Ni suala la muda tu kabla ya Mbappe kutawala Real Madrid

Muda wa kusoma: Dakika 4

Baada ya miezi kadhaa ya uvumi, hatimaye Kylian Mbappe alijiunga na Real Madrid, kufuatia kumalizika kwa mkataba wake huko Paris St-Germain.

Ametia saini mkataba hadi 2029, akipata pauni milioni 12.8 kwa msimu, pamoja na bonasi ya usajili ya pauni milioni 128 kulipwa kwa miaka mitano.

Lakini Mbappe ataingiaje katika safu ya mabingwa hao wa Ulaya, wakati huu safu yao ya ushambuliaji imejaa nyota kama Vinicius Junior, Rodrygo, Jude Bellingham na chipukizi wa Brazil, Endrick?

Watu wa ndani wa Real Madrid wameshangazwa na unyenyekevu, tabia nzuri na mafanikio ya Mbappe tangu kuwasili kwake - ingawa haijawashangaza wanaomfahamu vyema.

Akiwa na umri wa miaka 18 katika klabu ya PSG chini ya meneja Unai Emery, aliiambia klabu hiyo sio tu kwamba alipaswa kucheza kila mechi bali pia nafasi ambayo alipaswa kucheza.

Akiwa na Real Madrid anacheza nambari tisa. Meneja Carlo Ancelotti amempa ruhusa ya kuhama anavyotaka, lakini anapoelekea upande wa kushoto anaishia kukutana na Vinicius.

Amefunga mabao manne katika mechi sita, mabao mawili amefunga kwa mikwaju ya penalti. Katika mechi kubwa Ancelotti atamchezesha Vinicius, Mbappe na Rodrygo upande wa mbele. Lakini katika mechi za kawaida, kama ile ya ushindi wa Jumamosi wa 2-0 dhidi ya Real Sociedad, Madrid hucheza 4-4-2, hivyo Vinicius na Mbappe wanaweza kuamua nani atafanya nini na nani aende wapi.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufunga mabao mawili dhidi ya Real Betis, Mbappe alisema: "Mimi ndiye napaswa kuzoea mazingira. Mchezaji kama mimi anapofika, mambo mengi yanabadilika na itakuwa ajabu kama nisingefikiria kupambana na mabadiliko hayo."

Katika ushindi wao wa 2-0 dhidi ya Real Betis mwanzoni mwa mwezi huu, Vinicius alitoa nafasi kwa Mbappe kupiga penalti. Dhidi ya Real Sociedad.

Ancelotti amesema wachezaji wanaweza kuamua kati yao wenyewe, na Mbappe amefurahishwa na hilo kwa sababu anaamini yuko katika klabu ambayo itaimarisha thamani na ujuzi wake.

Ujio wa Mbappe

Kuna athari za ujio wa Mbappe - umemfanya Rodrygo kujihisi kusukumwa kando kidogo, ndani na nje ya uwanja. Madrid pia italazimika kubainisha ni jukumu gani Bellingham atakuwa nalo baada ya kupona majeraha.

Kibiashara, Mbappe yuko kila mahali. Amehifadhi asilimia 80 ya haki zake za kibiashara, ingawa asilimia hiyo inatofautiana kulingana na sehemu ambayo klabu hiyo inatazamia kuuza bidhaa zake.

Mechi ya wikendi iliyopita dhidi ya Real Sociedad ilikuwa ya kwanza kati ya mechi saba watakazocheza ndani ya siku 21 - tano kwenye La Liga na mbili za Ligi ya Mabingwa.

Tulichoona ni Mbappe, anaekimbia kwenye pembe zote za safu ya mbele, alikimbia zaidi na mpira kuliko katika mchezo mwingine wowote akiwa na Madrid, akashuka zaidi na kuchukua mipira zaidi.

Vinicius na Mbappe hawakupeana pasi nyingi katika mechi za kwanza za msimu, lakini ulikuwa mchezo mzuri wa mwishoni mwa wiki.

Na kwa upande wa klabu - ingawa inaweza kuchukua muda mrefu zaidi kumweka Mbappe katika kundi la wachezaji bora zaidi duniani, kila mtu anaamini ni suala la muda tu kabla ya kuwa nyota mkuu katika klabu kubwa zaidi duniani.

Kylian Mbappe wawili

Kuna Mbappe wawili; mmoja akilenga kujiimarisha huko Madrid, na mwingine anayepambana kudumisha nafasi yake katika timu ya taifa ya Ufaransa.

Mambo yalizidi kuwa mabaya hivi karibuni pale Ufaransa ilipochapwa nyumbani katika mechi ya Ligi ya Mataifa dhidi ya Italia.

Baada ya kipigo cha mabao 3-1, kipa wa Ufaransa Mike Maignan alianzisha mashambulizi makali dhidi ya timu nzima, ikiwa ni pamoja na, bila kutaja majina, nyota wanaojiita (Mbappe na Antoine Griezmann), akiwalaumu kwa kukosa hamu na ari.

L'Equipe, shirika lenye nguvu la vyombo vya habari vya michezo nchini Ufaransa, limesema Mbappe, kwa sasa hana maingiliano na timu ya Ufaransa.

Saa chache kabla ya mechi dhidi ya Ubelgiji, Mbappe aliviambia vyombo vya habari, anaamini timu hiyo inahitaji mbinu bora zaidi ili kuwaruhusu wachezaji kuzoea kile ambacho kocha anahitaji, jambo ambalo wengi waliona kama ukosoaji dhidi ya meneja Didier Deschamps.

Katika klabu yake ya zamani na nchi, alikuwa hawezi kuguswa na lawama. Alikuwa alama ya jiji la Paris, shujaa wa taifa kwa kukaa PSG hadi Michezo ya Olimpiki, kitu ambacho alikifanya baada ya kupata shinikizo kubwa kutoka kwa kila mtu, pamoja na Rais Emmanuel Macron.

Tangu aondoke Ufaransa, umekuwa msimu wa mashambulizi kwa mchezaji huyo kutoka kwa mashabiki, vyombo vya habari na haswa klabu ambayo ina takribani sababu milioni 46 za kutaka kuongeza chuki dhidi ya kijana wao wa zamani - Mbappe anasisitiza PSG ina deni lake la pauni milioni 46 na mishahara yake na malipo ya bonasi.

Klabu hiyo haikubaliani na hilo, inasema aliachana na pesa hizo ili ajumuishwe kwenye kikosi alichokuwa ameondolewa katika ziara ya PSG, wakati wa kujiandaa na msimu mpya nchini Japan.

Kwa sasa ligi hiyo imeamua kumuunga mkono mchezaji huyo na kuiamuru klabu hiyo kumlipa fedha hizo ambazo PSG itakata rufaa dhidi yake.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah