“Nilipigwa viboko kwa sababu ya picha katika mtandao wa kijamii nchini Iran”

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Reha Kansara and Ghoncheh Habibiazad
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Onyo: Makala hii ina maelezo ya vurugu. Baadhi ya majina yamebadilishwa ili kulinda utambulisho wao.
Wanawake nchini Iran wameiambia BBC jinsi shughuli zao za mtandaoni zinavyofuatiliwa na serikali, na kusababisha kukamatwa, vitisho na kupigwa.
Iran iliongeza uangalizi kufuatia maandamano yaliyoongozwa na wanawake kote nchini humo, baada ya kifo cha Mahsa Amini akiwa chini ya ulinzi wa polisi miaka miwili iliyopita.
Akiwa na umri wa miaka 22, Mahsa alikamatwa kwa madai ya kutovaa hijabu yake vizuri.
Kama wanawake wengine waliochochewa na maandamano hayo, Alef alichapisha picha kwenye mitandao ya kijamii akionyesha nywele zake. Ni kitendo cha kuonyesha mshikamano wa kupinga kulazimishwa kuvaa hijabu.
"Sikujali, sikujificha wala sikuficha mahali ambapo picha ilipigwa," anasema. "Nilitaka kusema, 'tupo'."
Picha hiyo iliifikia serikali, na Alef alikamatwa. Anasema alifungwa macho, pingu na kupelekwa kusikojulikana ambako alikaa kwenye kifungo cha upweke kwa karibu wiki mbili. Pia alihojiwa mara nyingi.
Katika mahojiano, anasema wachunguzi walijaribu kumlazimisha kuungama. Alilazimishwa kukabidhi simu yake kwa walinzi waliojifunika nyuso zao, ambao walipitia machapisho na picha zake kwenye mitandao ya kijamii.
Picha zilionyesha alishiriki katika maandamano na alipigwa risasi ya marisawa na vikosi vya usalama. Waliomuhoji pia walimshutumu kwa kufanya kazi kwa niaba ya Marekani.
Alef alishtakiwa, miongoni mwa mambo mengine, ni "kujitokeza hadharani bila hijabu na kuhamasisha uharibifu na uasherati.”
Alipatikana na hatia. Ingawa adhabu yake iliahirishwa, lakini alichapwa viboko 50.
"Afisa mmoja wa kiume aliniambia nivue koti langu na nilale chini. Alikuwa ameshika mjeledi mweusi wa ngozi na kuanza kunipiga mwili mzima. Iliuma sana lakini sikutaka kuonyesha udhaifu.”
Mkasa wake unafanana na wa wanawake wengine wawili na mwanaume mmoja – ambao tulizungumza nao nchini Iran. Kila mmoja alituambia walikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kufanya "propaganda dhidi ya serikali."
Wote walipewa vifungo vya jela vilivyosimamishwa.
Hali mbaya Jela

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wawili kati ya watu tuliozungumza nao walizuiliwa katika Gereza maarufu la Evin la Tehran - linalojulikana kwa kuwahifadhi wafungwa wengi wa kisiasa kabla ya kushitakiwa na kuhukumiwa.
Wote wawili walielezea hali mbaya ya maisha ambapo wafungwa wanasongamana kwenye seli ndogo, zisizo safi na zenye baridi, huku kukiwa na uhaba wa bafu na choo, jambo ambalo mara nyingi husababisha watu kuugua.
Mwanaume mmoja mwenye ushawishi katika mitandao ya kijamii, ambaye alizuiliwa kwa chini ya mwezi mmoja tu, alituambia katika seli yake kulikuwa na bafu moja tu na choo kimoja cha takribani watu 100.
Mwanamke mmoja, Maral, aliyeshikiliwa kwa zaidi ya miezi miwili, alisema mahali alipokuwa kizuizini wanawake huoga mara moja au mbili tu kwa wiki. Hali ilikuwa ngumu sana walipokuwa na hedhi.
"Wakati mwingine ilichukua muda mrefu hadi kuturuhusu kwenda chooni," alisema. "Tukilalamika husema, 'ukitoa ushirikiano, unaweza kuondoka mapema.'
Mitandao ya kijamii ya Kosar Eftekhari pia ilipekuliwa. Alikamatwa na kushtakiwa kwa makosa ikiwa ni pamoja na "propaganda dhidi ya serikali", "kutusi imani takatifu", "kusumbua umma", na "kufuru."
Kupoteza jicho

