Vijue vita vya muda mfupi zaidi duniani vilivyopiganwa Zanzibar

rfv

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Ikulu ya Sultani wa Zanzibar
    • Author, Walid Badran
    • Nafasi, BBC Arabic
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Kisiwa cha Zanzibar kipo katikati ya Bahari ya Hindi, ni eneo la kilomita za mraba 2,500, na ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini kina utawala wake wa ndani.

Historia ya Zanzibar imechangiwa kwa kiasi kikubwa na jiografia yake, na upepo wa bahari wa kusi na kaskazi, uliokuwa ukivuma katika eneo hilo, uliiweka Zanzibar kwenye njia za biashara za Bahari ya Hindi na kuifanya kuwa kivutio cha wafanyabiashara na walowezi kutoka Bara Arabu, Asia Kusini na Bara la Afrika.

The Encyclopædia Britannica inasema wahamiaji wa kwanza katika kisiwa hicho walikuwa Waafrika, kisha wakaja Waajemi, ambao waliwasili Zanzibar katika karne ya kumi.

Waarabu walikuwa na ushawishi mkubwa Zanzibar, kwa sababu ya biashara kupitia bahari, na Waarabu kutoka Oman walianzisha biashara na kumiliki ardhi Zanzibar, na hatimaye kuwa ushawishi katika kisiwa hicho.

Kisha Wareno wakaja katika karne ya 16 na kuteka bandari zote za pwani ya Afrika Mashariki, ikiwemo Mombasa, pamoja na visiwa vya Zanzibar na sehemu za pwani ya Arabuni, ukiwemo mji mkuu wa Oman, Muscat.

Hata hivyo, lengo la Wareno kwa sehemu kubwa lilikuwa la kibiashara badala ya la kisiasa, na mamlaka yao ilipoanguka karne ya 17, waliacha athari chache za uwepo wao, kulingana na Encyclopædia Britannica.

Pia unaweza kusoma

Dola ya Oman

dx

Chanzo cha picha, PINTEREST

Maelezo ya picha, Said bin Sultan alipata tena udhibiti wa Zanzibar

Waomani waliwafukuza Wareno kutoka Muscat mwaka 1650, na kutuma meli kushambulia vituo vya Ureno kwenye pwani ya India na Afrika. Waomani walianza kuunda meli zao kubwa za kijeshi, wakitegemea meli za Ureno ambazo walizidhibiti.

Jeshi la wanamaji la Oman lilifanikiwa kuwatimua Wareno katika mwambao wa Afrika Mashariki, isipokuwa Msumbiji, na Waoman wakaidhibiti Mombasa nchini Kenya mwaka 1661 na Zanzibar ikawa chini ya udhibiti kamili wa Oman mwaka 1696.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Womani pia walivishambulia vikosi vya Ureno huko Mumbai nchini India mwaka 1661 na 1662, na kusababisha uharibifu mkubwa kwa meli za Ureno.

Hivyo ndivyo Dola la Oman lilivyoundwa. Lakini vita vya wenyewe kwa wenyewe viliiharibu dola hiyo kutokana na mabishano juu ya nani atakuwa mrithi, yaani Imamu kama kiongozi mkuu.

Mwanzoni mwa karne ya kumi na nane, Oman ikaanguka kuwa mateka kutokana na uvamizi wa Waajemi 1737. Hadi pale Ahmed bin Said, mtawala wa Sohar, mwaka 1744 alipofanikiwa kuwafukuza Waajemi na kuanzisha nasaba ya Al Bou Said ambayo bado inatawala Oman hadi leo.

Al-Mazrui, gavana wa Oman huko Afrika Mashariki, alichukua fursa ya Imam Ahmed bin Saeed akipigana na Waajemi, na kuchukua udhibiti wa Mombasa na maeneo mengine, ikiwa ni pamoja na Zanzibar, na akajizuia kulipa kodi iliyowekwa.

Chini ya utawala wa Said bin Sultan, mjukuu wa Ahmed bin Said, Oman ilipata tena udhibiti wa Zanzibar mwaka 1828, na kuwa ni Sultani wa Oman na Zanzibar, na alihamishia mji wake mkuu kuwa Zanzibar mwaka 1832.

Uingereza na Ufalme wa Zanzibar

f

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Sultan Ali bin Said alipinga maagizo ya Waingereza

Kupanuka kwa biashara ya utumwa mwishoni mwa karne ya 18 na mwanzoni mwa karne ya 19, kutokana na mahitaji ya wafanyakazi wa mashambani huko Amerika Kaskazini na Kusini, kuliifanya Zanzibar kuwa kitovu cha njia za biashara ya watumwa na pembe za ndovu.

Zanzibar yenyewe ilikuwa na rasilimali kubwa ya nazi, karafuu, na vyakula.

Hata hivyo, baada ya kifo cha Said mwaka 1856, wanawe wawili, Majid na Thuwaini, walipigana juu ya urithi wa kiti hicho, na kusababisha ufalme huo kugawanywa kuwa milki mbili; sehemu ya Asia chini ya utawala wa Thuwaini bin Said. Na sehemu ya Afrika, yaani, Zanzibar, ambayo ilikuwa chini ya mamlaka ya Majid bin Said.

