa huko baada ya siku tatu, alisema Chris Wood, ambaye anaendesha kampuni ambayo imewekeza katika Eassy.
Licha ya kuzidi kwa miunganisho, utegemezi wa Afrika kwa idadi ndogo ya nyaya za chini ya bahari kwa mtandao hufanya bara hili kuathiriwa zaidi na usumbufu na kuzidisha athari zao.
Ulaya na Amerika Kaskazini, kwa upande mwingine, zina mtandao mzito wa nyaya za ardhini na chini ya bahari zenye uwezo wa juu ambazo hubadilisha njia za uunganisho na kuboresha ustahimilivu.
Wakati majadiliano yamekuwa yakiendelea kushughulikia changamoto za miundombinu ya mtandao barani Afrika, hatua zimekuwa za polepole kwa sababu ya vikwazo vya vifaa na kifedha.
Dk Jahajeeah alisema tatizo moja ni kwamba mifumo ya kusaidia kukarabati idadi inayoongezeka ya nyaya kote barani haijaendana na ukuaji huo.
Ingawa meli nyingine zinaweza kusaidia, Léon Thévenin ndiyo meli pekee ya ukarabati iliyojitolea kuhudumia Afrika.
"[Meli] ilikuwa ikifanya matengenezo mawili au matatu kwa mwaka [lakini] mwaka jana ilifanya tisa ... na kuna haja ya kweli kwa serikali za Afrika na serikali za kimataifa kuungana na kusema tunahitaji kuhakikisha kuwa hakuna mgawanyiko wa kidijitali. ,” Dk Jahajeeah alisema.
Baadhi ya watu wamependekeza njia mbadala kama vile viungo vya mtandao vya setilaiti ili kuimarisha uthabiti wa kidijitali.
Mradi wa Starlink wa Elon Musk, kwa mfano, unalenga kutoa intaneti ya kasi ya juu kwa watu wanaoishi maeneo ya mbali kupitia mtandao wa satelaiti. Lakini ni ghali sana na kwa sasa haipatikani kila mahali.
Jibu la kweli liko katika uwekezaji mkubwa zaidi wa kusaidia miundombinu muhimu ya mawasiliano.
"Inahitaji mitandao zaidi, muunganisho zaidi, vituo zaidi vya data na ubadilishanaji wa intaneti zaidi ili kuhakikisha kuwa tuna muunganisho wa aina mbalimbali," alisema Bw Roberts.
Kebo za chini ya bahari barani Afrika
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah