Msichana wa miaka 22 alivyouawa baada ya kubakwa akihudhuria kipindi cha dini

Muda wa kusoma: Dakika 5

Tahadhari: Maelezo katika makala haya yanasikitisha

Msichana mwenye umri wa miaka 22 alidaiwa kubakwa, kuuawa na mwili wake ukiwa mtupu kutupwa kwenye shimo la maji huko Ayodhya, mji ulioko kaskazini mwa jimbo la Uttar Pradesh nchini India.

Watu watatu wamekamatwa kufuatia mzozo wa kisiasa ulioibuka ukihusishwa na suala hilo.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya India, watu watatu waliokamatwa ni wa Ayodhya.

Afisa Mwandamizi wa Polisi wa Ayodhya (SSP) Raj Kiran Nair aliambia vyombo vya habari kwamba washtakiwa walikamatwa kwa kuzingatia upelelezi na uchunguzi wa kielektroniki.

SSP Rajkaran alidai kuwa washitakiwa wamekiri kutenda kosa hilo, na baada ya hapo "polisi wamepata nguo za binti huyo na koti lililochomwa na mmoja wa washtakiwa, alilokuwa amevaa wakati akitenda kosa hilo."

Ripoti ya awali ya uchunguzi wa maiti ya msichana aliyeuawa ilisema kwamba alikufa kutokana na kuvuja damu nyingi na mshtuko.

Kwa mujibu wa familia ya binti huyo, mwili wake ulikuwa na "alama za majeraha, macho yake yalikuwa yametoka nje, na viungo vyake vya mwili vilivunjika, huku mwili ukiwa umefungwa kwa kamba na kutupwa kwenye mfereji wa maji."

Tukio hilo lilitokea katika Barabara ya Ambedkar Nagar karibu na mji wa Ayodhya.

Msichana huyo mwenye umri wa miaka 22 alitoweka tangu Alhamisi iliyopita jioni.

Kwa mujibu wa familia hiyo, walimtafuta kila mahali msichana huyo baada ya kutoweka lakini hakupatikana.

Afisa wa Polisi wa Ayodhya Ashish Mishra alisema, "Mwili wa msichana huyo uliokatwakatwa ulipatikana kwenye shimo la maji asubuhi ya Februari 1 (Jumamosi)."

Siku ya Jumamosi, polisi walisajili ripoti ya mtu kutoweka baada ya kupokea taarifa kutoka kwa familia yake.

Wakati wanakijiji walipokuwa wakipeleka mwili wa msichana nyumbani, iligundulika kuwa mguu wake pia ulikuwa umevunjika. Kwa mujibu wa familia hiyo, "hali ya mwili ilikuwa mbaya kiasi kwamba dada mkubwa wa msichana huyo na wanawake wengine wawili walipoteza fahamu walipouona.

Familia inawalaumu polisi kwa uzembe

Kwa mujibu wa taarifa ya familia, msichana huyo mwenye umri wa miaka 22 alikuwa ameenda kusikiliza 'Bhagwat Gita' kwenye kipindi cha kidini saa 10 jioni mnamo Januari 30. Dadake mkubwa alisema, "Alipochelewa kurudi baada ya muda mrefu, wasiwasi ulianza kuongezeka."

"Tulimtafuta kila mahali lakini hakupatikana. Kisha tukaandikisha ripoti ya kupotea siku ya Ijumaa.

Unaweza pia kusoma

Je, vyama vya upinzani na BJP vimechukua hatua gani?

Viongozi wa upinzani wamekemea vikali tukio hilo na kuhoji hali ya sheria na utulivu katika jimbo hilo. Kiongozi wa BJP alisema kuwa tukio hili ni baya na la kusikitisha na kutaka familia itendewe haki.

Video ya Mbunge wa Ayodhya Awdesh Prasad kuhusu tukio hili inasambaa kwenye mitandao ya kijamii. Katika video hii anaonekana akilia huku akielezea hisia zake kuhusu tukio hili. Alisema hilo ni tukio la kinyama na iwapo haki haitatendeka atajiuzulu wadhifa wake.

