Mpangaji mkuu wa tukio la wafungwa kutoroka gerezani nchini India

Chanzo cha picha, Swastik pal
- Author, Soutik Biswas
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Jioni ya Jumapili tulivu Novemba 2005, mwandishi wa habari katika jimbo la Bihar nchini India alipokea simu ya mshituko akiwa nyumbani.
"Maoists wameshambulia gereza. Watu wanauawa! Nimejificha chooni,” mfungwa mmoja alisema kwenye simu huku sauti yake ikitetemeka na milio ya risasi ikisikika kwa nyuma.
Alikuwa akipiga simu kutoka jela ya Jehanabad, iliyo katika wilaya masikini, na wakati huo, ilikuwa ni ngome ya itikadi kali za mrengo wa kushoto.
Gereza la matofali mekundu la tangu enzi ya ukoloni lililokuwa limejaa wafungwa lilivunjwa. Ni gereza lililoenea katika ekari moja, lina majengo 13, lina giza na chafu. Hapo awali lilijengwa kwa ajili ya wafungwa 230, lakini kisha likawa na hadi wafungwa 800.
Uasi wa Maoist, ambao ulianza katika kitongoji cha Naxalbari, katika jimbo la Bengal Magharibi mwishoni mwa miaka ya 1960, ulienea katika sehemu nyingi za India, pamoja na Bihar.
Kwa takribani miaka 60, wapiganaji wa msituni – ambao pia waliitwa Naxalites - walipigana na serikali ya India ili kuanzisha jamii ya kikomunisti, vuguvugu hilo lililogharimu maisha ya watu 40,000.
Gereza la Jehanabad lilikuwa na wafungwa wa Maoists pamoja na maadui zao - walinzi kutoka vikosi binafsi vya Wahindu wa tabaka la juu. Makundi yote yalikuwa wakingojea kesi zao za uhalifu. Kama magereza mengi ya India, baadhi ya wafungwa walikuwa na simu za mkononi, kwa kuwahonga walinzi.
Usiku wa tarehe 13 Novemba 2005, wafungwa 389, wakiwemo waasi, walitoroka kutoka gereza la Jehanabad – tukio kubwa zaidi la wafungwa kutoroka nchini India. Takriban watu wawili waliuawa katika ufyatulianaji risasi gerezani, na bunduki za polisi ziliporwa katikati ya machafuko hayo.
Ripoti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ya mwaka 2005 kuhusu ugaidi ilisema waasi hao "waliwateka nyara wafungwa 30" ambao walikuwa wanachama wa kundi linalopinga Maoist.
Tukio lilivyopangwa

Chanzo cha picha, AFP
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Katika hali ya kushangaza, polisi walisema "mpangaji" wa tuki hilo alikuwa ni Ajay Kanu, kiongozi wa waasi aliyekuwa miongoni mwa wafungwa. Polisi wanadai Kanu alikuwa akiwasiliana na kundi lake lililopigwa marufuku - kupitia simu na ujumbe mfupi, akiwasaidia kuingia.
Lakini Kanu anasema hilo si kweli. Mamia ya waasi waliovalia sare za polisi walivuka mto uliokauka nyuma ya gereza, wakapanda na kushuka kuta ndefu kwa kutumia ngazi za mianzi na kuingia ndani, wakafyatua risasi.
Seli zilikuwa wazi kwani chakula kilikuwa kikipikwa jikoni. Waasi hao walitembea hadi kwenye milango mikubwa na kuifunga. Walinzi waliokuwa zamu walitazama bila kufanya chochote. 30 tu kati ya waliotoroka walikuwa wafungwa, wengine walikuwa wakingojea kesi zao - walitoroka kupitia geti kuu, na kutokomea gizani. Yote hayo yalifanyika chini ya saa moja, walioshuhudia walisema.
Kutoroka kwa wafungwa kulionyesha kuporomoka kwa sheria, kukosekana utulivu huko Bihar na uasi uliozidi wa Maoist katika mojawapo ya maeneo maskini zaidi ya India. Waasi walifanya tukio hilo wakati ambao usalama ulikuwa mdogo kutokana na uchaguzi wa majimbo uliokuwa ukiendelea.
Waasi barabarani

