Vita vya Ukraine: Mbinu mpya ya Urusi kuzuia usambazaji wa bidhaa za Ukraine

Baada ya Kremlin kukataa kusaini mpango mpya wa kuruhusu meli kusafirisha nafaka katika Bahari Nyeusi, Urusi ilianza kulenga njia kuu za Ukraine za kuuza bidhaa zake nje kupitia mto Danube.

Tumechunguza miundombinu ya nafaka inayolengwa na matokeo ya ongezeko hili la mbinu mpya kwa biashara ya dunia.

Ni nini kiliathiriwa?

Tangu kuzinduliwa kwake Agosti 2022, karibu tani milioni 33 za nafaka na vyakula vingine vimesafirishwa nje ya nchi chini ya Mkataba wa Nafaka za Bahari Nyeusi.

Hata hivyo, huku bandari za Bahari Nyeusi za Ukraine sasa zikiwa zimezuiliwa na Urusi, wataalam wanasema Ukraine italazimika kutegemea kwa kiasi kikubwa bandari zake kwenye mto Danube kusafirisha nafaka katika nchi jirani ya Romania.

Kutoka hapo, nafaka zinaweza kusafirishwa kwenye nchi zingine, huku bandari za Romania zikiendelea na shughuli.

Baada ya kuvilenga mara kwa mara vituo vya usafirishaji katika Bahari Nyeusi, Urusi sasa imeanza kushambulia kwa makombora na ndege zisizo na rubani bandari za Danube.

Moja ya mashambulio ya hivi karibuni ya Urusi yalilenga bandari ya Reni, huku makombora yakianguka karibu mita 200 kutoka mpaka na mwanachama wa NATO, Romania karibu na Danube.

Katika Bahari Nyeusi, uharibifu mkubwa zaidi wa miundombinu ya bandari ulionekana huko Chornomorsk, ambapo angalau maghala mawili ya kuhifadhi nafaka yanaonekana kushambuliwa usiku wa Julai 19.

Mamlaka ya Ukraine inadai kuwa tani 60,000 za bidhaa za kilimo ziliharibiwa kwenye eneo hilo.

Tulikichunguza pia kupitia picha za satelite Kituo kikuu cha nafaka kwenye bandari ya Odessa.

Jiji la Odessa hivi karibuni limekumbwa na mashambulizi kadhaa, lakini mashambulizi mengine hayaonekani kuvuruga biashara ya nafaka.

Kusini zaidi, katika maeneo ambako Ukraine hutumia njia nyinginezo za kusafirisha bidhaa karibu na Bahari Nyeusi, uharibifu ni mkubwa zaidi.

Kulingana na Lloyd's List, kampuni inayofuatilia masoko ya kimataifa ya baharini, mashambulizi 19 ya ndege zisizo na rubani kwenye bandari za Danube yalirekodiwa usiku wa Julai 24, na kugusa njia kuu za usafirishaji za nje za Ukraine.

Shambulio la Urusi dhidi ya Reni lilisababisha uharibifu mkubwa.

Picha za setelaiti zinaonyesha mashambulizi hayo yalilenga maghala kadhaa, na majengo mengine kwenye bandari.

Daraja la Zatoka - kiungo muhimu kinachoruhusu malori ya nafaka kufikia bandari ya Danube ya Izmail - pia liliripotiwa kugongwa.

Je, kuna athari gani kwa mauzo ya nje?

"Mwishoni mwa makubaliano ya mkataba wa nafaka, mauzo ya nafaka ya kutoka Ukraine yatafikia,kiwango chao cha juu zaidi, takriban tani milioni 2.5 kwa mwezi kupitia mto, barabara na reli," anasema mtaalamu wa sera Mariia Bogonos mtaalamu wa kilimo katika Shule ya Uchumi ya Kyiv.

Sehemu kubwa ya kiwango hichi kingepitia Danube.

"Kabla ya vita, Odessa ilikuwa msafirishaji mkuu wa nafaka, lakini katika miezi ya hivi karibuni, kutokana na shughuli za polepole huko Odessa, Danube imekuwa njia kuu ya usafiri," anasema Andrey Sizov, mtaalam wa masoko ya kilimo kutoka Bahari Nyeusi.

Ingawa mashambulizi ya hivi majuzi yamefunga kwa muda bandari ya Reni, bandari zote za Danube zinaonekana kurejea katika shughuli zao za kawaida tena kwa haraka. Kwa mujibu wa Lloyds List, mgomo huo haukuathiri sana biashara kwenye njia hiyo ya maji.

Usumbufu wowote zaidi huathiri maeneo mengine ya Ulaya na dunia, kwani bei ya ngano duniani kote itapanda iwapo biashara itasitishwa.

Bei ya ngano imepanda zaidi ya 10% tangu makubaliano ya kuruhusu usafirishaji wa nafaka kwa usalama kupitia bandari za Bahari Nyeusi kuvunjika.

Meli nyingi za kibiashara kwa sasa zinasafiri kupitia mto Danube na kusubiri kwenye mlango wa mto, kwa mujibu wa taarifa za kufuatilia meli ya Lloyd's List.