Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, mgogoro kati ya Israel na Iran unaweza kuathiri vipi Afrika?
Michael Race, Peter Hoskins, Nick Edser na Papa Atou Diaw
BBC News na BBC Africa
Jioni ya Jumamosi Aprili 13, macho yote yalikuwa katika eneo la Mashariki ya Kati. Kwa mara ya kwanza, Iran iliilenga kwa mashambulizi Israel moja kwa moja kwa kurusha ndege zisizo na rubani na makombora.
Makombora ambayo yalilenga taifa hilo la Kiyahudi yalizuiliwa zaidi na mfumo wa ulinzi wa Iron Dome kulingana na mamlaka ya Israeli.
Iran ilisema ilifanya shambulizi hilo kujibu shambulio la anga la Israel kwenye ubalozi mdogo mjini Damascus tarehe 1 Aprili, ambalo lilwaua maafisa wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Shambulio hili ambalo halijawahi kushuhudiwa limesababisha wasiwasi ndani na hata nje ya kanda hiyo hasa barani Afrika.
Je, nini maoni ya viongozi wa nchi za Afrika?
Kufuatia shambulizi la ulipizaji kisasi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, nchi kadhaa za Kiafrika zilitoa maoni yake. Viongozi wa nchi hizo walitoa wito wa kujizuia baada ya shambulio la Iran dhidi ya Israel.
Afrika Kusini, Nigeria, Kenya, Somalia na nchi nyingine kadhaa za Afrika zimeitaka Israel kujizuia wakati baraza lake la mawaziri la vita likikutana ili kuamua iwapo italipiza kisasi dhidi ya shambulio la anga la Iran ambalo halijawahi kushuhudiwa.
Wizara Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano ya Afrika Kusini ilisema katika taarifa yake kuwa: "Afŕika Kusini daima imekuwa ikisisitiza kwamba, hata kama Mataifa yanaamini kuwa matumizi yao ya ni halali, kamwe si jambo la busara kukimbilia vita kwa sababu, bila shaka, ni watu wa kawaida wanaoteseka kutokana na mizozo,” iliongeza wizara.
Rais wa Kenya William Ruto aliitaka Israel "kujizuia kwa kuzingatia hitaji la dharura la pande zote kujiondoa katika mapigano ambayo yanaweza kuwa vigumu sana kumalizika."
Alisema shambulio la Iran "linawakilisha tisho halisi la amani na usalama wa kimataifa."
Somalia ilitoa wito kwa "jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka na madhubuti za kupunguza hali hiyo ya uhasama na kupunguza hatari ya migogoro zaidi."
Wizara ya mambo ya nje ya Nigeria ilizitaka Israel na Iran "kutafakari juu ya kujitolea kwa wote katika utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani."
Iran na Israel kwa pamoja hazijawa na uhusiano wa muda mrefu wa kisiasa na Mataifa ya Kusini mwa Jangwa la Sahaŕa, huku uhusiano wa nchi hizo mbili na nchi za kanda hiyo ukiwa umedhoofika kutokana na mahusiano yake mabaya na nchi za Kiarabu kwa ujumla na hasa kuhusu suala la Palestina.
Ni nini athari ya shambulio la Iran kwa bei ya mafuta?
Bei ya mafuta ilishuka Jumatatu kufuatia shambulio la kulipiza kisasi la Iran dhidi ya Israeli mwishoni mwa juma.
Pipa la Brent, mojawapo ya vigezo kuu vya bei ya mafuta vya kimataifa, lilikuwa la bei ya chini, lakini bado liliuzwa kwa karibu dola 90 kufikia Jumatatu asubuhi.
Bei zilikuwa tayari zimepanda kwa kutarajia hatua kutoka Iran, huku Brent akifikia kiwango cha juu cha miezi sita wiki iliyopita.
Wachambuzi walisema masoko yatakuwa yakiangalia jinsi mzozo huo unavyoweza kuathiri mifumo ya ugavi wa bidhaa hiyo duniani.
Kushuka kwa bei ya mafuta kunaweza kuwa na madhara duniani kote, kwani nchi zinategemea sana malighafi hii, ambayo hutumiwa kuzalisha nishati kama vile petroli na dizeli.
Bei za mafuta na nishati zimekuwa mojawapo ya sababu kuu za kupanda kwa gharama za maisha duniani kote katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Wakati Urusi ilipoivamia Ukraine mwaka wa 2022, bei ya mafuta ilipanda hadi $120 kwa pipa kutokana na hofu ya usambazaji huku nchi za Magharibi zikiiwekea vikwazo Urusi, msafirishaji mkuu wa mafuta duniani.
Kupanda huku hakukusababisha mfumuko mkubwa wa bei ya juu tu ya mafuta lakini pia bidhaa nyingine nyingi, kwani kampuni zilirekebisha bei zao ili kufidia gharama za juu.
Wachambuzi wanasema jibu la Israeli kwa shambulio hilo litakuwa muhimu kwa masoko ya kimataifa katika siku na wiki zijazo.
Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant alisema makabiliano na Iran "bado hayajaisha."
Mwishoni mwa wiki iliyopita, bei ya pipa la Brent ilifikia $92.18, kiwango chake cha juu zaidi tangu Oktoba, lakini ilishuka Jumatatu hadi karibu $89.70.
Wakati bei ya mafuta ilishuka kidogo, bei ya dhahabu ilipanda kidogo, ikikaribia kiwango cha juu cha wakati wote kwa karibu $2,400.
Dhahabu mara nyingi inachukuliwa kuwa uwekezaji salama wakati wa kutokuwa na uhakika na bei yake ilishuhudiwa kupanda kwa kasi kabla ya wikendi.
Je, mgogoro huu unaweza kuathiri Afrika?
Kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya mafuta Mohamed Julien Ndao, katika hali ya sasa ya mambo, mataifa ya Afrika hayapaswi kuwa na hofu kwa sababu masoko ya mafuta tayari yalikuwa yakitarajia jibu kutoka kwa Iran.
"Kama ilivyotarajiwa, bei ilishuka kwa sababu ni taarifa ambazo tayari zilikuwa kwenye bei," anaeleza Bw. Ndao. "Bei zinaendelea kushuka kwa sababu hatutarajii jibu la Israeli linaweza kuhatarisha soko," anaendelea.
Hata hivyo, Mohamed Julien Ndao anasisitiza kuwa Afrika itaathirika moja kwa moja iwapo mzozo huo utadorora au kuenea.
"Tutakuwa na wasiwasi kwanza, hata kama hatuko mstari wa mbele kwenye mapigano kwa sababu sisi ni nchi ambazo zina uwezo wa wastani wa kununua," anasema Bw. Ndao.
“Na iwapo bei ya mafuta itapanda kwa kiwango cha juu kesho kwa sababu ya mzozo huu, kama ilivyokuwa wakat iwa vita kati ya Urusi na Ukraine, utaona kwamba gharama za usafirishaji wa mizigo zitaongeza gharama ya bidhaa kufika hapa.
Ikizingatiwa kwamba tunaagiza bidhaa nyingi zitaongezeka, mafuta ghafi yataongezeka, mafuta ya petroli yataongezeka katika mfumo mzima wa thamani,” anasema Bw. Ndao.
Kwa hivyo anayashauri mataifa ya Afrika kushiriki katika kutafuta suluhu la kidiplomasia ili kuzuia hali kuwa mbaya zaidi.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Yusuf Jumah