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwezi mmoja baada ya kifo cha Mahsa Amini, Kosar alipigwa risasi ya mpira katika sehemu yake ya siri na afisa wa kikosi cha kutuliza ghasia. Muda mfupi baadaye alimpiga risasi tena, wakati huu jichoni. Akiwa na tabasamu usoni, ghafla aliona jicho lake la kulia likidondoka na akawa kipofu.
Tukio hilo baya lilirekodiwa na kuwekwa kwenye Instagram. Licha ya majeraha na kiwewe, Kosar aliendelea kuwepo zaidi mtandaoni, na kumfanya kuwa shabaha kuu ya ufuatiliaji kuongezwa.
Anasema katika kesi yake, mamia ya machapisho yake kwenye mitandao ya kijamii, zikiwemo picha zake bila hijabu, zilitumiwa kama ushahidi na mwendesha mashtaka.
Kosar alipatikana na hatia na kuhukumiwa miaka minne na miezi mitatu jela. Pia alipigwa marufuku kutumia mitandao ya kijamii na simu janja kwa miaka mitano.
Ili kuepuka kutumikia kifungo Kosar alikimbilia Ujerumani, ambako sasa anatetea wanawake wa Iran. Mapema mwaka huu alizungumza na Ujumbe wa Kutafuta Ukweli wa Umoja wa Mataifa kuhusu Iran (FFMI), kuhusu yaliyompata na kile walichokiita "uhalifu dhidi ya ubinadamu."
FFMI iliiambia BBC "hakuna mtu anayepaswa kufungwa kwa chapisho la amani mtandaoni."
Tulipeleka madai yaliyotolewa na watu watano tuliozungumza nao kwa serikali ya Iran lakini hawakujibu. Kamanda wa polisi wa kutuliza ghasia nchini Iran hapo awali alikanusha vikosi vyake kuwapiga risasi waandamanaji usoni kwa makusudi.
Mfumo wa ufuatiliaji

Chanzo cha picha, Getty Images
Serikali ya Iran imezuia maandamano kwa miaka mingi, wanaona kuwa ni shughuli za uasi. Wamefanya hivyo kwa kuongeza udhibiti wa serikali juu ya maisha ya watu mtandaoni.
Wamezima intaneti mara nyingi na inasemekana walitumia mbinu za kuhadaa ili kudukua simu na kupata taarifa za watu.
Mitandao ya kijamii ya Magharibi kama Instagram, X na Telegram imezuiwa, lakini Wairani wengi wamekwepa hilo kwa kutumia VPN, ambayo huwasaidia kuficha eneo lao walipo na kuweza kutumia mitandao hiyo.
Wimbi la hivi karibuni la maandamano lilienea kupitia majukwaa haya. Lakini kutokana na ufuatiliaji, maelfu ya waandamanaji walikamatwa ndani ya miezi michache ya kwanza.
Mtafiti mkuu katika shirika la haki za binadamu liitwalo Article 19, Mahsa Alimardani anasema wengi wa waandamanaji walikuwa ni Gen Z na hutumia sana mitandao, ambapo kazi ya kuwafuatilia kupitia mitandao ya kijamii kabla na wakati wa kuwekwa kizuizini ilikuwa rahisi.
Serikali pia imeunda programu, inayoitwa Nazer, ambayo inaruhusu polisi na watu wa kujitolea waliopitishwa na serikali kuripoti wanawake kwa kutovaa hijab.
Miaka miwili baada ya kifo cha Mahsa Amini, upinzani kupitia mitandao ya kijamii chini ya kauli mbiu, Woman Life Freedom, hauonyeshi dalili za kukoma.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












