PAM: Ameba mla-ubongo anavyoua watu duniani

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 2

Hivi karibuni jimbo la Kerala nchini India limegubikwa na hofu baada ya wagonjwa 19 kupoteza maisha kutokana na maambukizi ya kiumbe mdogo anayeitwa Naegleria fowleri, maarufu kama "ameba mla-ubongo".

Tukio hili limeibua mijadala mipana kuhusu ugonjwa adimu unaoitwa Primary Amoebic Meningoencephalitis (PAM), ambao licha ya kuwa nadra, karibu kila anayeambukizwa hufariki.

Wagonjwa waliokufa walikuwa wakiwa na umri wa miezi 3 hadi miaka 92, na tukio hili limeonesha hatari kubwa ya PAM, hasa pale ambapo maji machafu au yasiyo safi yanatumiwa kwa kuogelea au kutumika kusafisha pua.

Si India tu, nchi nyingi zilitoa tahadhari kuhusu ugonjwa huu, ikiwemo Marekani badaa ya kuathiri watu kadhaa.

Unasababishwa na nini na dalili zake

PAM husababishwa na ameba au amoeba mdogo anayeishi majini aitwaye Naegleria fowleri. Kiumbe hiki huishi hasa kwenye maji ya moto au yasiyo safi kama mabwawa, mito, visima, na mabwawa ya kuogelea. Kwa kawaida ni chakula cha bakteria, lakini pale anapoingia mwilini kupitia puani, husafiri hadi kwenye ubongo na kuharibu tishu kwa kasi.

Dalili za mwanzo za ugonjwa huu ni kama za mafua: kichwa kuuma, homa, kichefuchefu, kutapika na shingo kukakamaa.

Mara dalili hizi zinapobadilika, mgonjwa hupata kuchanganyikiwa, wakati mwingine kifafa, kupoteza fahamu na hatimaye kifo.

Mara nyingi, wagonjwa hufariki ndani ya siku 7–10 tangu dalili za mwanzo kuonekana. Kwa kuwa dalili za awali hazionekani tofauti na magonjwa ya kawaida ya mafua, wengi hawafahamu wanaugua PAM hadi pale hali zao zinapobadilika na kuwa mbaya kabisa.

Unaambukizwaje na madhara yake

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maambukizi hutokea pale maji yaliyo na ameba au amoeba yanapoingia puani, kwa mfano wakati wa kuogelea au kuosha pua kwa maji yasiyo safi. Haiambukizi kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine, na kunywa maji yenye amoeba hakuleti maambukizi. Ameba hupitia mishipa ya harufu hadi ubongo na kusababisha uharibifu wa tishu, uvimbe, na shinikizo kubwa ndani ya fuvu.

Madhara yake ni makubwa ikiwemo uvimbe wa ubongo, uharibifu wa mishipa ya fahamu, na kusababisha kifo ndani ya muda mfupi.

Takwimu zinaonyesha kuwa dunia kote, asilimia 95% mpaka 98% ya wagonjwa wa PAM hupoteza maisha. Katika eneo la Kerala, India, mwaka huu tu visa 69 vimeripotiwa na vifo 19, ikionyesha hatari ya ugonjwa huu hata pale ambapo ugonjwa ni adimu. Hali hii imeibua umuhimu wa elimu ya umma na uchunguzi wa mapema duniani kote ili kuongeza nafasi ya kupona.

Tiba

Hadi sasa, PAM haina tiba kamili. Wagonjwa wachache waliopona walipewa mchanganyiko wa dawa za kuua amoeba kama amphotericin B na miltefosine, pamoja na dawa za kupunguza uvimbe (steroids) na matibabu ya kushusha shinikizo la ubongo.

Ufanisi wa matibabu haya ni mdogo kwa sababu ugonjwa unakuwa na kusambaa kwa haraka, na mara nyingi wagonjwa wanapowasili hospitalini, tishu za ubongo tayari zinakuwa zimeharibiwa.

Kwa mujibu wa wataalamu kinga bora ni kuzuia maambukizi ikiwemo kuepuka maji machafu au yasiyo safi kuingia pua, kuhakikisha mabwawa na visima yanasafishwa, na kuelimisha jamii kuhusu hatari ya kuogelea au kutumia maji yasiyo salama. Hatua hizi ndizo pekee zinazoweza kuokoa maisha kutokana na ugonjwa huu hatari.