Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Inawezekana kuwa na katiba mpya kabla ya Uchaguzi Mkuu Tanzania?
- Author, Na Rashid Abdallah
- Nafasi, Mchambuzi Tanzania
Mwanzoni mwa mwezi Januari 2023, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alitoa tangazo rasmi la kuruhusu mikutano ya hadhara ya kisiasa. Kufuatia katazo lililodumu kwa takribani miaka saba, tangu wakati wa hayati John Pombe Magufuli.
Ruhusa hiyo imezileta siasa za Tanzania katika viriri badala ya mitandao ya kijamii. Takribani kila wiki kuna mikutano ya hadhara hasa vyama vya upinzani, kile kikuu cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na ACT Wazalendo.
Vyama vyote vinajadili sera zao, vinakosoa serikali, vinaahidi hiki na kile ikiwa vitangia madarakani, sambamba na kusaka wanachama wapya. Fauka ya hilo, vinadai katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025. Imekuwa ni ajenda kuu katika majukwaa ya siasa za Tanzania.
Shinikizo la Upinzani
Wito wa kupatikana katiba mpya kabla uchaguzi mkuu ulianza kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020. Wito huo haukufanikiwa kushawishi serikali ya wakati huo. Sehemu ya waraka wa maaskofu wa Kanisa la Kiinjili na Kilutheri Tanzania (KKKT) uliotolewa Machi 2018, unaeleza:
“Tunawashauri raia wema, kwa njia za kidemokrasia kupitia majukwaa ya kikatiba yaliyo katika maeneo yao, kudai upatikanaji wa katiba mpya. Itapendeza katiba mpya ikipatikana kabla uchaguzi mkuu ujao (2020).”
Vuguvugu bado linaendelea. Chadema imezindua ‘operesheni +255 Katiba mpya,’ yenye lengo la kushinikiza upatikanaji wa katiba mpya kabla ya chaguzi zijazo za 2024 na 2025. Makamu mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu ni miongoni mwa wanasiasa wanaokoleza shinikizo hilo.
Mei 27, 2023 akihutubia maelfu ya wakazi wa mkoa wa Tabora katika viwanja vya Town School, alieleza, “tunahitaji kupambana na kulianzisha nchi nzima, tumkabili Rais Samia, tumwambie bila Katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu hakitaeleweka.”
Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Juma Duni Haji amenukuliwa na vyombo vya habari mwezi Machi mwaka huu akisema, “mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya unapaswa kukamilika kabla ya uchaguzi mkuu wa 2025, ili wananchi waongozwe na watu waliowachagua kwa ridhaa zao.”
Shinikizo la sasa kutoka upinzani limezidi kupata nguvu tangu Rais Samia kueleza azma ya kufufua mchakato huo. Ingawa mchakato wenyewe haujapangiwa siku wala tarehe ya kuanza. Pia, haijaelezwa mchakato huo utaanzia kwenye hatua ipi.
Muda na wapi mchakato utaanza ni vitendawili. Uanze kabla rasimu haijapelekwa katika Bunge Maalum la wakati huo au uanze na rasimu iliopitishwa na Bunge ambalo lilisusiwa na upinzani! Huo ni mjadala wa baadaye.
Katiba ni hoja ya muda mrefu
Mchakato wa kutafuta katiba mpya ulianza wakati wa rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete. Ingawa wito wa kuundwa katiba mpya upo muda mrefu, wakati hayati Rais wa kwanza Julius Kambarage Nyerere yu hai, walikuwepo watu wakidai katiba mpya.
Mwaka 1992 Tanzania ikielekea kufanya maamuzi ya kuondokana na mfumo wa chama kimoja. Hapakuwa na mchakato wa kuunda katiba mpya, bali kulikuwa na mchakato wa kufuta ibara zilizokipa Chama cha Mapinduzi (CCM) haki pekee ya kuendesha siasa. Pia, palirekebishwa vipengele ili kuruhusu mfumo wa vyama vingi.
Mavuguvugu yanayoibuka kudai katiba mpya, msingi wa hoja zao mara nyingi umegawika katika kuu sehemu mbili. Mosi, katiba ya sasa ni ya zamani tangu wakati wa chama kimoja, hivyo haitendi haki kwa vyama vya upinzani hasa uhuru wa kisiasa, maswala ya haki na mwenendo wa chaguzi.
Pili, kuna wale wanaotaka katiba mpya ili kuleta mabadiliko katika muundo wa muungano. Kundi hili mara nyingi hutokea Zanzibar, ndiko kwenye chimbuko la malalamiko kuhusu kero zinazotokana na muundo wa muungano.
Ikiwa Rais Samia ndiye ataandika historia ya kuwapatia Watanzania katiba mpya – kabla ama baada ya uchaguzi. Atakuwa kaandika historia ya kipekee ambayo watangulizi wake wameshindwa kuifanikisha.
Je, muda unatosha?
Ratiba ya uchaguzi mkuu wa Tanzania ni Oktoba 2025, kwa hesabu za haraka haraka kuna miaka miwili na miezi kadhaa kabla ya uchaguzi huo. Kwa kuupima mchakato huo kwa kuhesabu miezi, bila shaka siku zinaonesha upo uwezekano wa katiba kupatikana kabla ya Oktoba 2025.
Kwa upande mwingine, siasa nazo zina hesabu zake. Wale wenye nguvu na mamlaka ya kuamua juu ya jambo hilo, nao wana hesabu zaidi ya zile za kujumlisha siku na miezi – zinaitwa hesabu za kisiasa. Changamoto ni kuwa, hisabati za kisiasa za Rais Samia na chama chake kuhusu katiba mpya haziko wazi.
Rais Samia amekuwa tofauti kidogo na mtangulizi wake, John Pombe Magufuli ambaye aliweka wazi tangu mwali, katiba siyo kipau mbele cha utawala wake. Rais Samia kwa upande wake ameweka wazi katiba ni ajenda ya utawala wake.
Madai ya vyama vya upinzani yako wazi - katiba mpya ni muhimu kabla ya chaguzi za 2024 na 2025. Wakiamini itakuwa chachu ya kufanyika chaguzi huru na za haki, miongoni mwa mambo mengine. Ila aliyeshikilia saa ya kuanza mchakato huo ni Rais Samia na chama chake.