Akihutubia mkutano na waandishi wa habari, Udhesh Prasad alisema: "Niruhusu niende Delhi Lok Sabha. Suala hili nitaeleza mbele ya Waziri Mkuu. Tusipopata haki nitajiuzulu wadhifa huo.

Wakati huo huo, wafanyakazi wenzake Awdesh Prasad walijaribu kumfariji na kueleza nia yao ya kufanya kila wawezalo kuleta haki kwa familia ya marehemu.

Kiongozi wa Congress na Kiongozi wa Upinzani Bungeni Rahul Gandhi ameelezea tukio hilo kupitia akaunti yake ya X.

"Msichana wa Dalit aliteswa kikatili na kuuawa huko Ayodhya. Tukio hili ni la aibu na la kuhuzunisha sana," alisema.

Rahul Gandhi ameshutumu utawala kwa kutozingatia suala hilo kwa wakati. Aliandika, "Kama utawala ungezingatia kwa wakati, maisha ya msichana huyo yangeokolewa.

Wametaka uchunguzi wa haraka kuhusu suala hilo kutoka kwa serikali ya Uttar Pradesh na wametaka adhabu kali kwa wahusika na hatua kali dhidi ya polisi waliozembea.

Kiongozi wa Congress Priyanka Gandhi pia amejibu tukio hilo kupitia akaunti yake ya X.

Alisema, "Msichana wa Dalit ambaye alikuwa amekwenda Ayodhya kusikiliza mawaidha ya kidini aliuawa kwa njia isiyo ya kibinadamu na ya kikatili. Tukio hili ni la kuhuzunisha na la aibu kwa ubinadamu. Msichana aliyeuawa alikuwa amepotea kwa siku tatu lakini polisi walizembea kumtafuta.

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jimbo na mkuu wa BSP Mayawati alisema kwamba serikali inapaswa kuchukua hatua kali kuzuia matukio kama haya kutokea tena.

Kiongozi wa Chama cha Samajwadi na Waziri Mkuu wa zamani wa jimbo la Uttar Pradesh Akhilesh Yadav amedai kuwa ukatili dhidi ya jamii za watu walio wachache, Dalit unaongezeka nchini India.

Waziri wa Kazi na Ajira wa Uttar Pradesh Manohar Lal alitembelea Ayodhya na kukutana na familia iliyoathiriwa na kuwahakikishia haki.

"Tukio hili lilikuwa gumu na lisilopendeza, Waziri Mkuu analifahamu suala hilo na ametoa maelekezo ya wazi ya kumkamata mhalifu haraka iwezekanavyo na kumchukulia hatua kali," alisema.

Lakini wakati akihutubia mkutano, Waziri Mkuu wa Jimbo na kiongozi wa BJP Yogi Adityanath aliita machozi ya Udhesh Kumar kuwa mchezo wa kuigiza, akimlenga Akhilesh Yadav na kusema kwamba wale waliokamatwa watajiunga na Chama cha Samajwadi.

Lakini SSP Raj Kiran Nair amesema kuwa polisi hawajapata ushahidi kwamba washukiwa watatu waliokamatwa wanahusishwa na chama chochote.

Kwa upande mwingine, mjumbe wa Tume ya Wanawake ya Uttar Pradesh Priyanka Maurya alisema kwamba tukio la kinyama na la kikatili limetokea kwa msichana huyo. Kila juhudi itafanywa kuhakikisha kuwa familia inapata haki haraka iwezekanavyo. Pia alisema kuwa uongozi wa polisi unasaidia familia na uchunguzi unafanywa.

Tukio hilo linakosolewa vikali kwenye mitandao ya kijamii, huku wasiwasi ukionyeshwa kuhusu hali ya sheria na utulivu katika jimbo hilo, wakiita 'jungle raj'.

Mtu mmoja aliyefahamika kama Tanmay aliandika kuhusu tukio hilo, "Kuna sheria huko Uttar Pradesh. Leo, ukatili unafanywa dhidi ya Dalits huko akihusisha Serikali ya BJP na mfumo wao wote unahusika katika hili.