Jamshid bin Abdullah Al Said: Sultani wa mwisho wa Zanzibar afariki dunia

Chanzo cha picha, Getty Images
Jamshid bin Abdullah, Sultani wa mwisho kuitawala Zanzibar na aliyeondolewa mamlakani kwa mapinduzi ya Januari 1964 amefariki dunia.
Jamshid amefariki hospitalini nchini Oman Jumatatu, Disemba 30 akiwa na umri wa miaka 95.
Taarifa za kifo chake zimeripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari nchini Oman. Sababu za kifo zinaelezwa kuwa ni maradhi ya muda mrefu na uzee. Anatarajiwa kuzikwa Jumanne katika makaburi ya kifalme jijini Muscat, Oman.
Jamshid ameishi wapi baada ya kupinduliwa?

Chanzo cha picha, Getty Images
Jamshid alichukua madaraka ya Usultani mnamo Julai mosi mwaka 1963. Miezi mitano baada ya kutawazwa kuwa Sultani Zanzibar ilipata uhuru wake kutoka kwa Waingereza mnamo Disemba 1963.
Hata hivyo, uhuru huo haukubaliwa na wote visiwani Zanzibar, na kusababisha mapinduzi ya Januari 12, 1964 ambayo yalitamatisha utawala wa Jamshid ambaye alikaa madarakani kwa miezi sita tu.
Baada ya kupinduliwa kwa serikali ya kisultani, Jamshid alikimbilia uhamishoni, awali nchini Oman ambapo hakupewa hifadhi na hatimaye alielekea nchini Uingereza.

Chanzo cha picha, Getty Images
Jamshid aliishi uhamishoni nchini Uingereza katika jiji la pwani ya kusini la Portsmouth kwa miaka 56. Gazeti la The Guardian la Uingereza linaripoti kuwa Jamshid alikataliwa mara kadhaa maombi yake ya kutaka kuishi nchini Oman japo watu wa familia yake waliruhusiwa kuishi nchini humo toka miaka ya 1980.
Aliruhusiwa mwaka 2020 na serikali ya Oman kurejea katika nchi hiyo ya asili ya familia yake.
Kwa kipindi chote alichoishi Uingereza inaripotiwa kuwa Jamshid aliishi kwa ukimya na hata baadhi ya jirani zake hawakujua yeye ni nani.
Mwandishi Ned Donovan, aliyekuwa akifuatilia maisha ya sultani huyo uhamishoni alisema: "Sikupata mkaazi hata mmoja ambaye alifahamu uwepo wake, hakuzungumza na vyombo vya habari, aliishi maisha ya kunyamaza sana."
Rais wa zamani wa Zanzibar (1990-2000) Dkt Salmin Amour alimruhusu Jamshid kurejea Zanzibar kama raia wa kawaida lakini hakufanya hivyo.
Maisha yake kabla ya usulatani

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Jamshid alizaliwa visiwani Zanzibar mnamo Septemba 16, 1929 na kupata elimu yake ya msingi visiwani humo na baadaye aliendelea na masomo nchini Misri na hatimaye Uingereza ambako baada ya msomo alihudumu katika jeshi la wanamaji la nchi hiyo kwa takriban miaka miwili.
Alirejea Zanzibar katika miaka ya mwisho ya utawala wa babu yake Sultani Sayyid Khalifa. Baba yake Jamshid, Sultan Abdullah bin Khalifa alitawala kutoka Oktoba 1960 mpaka Julai 1963 alipofariki na kiti chake kurithiwa na Jamshid.
Jamshid alikuwa Sultani wa mwisho kuitawala Zanzibar na kabla yake walitawala masultani wengine 12. Sultani wa mwanzo akiwa Sayyid Said, ambaye alihamisha makao makuu yake kutoka Muscat Oman hadi Zanzibar mwaka 1840. Sayyid Said alikuwa Sultani wa Oman na Zanzibar kwa wakati mmoja.
Baada ya kufariki kwa Sayyid Said mwaka 1856, kukatokea ugomvi wa madaraka baina ya wototo wake wawili Majid na Thuwain. Chini ya makubaliano yaliyosimamiwa na Waingereza, wakaigawa dola ya baba yao katikia nchi mbili.
Majid akawa Sultani wa Zanzibar na Thuwain akawa Sultani wa Oman.
Japo utawala wa familia hiyo ya Busaidi ulikomeshwa visiwani Zanzibar Januari 1964 kwa kupinduliwa kwa Jamshid, nchini Oman bado familia hiyo inaendelea kutawala.
Moja ya masharti aliyopewa Jamshid aliporejea nchini Oman mwaka 2020 ni kuwa arejee kama mwanafamilia ya kifalme lakini si kama Sultani.