Mwishoni mwa karne ya kumi na tisa, Uingereza ilipanua ushawishi wake na kuijumuisha Afrika Mashariki, na hasa Zanzibar.

Mrithi wa Sultan Majid bin Said, aitwaye Barghash bin Said (aliyetawala kutoka 1870 hadi 1888), alilazimishwa na Wazungu kuigawanya ardhi kati ya Waingereza na Wajerumani.

Ilipofika mwaka 1890, Uingereza iliushawishi utawala wa Kisultani kuachana na ardhi yake huko Bara (Tanganyika) na kuiachia Ujerumani, na kuutangaza Usultani wa Zanzibar kuwa chini ya ulinzi wa Uingereza, na ulinzi huo uliodumu kwa zaidi ya miaka 70.

Zanzibar ilipokuwa chini ya ulinzi wa Uingereza, Uingereza iliweka malengo makuu mawili; kukomesha utumwa na kuirejesha Zanzibar katika uchumi wa kibiashara.

Sera ya kiuchumi ya Balozi Jenerali Gerald Portal iliwakasirisha wafanyabiashara wa Kizanzibari, na Sultan Ali bin Said alipinga maagizo ya Uingereza hadi kifo chake mwaka 1893. Wakati ulipofika wa kumchagua mrithi wake, Uingereza ilitaka Sultani ajaye awe chini ya mamlaka na maagizo yake zaidi.

Waingereza walimuunga mkono Hamad bin Thuwein, lakini Mwanamfalme Khalid bin Barghash alikaidi hili na akaikalia kwa nguvu kasri ya Usultani kwa sababu alikuwa mtoto wa pekee wa marehemu Barghash.

Mamlaka za Uingereza ziliweza kumshawishi Khalid kuachia ngazi, na kumfanya Hamad bin Thuwein kuwa Sultani.

Hamad bin Thawein alipofariki dunia, mzozo mwingine kuhusu kiti cha ufalme ukazuka. Mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Uingereza, Arthur Harding, akitaka Hamoud bin Muhammad kushika kiti cha ufalme, akiamini kuwa angekuwa sultani mwenye kushawishika na hatapinga mpango wa Waingereza wa kutaka kukomesha utumwa.

Lakini Khalid alijitangaza kuwa ni Sultani wa Zanzibar na kudhibiti mamlaka.

Vita vya muda mfupi zaidi duniani

d

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Sultan Barghash akutana na maafisa kutoka Jeshi la Wanamaji la Uingereza

Tofauti na jaribio lake la kwanza la kunyakua kiti, wakati huu Khalid alilizunguka kasri akiwa na askari wapatao 3,000 na wafuasi wake, wakiwa na mizinga na boti ndogo ya kivita.

Katika kukabiliana na hali hiyo, mkuu wa Harding aitwaye, Basil Cave, alikusanya kikosi cha watu 400 Wazanzibari watiifu na kikosi cha wanamaji wa Uingereza, na inakadiriwa ukubwa wa kikosi hicho kilikuwa ni watu 900, pamoja na meli 5 za Jeshi la Wanamaji la Uingereza.

Admirali wa Uingereza Harry Rawson alituma makataa kwa kwa Khalid, na kumpa hadi asubuhi ya Agosti 27, 1896, aondoke kwenye kasri na kujisalimisha yeye na majeshi yake, lakini Khalid alikataa, akiamini Waingereza hawatotekeleza shambulio.

Baada ya muda huo kuisha, Rawson aliamuru meli za kivita HMS Rocon, HMS Philomel, Thrush, Sparrow, na St. George kufyatua makombora kwenye jumba hilo, ambalo lilishika moto haraka.

Baada ya dakika 40, Waingereza waliacha kufyatua makombora baada ya shambulio hilo kuwaua na kuwajeruhi wanajeshi 500 wa Khalid bin Barghash, huku mwanajeshi mmoja tu wa Uingereza akijeruhiwa vibaya.

Askari wa miguu wa Waingereza na Wazanzibari waliokuwa watiifu kwao walichukua udhibiti wa kisiwa hicho, huku vikosi vya Sultan Khalid bin Barghash, vilivyokimbia kasri na kukimbilia katika ubalozi mdogo wa Ujerumani, vikijisalimisha.

Kufikia alasiri ya siku hiyo hiyo, Hamoud bin Muhammad aliteuliwa kuwa Sultani wa Zanzibar. Sultan Hamoud alikubali mara moja masharti yote ya Uingereza, na akakubali matakwa ya Waingereza ya kukomesha utumwa.

Wajerumani walimruhusu Khalid bin Barghash kuishi uhamishoni huko Dar es Salaam, ambako alibakia hadi Waingereza walipomkamata wakati wa Vita Vikuu vya Kwanza ya Dunia. Khalid alifariki Mombasa mwaka 1927.

Hakuna uasi mwingine uliotokea kwenye kisiwa cha Zanzibar, hadi Uingereza ilipoondoka mwaka 1963.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa ana Ambia Hirsi