Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Msafirishaji haramu wa watu: 'Ninawapa wateja fomu ya kusaini kukubaliana na hatari'
Msafirishaji haramu wa watu anasema mpango wa serikali ya Uingereza kupeleka watu wanaotafuta hifadhi nchini Rwanda sio kikwazo kwa wateja wake. Mwandishi wa BBC anakutana naye katika kituo chake huko Uturuki ikiwa ni katika uchunguzi kuhusu jinsi maelfu ya wahamiaji wanavyoishia kwenye fukwe za kusini mwa Uingereza wakidai hifadhi.
Msafirishaji huyu wa watu anayetoka Mashariki ya Kati -ni kijana na anayezungumza kwa upole, amevalia nguo nadhifu za rangi nyeusi, anakubali kuzungumza kuhusu biashara yake ikiwa utambulisho wake utafichwa akiwa na walinzi nje ya nyumba.
"Najua hii si halali," anasema, "lakini kwangu mimi ni kuhusu ubinadamu - hiyo ni ya thamani zaidi kuliko sheria. Tunasaidia watu, tunawatendea vizuri, tunaheshimu wanawake, hatudharau au kumdhuru mtu yeyote."
Karibu watu 2,000 wamefariki katika Bahari ya Mediterania mwaka jana.
Mwezi Aprili, serikali ya Uingereza ilitia saini mkataba wa pauni milioni 120 na Rwanda kutuma baadhi ya wahamiaji, wengi wao wakiwa wanaume wasio na wenza, kwenda Afrika ili madai yao ya hifadhi yashughulikiwe.
Serikali ilisema lengo ni kuvunja muundo wa biashara ya watu wanaosafirishwa kimagendo na kuzuia idadi ya watu wanaovuka njia hatari katika mkondo wa Bahari Uingereza.
Tayari mwaka huu, zaidi ya watu 30,000 wamevuka kwa boti ndogo, kama wengi wa mwaka jana.
Mfanyabiashara huyu wa magendo ya watu hutuma mamia ya wahamiaji nchini Uingereza. Anakiri kwa urahisi biashara yake ina faida kubwa na anasema anaiendesha kama mfanyabiashara.
"Haijalishi ikiwa ni familia nzima au mtu binafsi - kila mtu analipa bei sawa," anasema. "Safari ya Uingereza itagharimu $17,000 [kama £15,000] kwa jumla."
Kwa hivyo anawezaje kuhalalisha kuweka maisha ya watu hatarini katika vivuko hatari vya baharini katika boti dhaifu?
"Ajali zinaweza kutokea. Tunajaribu na kuwatisha watu ili kuwakatisha tamaa," anadai. "Ninawaambia, 'Barabara hii ni hatari na haifai. Unaweza kufa. Na ninawaambia mama yake na baba yake pia."
Anatuonyesha fomu ya madai, ambapo anasema huwapa wateja kusaini, kukubali hatari.
Istanbul ni lango kati ya Asia, Mashariki ya Kati, Afrika na Ulaya na biashara hii haramu inashamiri hapa.
Soko lina ushindani. Kwenye mitandao ya kijamii, wasafirishaji haramu hutoa viwango tofauti kulingana na mahali wanaposafirisha.
Kuna pasi bandia na leseni za udereva za Uingereza zinazouzwa. Hata sampuli za maswali kutoka kwa maafisa wa Ofisi ya Mambo ya Ndani ya Uingereza ili kuwatayarisha wahamiaji kwa mahojiano
Mlanguzi wa watu hukusanya wateja wake katika nyumba salama katika jiji hili kubwa, ambalo ni makao ya wakimbizi wapatao milioni tano. Wamefungwa ndani ya vyumba vidogo, ambapo wanaweza kusubiri miezi wakati safari yao inapangwa. Genge lake linawaletea chakula na maji kutoka kwenye maduka makubwa ya mitaani.
"Tunawaweka ndani ya nyumba na kusubiri kila kitu kitayarishwe. Na ikiwa tayari tunachukua simu zao ili polisi wasijue kuhusu sisi," mfanyabiashara wa watu anaeleza.
Kisha wahamiaji hao huchukuliwa kwa gari usiku kutoka Istanbul hadi milimani. Wanatembea kwa vikundi vya watu sita au kumi, chini hadi Mediterania, kwenye mojawapo ya mashua za wasafirishaji wa magendo.
Wanakwenda Ugiriki au Italia.
Licha ya Msafirishaji haramu wa watu kukanusha, lakini kumekuwa na madai kuwa mhamiaji alifariki kwenye boti yake.
Anaonyesha baadhi ya video makumi ya vijana waliojaa kwenye viti vya boti wakipunga mkono, wakipiga kelele, wakimshukuru. Hizi sio shuhuda tu, ni uthibitisho kwamba wamevuka.
Pesa walizolipa kwa safari hiyo zinashikiliwa na wafanyabiashara wa kati(mtu wa kati) na hazitolewi hadi familia zione wako salama. Msafirishaji haramu hutoa hadi huduma ya kifahari ya VIP kwa wateja wanaoweza kulipa zaidi.
Wahamiaji hao kisha wanapitia Ulaya hadi ufukwe wa kaskazini mwa Ufaransa na, kwa baadhi, lengo lao kuu kuvuka Mfereji wa Uingereza hadi Uingereza.
Kuna mtandao wa magenge ya wahalifu kwenye umbali wa kilomita 100 (maili 60) kuzunguka Calais, ambao huwasaidia watu wanaosafirisha magendo nchini Uturuki kuwavusha wateja wake katika kizingiti cha mwisho.
"Tunanunua boti ndogo. Inagharimu takriban $10,000-$20,000," msafirishaji wa watu anasema. "Mmoja wa abiria anapata safari ya bure kwa kuongoza boti. Wanaenda moja kwa moja na wakifika huko, wanajisalimisha kwa polisi," anasema.
Biashara yake, mbali na kupata pigo, bado inaendelea.IUdadi ya watu bado inaendelea kuvuka bahari, wakati serikali ya Uingereza imerudi mahakamani kutetea kwamba mpango wake wa Rwanda uko salama na halali. Hukumu ya iwapo wahamiaji wanaweza kuanza kuondolewa inatarajiwa mwezi ujao.
Je, mkakati wa serikali utaleta mabadiliko yoyote?
"Hata wakipeleka watu 1,000 kwa siku nchini Rwanda, watu hawatasimama, au kubadilisha uamuzi wao," alisema kwa msisitizo. "Kama hawaogopi kifo, hawataogopa kwenda Rwanda."