Chanzo cha picha, Prashant Ravi
Rajkumar Singh, mwandishi wa habari wa eneo hilo, baada ya kupigiwa simu, aliendesha pikipiki yake katika mji uliohamwa, akijaribu kufika ofisini kwake.
Anakumbuka hewa ilikuwa nzito na milio ya risasi ikilia kwa mbali. Waasi hao pia walikuwa wakijaribu kushambulia kituo jirani cha polisi.
Alipoingia kwenye barabara kuu, mwanga hafifu wa barabarani ulionyesha makumi ya wanaume na wanawake wenye silaha waliovalia sare za polisi wakiwa wamefunga njia, wakipiga kelele kupitia spika.
"Sisi ni Maoist," walisema. "Hatupigani na watu, tunapigana tu na serikali. Kuvamia jela ni sehemu ya upinzania wetu.’
Waasi hao walikuwa wametega mabomu kando ya barabara. Baadhi yalikuwa tayari wakilipuka, wakiporomosha maduka ya karibu na kueneza hofu katika mji huo.
Singh anasema alipambana kufika ofisini kwake ghorofa ya nne, ambapo alipokea simu ya pili kutoka kwa mfungwa huyo huyo.
"Kila mtu anatoroka. Nifanye nini?” aliuliza mfungwa.
"Ikiwa kila mtu atatoroka, unapaswa kutoroka pia," alisema Singh.
Kisha akaelekea gerezani kupitia mitaa mitupu. Alipofika alikuta milango iko wazi. Mchele umetapakaa jikoni, milango ya seli ilikuwa wazi. Hakukuwa na askari jela wala polisi.
Katika chumba kimoja, polisi wawili waliojeruhiwa walikuwa sakafuni. Singh anasema pia aliona mwili wa mfungwa Bade Sharma ukiwa umetapakaa damu. Huyu ni kiongozi wa manamgambo wa makabaila walioitwa Ranvir Sena, ukiwa umelala sakafuni. Polisi baadaye walisema waasi walimpiga risasi wakati wakiondoka.
Sakafuni pia kulikuwa na vijitabu vilivyoganda vilivyoandikwa kwa mkono vikiwa na damu.
“Tunataka kuionya serikali ya jimbo na serikali kuu kwamba ikiwa watawakamata wanamapinduzi na watu masikini na kuwaweka jela, basi tunajua jinsi ya kuwakomboa kutoka jela kwa njia ya mapinduzi ya Ki-Marx," kijitabu kimoja kilisema.
Uso kwa uso na Kanu

Chanzo cha picha, Swastik Pal
Miezi michache iliyopita, nilikutana na Kanu, kiongozi wa waasi mwenye umri wa miaka 57 ambaye polisi wanamtuhumu kupanga na kutorosha wafungwa huko Bihar.
Miezi kumi na tano baadaye, Februari 2007, Kanu alikamatwa katika kituo cha treni alipokuwa akisafiri kutoka Dhanbad, Bihar kuelekea jiji la Kolkata.
Takriban miongo miwili baadaye, Kanu alifutiwa kesi zote isipokuwa sita kati ya 45 za awali za jinai dhidi yake. Kesi nyingi zinatokana na kuvamia jela, pamoja na ile ya mauaji ya Sharma. Ametumikia kifungo cha miaka saba jela kwa mojawapo ya kesi hizo.
Akiwa mtoto, Kanu alitumia mchana na usiku kusikiliza hadithi kutoka kwa baba yake, mkulima wa tabaka la chini kuhusu uasi wa Kikomunisti nchini Urusi, China na Indonesia. Kufikia darasa la nane, marafiki wa babake walikuwa wakimhimiza kukumbatia siasa za kimapinduzi.
Katika tukio la kushangaza baada ya kufunga bao dhidi ya mtoto wa mwenye nyumba katika mechi ya soka, watu wa tabaka la juu wenye silaha walivamia nyumba yao.
“Nilijifungia ndani,” anasema. "Walikuja kwa ajili yangu na dada yangu, wakapora nyumbani na kuharibu kila kitu. Hivyo ndivyo watu wa tabaka la juu walivyotufanya tuwe na hofu."
Alipokuwa akisoma sayansi ya siasa Chuoni, Kanu aliongoza wanafunzi wa Chama cha Kihindu cha Bharatiya Janata (BJP), ambacho kilianzisha vita dhidi ya Maoism. Baada ya kuhitimu, alianzisha shule, lakini alifukuzwa kwenye jengo na mmiliki wa jengo.
Aliporudi kijijini kwake, mvutano na mwenye nyumba ulizuka. Siku mwenye nyumba alipouawa, Kanu, mwenye umri wa miaka 23 tu, alitajwa kwenye malalamiko ya polisi - na akaenda kujificha.

