Filamu ya utekaji nyara wa ndege ya India yazua utata

    • Author, Neyaz Farooquee
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Tamthilia fupi kuhusu kutekwa nyara kwa ndege ya abiria ya India mwaka 1999, imezua mjadala nchini humo kuhusu majina ya watekaji.

Imeongozwa na Anubhav Sinha kwa ajili ya Netflix. Tamthilia ya ‘The Kandahar Hijack’ inasimulia juu ya utekaji nyara wa ndege iliyokuwa ikitoka Kathmandu kwenda Delhi ambayo ilipelekwa Kandahar, Afghanistan inayotawaliwa na Taliban ili kudai kuachiliwa kwa wanamgambo waliofungwa jela nchini India.

Mazungumzo hayo yalichukua siku nane, na kusababisha serikali ya India kuwaachilia wanamgambo watatu, akiwemo Masood Azhar, ili kubadilishana na abiria.

India inamlaumu Azhar, ambaye alianzisha kundi la Jaish-e-Mohammad baada ya kuachiliwa kwake, kwa mashambulizi kadhaa nchini humo. Pia anatajwa na Umoja wa Mataifa kuwa ni gaidi.

Uamuzi wa kumwachilia Azhar na wengine unasalia kuwa na utata nchini India, huku upinzani mara nyingi ukikosoa chama tawala cha Bharatiya Janata Party (BJP), ambacho kilikuwa madarakani mwaka 1999, kwa hatua hiyo.

Kuna utata gani?

Ni tamthilia ya vipande sita vinavyotokana na kitabu cha Flight Into Fear: The Captain's Story, cha Devi Sharan, ambaye alikuwa rubani wa ndege iliyotekwa nyara, na mwanahabari Srinjoy Chowdhury.

Tamthilia hiyo uliyotolewa wiki iliyopita, inaanza na watekaji nyara wakiingia kwenye ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Tribhuvan huko Kathmandu.

Ndani ya dakika chache baada ya kupaa, wanamgambo hao walitangaza kuwa ndege hiyo - iliyobeba abiria 179 wakiwemo watekaji nyara watano na wafanyakazi 11 - imetekwa nyara.

Tamthilia hiyo inaangazia mwingiliano kati ya watekaji nyara, wafanyakazi na abiria, na pia inaonyesha maafisa wa serikali ya India wakifanya kazi kutatua mzozo huo.

Mzozo huo ulianza baada ya baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii kuwakosoa wasanii hao kwa kuwaonyesha watekaji nyara wakiitana majina ya Kihindi kama vile Bhola na Shankar, ingawa majina yao ni Ibrahim Athar, Shahid Akhtar Sayed, Sunny Ahmed Qazi, Mistri Zahoor Ibrahim na Shakir. Wote walikuwa kutoka Pakistan.

Kiongozi wa BJP Amit Malviya alisema katika chapisho kwenye X (zamani Twitter), kwa kutumia utambulisho usio wa kiislamu wa watekaji nyara katika tamthilia hiyo, watengenezaji wa filamu wanataka kuwaaminisha watu kuwa Wahindi ndio waliteka nyara ndege."

Shirika la mrengo wa kulia la Kihindu limewasilisha kesi katika mahakama ya Delhi kutaka kupigwa marufuku kwa tamthilia hiyo. Shirika la habari la PTI liliripoti, ombi hilo limemshutumu mtengenezaji wa filamu kwa kupotosha ukweli muhimu kuhusu matukio ya kihistoria.

Vyombo kadhaa vya habari vya India, viliripoti kwamba serikali ya shirikisho ilifanya mkutano na mtendaji mkuu wa Netflix kuhusu suala hilo.

Netflix na wizara ya habari na utangazaji ya India hazijajibu ombi la BBC la kutoa maoni.

Ukweli ni upi?

Wengine wametetea tamthilia hiyo, wakisema iko sahihi. Taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya ndani ya India mwaka 2000 inathibitisha, watekaji nyara walitumia majina ya lakabu kuwasiliana ndani na nje ya ndege.

"Kwa abiria, watekaji nyara hawa walijuulikana kama (1) Mpishi, (2) Daktari, (3) Burger, (4) Bhola, na (5) Shankar, majina ambayo watekaji nyara waliitana kila wakati,” ilisema taarifa hiyo.

Mashahidi na waandishi wa habari walioripoti tukio hilo pia wamethibitisha hilo siku za nyuma.

Kollattu Ravikumar, manusura wa utekaji nyara ambaye alifanya kazi kama nahodha wa meli ya kibiashara ya kampuni moja yenye makao yake makuu nchini Marekani, alithibitisha lakabu hizo katika makala kwenye tovuti ya habari ya Rediff mwaka 2000.

“Watekaji nyara wanne waliokuwa wakituangalia walikuwa na kiongozi anayeitwa Berger. Na Berger mara nyingi alikuwa akipiga kelele. Berger alivyowaita, nilishika majina ya wengine - Bola, Shankar na Doctor," alisema.

Hii si mara ya kwanza kwa majukwaa ya kimataifa ya kuonyesha filamu kupokea malalamiko kuhusu maudhui kwenye majukwaa yao nchini India.

Mnamo Januari, Netflix iliondoa filamu ya lugha ya Kitamil baada ya mashirika ya Kihindu yenye msimamo mkali kupinga matukio kadhaa katika filamu hiyo.

Mnamo 2021, waigizaji na wasimamizi wa onyesho la Amazon Prime, Tandav, waliomba msamaha baada ya kushutumiwa kwa kudhihaki miungu ya Kihindu.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah