Belarus yawatenga wafungwa wa kisiasa ili kuwavunja moyo

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Maria Kolesnikova, mwaka 2020, alihukumiwa kifungo cha miaka 11 jela kwa tuhuma za itikadi kali na kujaribu kunyakua madaraka.

Kwa karibu miezi sita, Maria Kolesnikova amefichwa na ulimwengu.

Mwanaharakati huyo wa upinzani nchini Belarus amezuiliwa kwa kutengwa gerezani nchini humo tangu Februari, bila simu, barua wala kutembelewa na jamaa au wakili wake.

"Nasubiri habari kila siku...hatujui kama yuko hai," dadake Maria, Tatsiana Khomich, aliiambia BBC hivi majuzi huko Warsaw.

"Natumai hii haitamvunja moyo, lakini bila shaka itaathiri akili ya mtu yeyote mwishowe," alisema, na kuongeza: "Inaweza kuchukuliwa kama mateso."

Huku mamlaka nchini Belarus ikiendelea kuwasaka na kuwaweka kizuizini wale waliohusika katika mikutano mikubwa ya upinzani miaka mitatu iliyopita, pia sasa wanawashikilia wafungwa maarufu wa kisiasa nchini humo "bila mawasiliano".

Sergei Tikhanovsky na Viktor Babaryko wametoweka kwenye mfumo wa magereza, pamoja na watu wengine muhimu kutoka kwa upinzani.

Mnamo mwaka wa 2020, wanaume wote wawili walijaribu kugombea urais dhidi ya Alexander Lukashenko, lakini walikamatwa.

"Nadhani wanataka kuwavunja azma" ndivyo Tatsiana alivyoelezea kutengwa kwa wafungwa mashuhuri kama dada yake.

"Wanaona bado wana matumaini na wana nguvu sana, na wanataka kuvunja mawazo yao."

.

Chanzo cha picha, Matt Goddad

Maelezo ya picha, Tatsiana Khomich anasema dadake Maria ametengwa kabisa na ulimwengu wa nje kwa karibu miezi sita
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Maria Kolesnikova alikuwa mmoja wa wanawake watatu ambao waliukusanya umati wa watu katika maandamano ya nchi nzima baada ya Bwana Lukasjenko kudai kuwa alipata ushindi mwingine wa kishindo katika uchaguzi huo.

Mwitikio wa mkusanyiko huo haujawahi kushuhudiwa nchini humo .

Maandamano ya kupinga kura iliyoibiwa yaliishia katika kukamatwa kwa watu wengi, kupigwa na kuteswa - yote yakiwa yamethibitishwa, lakini bado yalikanushwa kabisa na maafisa.

Maria alisimama kidete sio tu wafuasi wake, lakini kwa tabasamu la mara kwa mara walilounda na mtazamo wake mzuri wa ukaidi.

Ni roho hiyo iliyomfanya aikate pasipoti yake hati waati mamlaka ilipojaribu kumfukuza nchini - na hiyo ilimfanya akamatwe.

Mara ya mwisho Tatsiana kuwasiliana na dada yake ilikuwa kupitia kadi iliotumwa tarehe 2 Februari 2023.

Maria aliandika kuhusu siku zake za zamani, zilizokuwa huru ambapo angekunywa kahawa nyingi na kujadili miradi mipya na marafiki.

Lakini alitabasamu, akimhakikishia Tatsiana kwamba alikuwa "mwenye afya", na hali yake "iliuwa njema.

Alexander Lukashenko amedai mara kwa mara kuwa hakuna mfungwa wa kisiasa "hakuna hata mmoja" huko Belarusi, kwa sababu hakuna nakala kama hiyo katika kanuni za uhalifu.

Lakini kundi linaloheshimika la haki za binadamu la Viasna kwa sasa linaorodhesha takriban watu 1,500 waliofungwa jela kwa matendo yao ya kisiasa au mitazamo.

Mmoja wa wanaharakati wake, aliyeachiliwa hivi punde, alilazimishwa kutumia siku zake tisa za mwisho katika kifungo cha upweke, akilala kwenye sakafu yenye unyevunyevu ya saruji na akitumia mkono wake kama mto.

"Wafungwa watatu wa kisiasa wamekufa gerezani, kwa hivyo inaweza kuwa muhimu kwa angalau mtu kuwaona," Natalia Satsunkevich aliniambia kutoka Lithuania, ambapo mwanaharakati wa Viasna sasa anaishi akihofia usalama wake.

Alimkumbuka msanii Alex Pushkin ambaye alifariki hivi karibuni akiwa kizuizini kwa sababu isiojulikana .

"Alikuwa amepoteza uzani mwingi.

Kwa hivyo ni dhahiri," Natalia alisema.

Na kumata kamata haijakoma.

.

Chanzo cha picha, Matt Goddad

Maelezo ya picha, Inga na mwanawe walilazimika kukimbilia Poland baada ya kukamatwa kwa kushiriki maandamano

Katika makao ya wanawake huko Warsaw, Inga alielezea jinsi polisi walikuja kwake miaka miwili baada ya maandamano kukandamizwa.

Walikuwa wamepata picha zake kwenye simu ya rafiki yao, ikiwa ni pamoja na moja kutoka kwenye mkutano ambapo alikuwa amevalia bendera ya upinzani nyekundu na nyeupe kama kofia.

"Walisema, ikiwa wewe ni 'wa kisiasa', basi utahisi," Inga alisema, alipokuwa akikumbuka wiki yake katika kituo cha kizuizini cha Okrestina katika mji mkuu wa Belarusi Minsk.

Kulikuwa na wanawake 14 katika seli yenye vitanda vinne; hakuna kuoga, kupiga mswaki au karatasi ya kwenda haja kubwa.

"Walitutendea kama wanyama," aliongeza.

Lakini hiyo sio kumbukumbu inayomfanya alie. Ni wakati anakumbuka kuhamia kizuizini kabla ya kesi na kugundua kuwa kila mtu katika seli yake alikuwepo kwa ajili ya siasa.

"Tulikuwa na runinga ya serikali na ilizungumza kana kwamba hakuna kitu kibaya kinachoendelea," Inga alisema. "Na tulisema inawezaje kusema hali iko sawa, ilhali watu wengi wako gerezani?

"Sikujua watu wanafungwa kwa idadi kama hiyo. Halafu unafika na kila mtu ni mwanasiasa. Ni ndoto," alijificha, akilia kimya kimya. "Tunapelekwa gerezani, kwa maneno yetu tu."

Akiwa amehukumiwa kifungo cha nyumbani, Inga alitoroka nchini mapema mwaka huu akisaidiwa na wanaharakati.

Hakumwambia mwanawe wanakwenda wapi hadi walipofika salama Ulaya. Hakuweza kumuhatarisha kufichua siri.

Sasa anajiunga na mkutano wa hadhara katikati mwa mji wa Warsaw kila Jumapili ili kuimba nyimbo za Belarusi, kukumbuka wafungwa wengine wa kisiasa na kuimba dhidi ya vita ambavyo nchi yao inasaidia kuipiga Ukraine.

Ni wachache tu waliojitokeza, ingawa idadi ya wahamiaji wa Belarusi nchini Poland inaongezeka kila wakati.

" Nafikiri huo ni usaliti,” mratibu Anna Fedoronok aliniambia. “Ikiwa tutawasahau watu wote walio gerezani, basi tunawasaliti.

"Tuko huru hapa. Tusipozungumza, nani atazungumza?"

Yeye na rafiki yake sasa wanacheza filamu za mitandao ya kijamii: wanavaa kama wanawake wazee, wamevaa hijabu na makoti ya nyumbani, wakikunja nyuso zao na kupiga kelele kwenye kamera.

Wanatoa picha ya Bwana Lukashenko kwenye sofa nyuma yao.

Wanawake wanapambana na utawala dhalimu kwa kuucheka.

.

Chanzo cha picha, ANN FEDERONOK

Maelezo ya picha, Mwanaharakati aliye uhamishoni Anna Fedoronok (kushoto) anaendelea kutoa upinzani kupitia michoro ya kejeli mtandaoni

"Sina silaha nyingine," Anna alisema. "Nikae tu hapa na kusubiri mabadiliko? Siwezi."

Wakati viongozi mashuhuri wa upinzani kama Maria Kolesnikova walipohukumiwa vifungo virefu, wafuasi wao walijaribu kubaki na mtazamo chanya: Alexander Lukashenko hangeweza kudumu madarakani kwa muda mrefu hivyo, walisema.

Kwa hiyo wafungwa wangeachiliwa hivi karibuni.

Badala yake wanaadhibiwa zaidi, kwa kutengwa.

"Wanataka kuwasahaulisha watu, ili wasiongee kuwahusu," Tatsiana Khomich anaamini.

"Wanataka kurejea maishani kama kawaida, kana kwamba hawakuwahi kuwatesa watu au kuwahukumu miaka 10 au 20," aliongeza.

"Lakini hawawezi kufanikiwa katika hilo."