Chanzo cha picha, AFP
"Tangu wakati huo nimekuwa nikikimbia. Niliondoka na nilijiunga Mao na kuwa mfuasi wa siri," anasema. Alijiunga na Chama cha Kikomunisti cha India (Marxist-Leninist), chama cha kikomunisti chenye msimamo mkali.
"Taaluma yangu ni ukombozi - ukombozi wa watu maskini. Kusimama dhidi ya ukatili wa tabaka la juu. Nilipigana kwa ajili ya wale waliovumilia ukosefu wa haki na uonevu.”
Mwezi Agosti 2002, akiwa na sifa ya kuogopwa kama kiongozi wa waasi na zawadi nono ya dola za kimarekani 36,000, ikiwa imetolewa kwa atakaye toa taarifa za kupatikana kwake.
Kanu akiwa njiani kukutana na viongozi ili kupanga mikakati mipya, akiwa karibu kufika Patna, kwenye makutano ya barabara yenye shughuli nyingi, gari lake lilizuiwa. “Kisha wanaume waliovalia kiraia walitoka nje, wakiwa na bunduki, wakiniamuru nijisalimishe. Sikupinga.
Katika kipindi cha miaka mitatu iliyofuata, Kanu alikuwa katika magereza huku polisi wakihofia atatoroka. Kanu anasema aliunda vyama vya wafungwa kupinga ufisadi, huduma duni za afya na hongo. Katika gereza moja, aliongoza mgomo wa kutokula kwa siku tatu, kudai hali bora zaidi ya maisha.
“Hakukuwa na mahali pa kulala. Katika kambi yangu ya kwanza, wafungwa 180 walisongamana katika nafasi iliyokusudiwa watu 40 tu. Tulibuni mfumo wa kuishi. Hamsini kati yetu tungelala kwa saa nne huku wengine wakikaa, wakingoja na kuzungumza gizani. Saa nne zilipotimia, kundi lingine lingechukua zamu yao. Ndivyo tulivyostahimili maisha ndani ya kuta hizo."
Kutoroka 2005

Chanzo cha picha, Prashant Ravi
“Tulikuwa tukingoja chakula cha jioni wakati milio ya risasi ilipolia. Mabomu, risasi – yalikuwa ni machafuko," anakumbuka. "Maoists waliingia ndani, wakipiga kelele ili tukimbie. Kila mtu alikimbilia gizani. Je, ningebaki nyuma na kuuawa?"
Wengi wanatilia shaka usahili wa madai ya Kanu. Afisa wa polisi anasema. "Kwa nini chakula cha jioni kilitayarishwa usiku wakati kwa kawaida kilipikwa na kuliwa jioni, huku seli zikifungwa mapema? Hilo pekee liliibua shaka juu ya njama ya ndani."
Baadhi ya wafungwa wengi waliotoroka walirudi gerezani katikati ya Desemba - wengine kwa hiari, wengine sio kwa hiari. Hata hivyo, hakuna hata mmoja wa waasi aliyerudi.
Nilipomuuliza Kanu ikiwa alipanga kutoroka, alitabasamu. "Maoists walituweka huru - kazi yao ni kukomboa," anasema.
Lakini Afisa wa polisi aliwahi kumuuliza kama anapanga kutoroka tena sasa. Akajibu, "Bwana, mwizi hukwambia ataiba nini?" Kanu alijibu kwa jazba.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












