Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jinsi Biden alivyotia dosari utawala wake
- Author, Anthony Zurcher
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Katika kuuunadi urithi wake, kupitia mahojiano ya runinga, Biden alisema, "natumai historia itasema niliingia madarakani na mpango wa kurejesha uchumi na kurudisha uongozi wa Marekani ulimwenguni."
"Na natumai historia itaeleza kwamba nilifanya hayo kwa uaminifu na uadilifu; nilisema kile kilichokuwa akilini mwangu."
Lakini Biden anaondoka Ikulu akiwa na 39% tu ya watu wenye mtazamo chanya kuhusu yeye, kulingana na uchunguzi wa hivi karibuni wa Gallup, chini kutoka 57% mwanzoni mwa muhula wake.
Biden alikuwa na mafanikio yake - kuweka sheria za uwekezaji na miundombinu kupitia Bunge la Congress, kuimarisha na kuipanua Nato, na kuteua idadi kubwa ya majaji wenye asili tofauti - lakini hayo kwa sasa yamefunikwa.
"Angependa urithi wake uwe kwamba alituokoa kutoka kwa Trump," anasema mwandishi na mfuasi wa chama cha Democratic, Susan Estrich. "Lakini cha kusikitisha, urithi wake ndio umemleta Trump tena. Yeye ndiye daraja kutoka Trump mmoja hadi Trump wa pili."
Msururu wa matatizo
Makosa ya kwanza mabaya ya Biden kama rais ni katika machafuko yaliyotokea wakati wa kujiondoa kwa jeshi la Marekani, huko Afghanistan Agosti 2021.
Kufikia majira ya joto, mfumuko wa bei nchini Marekani ulikuwa umepita 5% kwa mara ya kwanza katika miaka 30. Na mfumuko huo ukafikia hadi 9.1% Juni 2022.
Ingawa mfumuko wa bei wa kila mwezi ulishuka chini ya 3% kufikia msimu wa joto wa 2024, ukosefu wa ajira ukapungua, ukuaji wa uchumi ukawa imara, lakini bado wapiga kura waliendelea kuwa na mtazamo wa kukata tamaa kuhusu uchumi.
Maswala mengine yakawa ni uhamiaji: Utawala wa Biden ulichelewa kutoa ufumbuzi wa tatizo la uhamiaji katika mpaka wa Mexico baada ya janga la corona. Na athari za usumbufu wa mpango ulioungwa mkono na Republican wa kuwahamisha wahamiaji hadi miji ya kaskazini yenye wafuasi wengi wa Democratic.
Uhaba wa vipimo vya Covid na maziwa ya unga ya watoto wachanga, ongezeko kubwa la bei ya mayai, na vita vya Ukraine na Gaza - kwa kila tatizo ambalo halikutarajiwa ambalo utawala wa Biden ulilishughulikia, matatizo mapya yaliibuka.
'Mzee asiye na kumbukumbu'
Biden - ambaye wakati fulani alichukuliwa kuwa mzungumzaji mwenye kipawa - alionekana kutokuwa na uwezo wa kuwasiliana na watu wa Marekani. Dalili za uzee wake zilionekana.
Ripoti ya Robert Hur, mwanasheria maalum aliyeteuliwa kumchunguza Biden na namna anavyoshughulikia hati za siri, ilimtaja rais huyo kama "mzee asiye na kumbukumbu."
Mwingiliano wa Biden na vyombo vya habari ulipunguzwa, na kuonekana kwake hadharani kulidhibitiwa sana. Makosa yake ya maneno na kujikwaa yakawa lishe ya mashambulizi ya Republican. Lakini Biden aliendelea, akidhamiria kushinda muhula wa pili ofisini.
Katika mwaka wake wa kwanza, mpango wa "American Rescue Plan" wa Biden, ulijumuisha karibu dola trilioni 2 katika matumizi mapya ya serikali. Ulipanua ruzuku za huduma ya afya, na kufadhili usambazaji wa chanjo za Covid na mpango wa malipo ambao ulipunguza umaskini kwa watoto hadi 5%.
Ndani ya mwaka wake wa kwanza, wabunge wa Democratic na baadhi ya Warepublican walijiunga ili kupitisha mswada wa uwekezaji katika miundombinu, ambao ulijumuisha dola trilioni 1 katika matumizi mapya ya usafiri, nishati safi, maji, na programu nyingine za ujenzi.
Cebul anasema: "Hisia za Biden kwamba Marekani ilikuwa inafanya vizuri kiuchumi ilimfanya yeye na washauri wake kuondoa macho yao kwenye mpira wakati Wamarekani wengi walikuwa bado wanaumia sana."
Baada ya miaka miwili, wapinzani wake wa kisiasa walianzisha uchunguzi, wakafanya vikao (kuhusu kujiondoa Afghanistan, shughuli za biashara za familia ya Biden na mengineyo) na, Septemba 2023, walianzisha rasmi uchunguzi wa kumuondoa.
Gaza, Ukraine na Hunter
Katika msimu wa vuli, Biden alikabiliana na mzozo mwingine tena - kufuatia shambulio la Oktoba 7 la Hamas dhidi ya Israel, alionya kwamba Israel isichukue hatua za kulipiza kisasi kupita kiasi.
Uungaji mkono wa Marekani kwa Israel uliondoa uungwaji mkono wa Biden katika baadhi ya maeneo ya nyumbani.
Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, Biden alielekeza nguvu kuunganisha umoja wa Ulaya ili kupambana na uvamizi huo.
Wakati huo huo, Biden alikuwa akikabiliana na matatizo ya kisheria ya mwanawe Hunter katika kesi ya Juni na kuhukumiwa kwa mtoto huyo.
Uamuzi wake wa mwisho wa kumsamehe mwanawe, uliofanywa baada ya uchaguzi wa Novemba, ulilaaniwa na wengi, wakiwemo washirika wake.
Tarehe 25 Aprili, 2023, Biden alitangaza azma yake kuwania urais akionya kwamba Trump ana msimamo mkali" na ni hatari kwa Marekani.
Hatimaye, azma ya Biden ya urais - ilianguka mwishoni mwa Juni huko Atlanta wakati wa mjadala na Trump. Kubabaika kwake kukawa pigo kubwa ambalo lilionekana kuthibitisha mashambulizi ya Republican - na hofu kuhusu uzee wake.
Ushindi wa Trump dhidi ya Kamala Harris, mrithi aliyechaguliwa na Biden, ulikuwa ndio mwisho wa maisha ya kisiasa ya Biden, baada ya kukataliwa na kushindwa.
Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi