Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wagonjwa wa Ghana wapo hatarini kwani wauguzi wanaelekea NHS nchini Uingereza - madaktari
Kuajiriwa kwa wauguzi na nchi zenye mapato ya juu kutoka mataifa maskini "kuko nje ya udhibiti", kulingana na mkuu wa moja ya vikundi vikubwa zaidi vya wauguzi duniani.
Maoni hayo yanakuja wakati BBC inapata ushahidi wa jinsi mfumo wa afya wa Ghana unavyotatizika kutokana na 'kuhama kwa wafanyikazi wenye ujuzi kutoka nchi hiyo hadi Ulaya'
Wauguzi wengi waliobobea wameondoka katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi kwa ajili ya kazi zenye malipo zaidi nje ya nchi.
Mnamo 2022 zaidi ya wauguzi 1,200 wa Ghana walijiunga na rejista ya uuguzi ya Uingereza.
Haya yanajiri huku Huduma ya Kitaifa ya Afya (NHS) ikizidi kutegemea wafanyikazi kutoka nchi zisizo za EU kujaza nafasi zilizoachwa wazi.
Ijapokuwa Uingereza inasema kuajiri watu nchini Ghana hairuhusiwi, mitandao ya kijamii inamaanisha wauguzi wanaweza kuona kwa urahisi nafasi zinazopatikana katika ndani ya NHS. Kisha wanaweza kutuma maombi ya kazi hizo moja kwa moja. Hali mbaya ya kiuchumi ya Ghana ni kigezo kikubwa.
Howard Catton kutoka Baraza la Kimataifa la Wauguzi (ICN) ana wasiwasi kuhusu ukubwa wa idadi inayoondoka katika nchi kama Ghana.
"Hisia yangu ni kwamba hali kwa sasa iko nje ya udhibiti," aliambia BBC.
"Tuna uajiri mkubwa unaoendeshwa hasa na nchi sita au saba za kipato cha juu lakini kwa kuajiriwa kutoka nchi ambazo ni baadhi ya nchi dhaifu na zilizo hatarini zaidi ambazo haziwezi kumudu kupoteza wauguzi wao."
Mkuu wa wauguzi katika Hospitali ya Mkoa ya Greater Accra, Gifty Aryee, aliiambia BBC kitengo chake pekee cha wagonjwa mahututi kimepoteza wauguzi 20 waliohamia Uingereza na Marekani katika kipindi cha miezi sita iliyopita - na madhara yake ni makubwa.
"Huduma inaathirika kwani hatuna uwezo wa kuchukua wagonjwa zaidi. Kuna ucheleweshaji na inagharimu zaidi vifo - wagonjwa wanakufa," alisema.
Aliongeza kuwa wagonjwa waliougua sana mara nyingi walilazimika kushikiliwa kwa muda mrefu katika idara ya dharura kwa sababu ya uhaba wa wauguzi.
Muuguzi mmoja katika hospitali hiyo alikadiria kuwa nusu ya wale aliokuwa amehitimu nao walikuwa wameondoka nchini - na alitaka kujiunga nao.
'Wauguzi wetu wote wenye uzoefu wamekwenda'
BBC ilipata hali kama hiyo katika Hospitali ya Manispaa ya Cape Coast.
Naibu mkuu wa huduma za wauguzi wa hospitali hiyo, Caroline Agbodza, alisema ameona wauguzi 22 wakiondoka kwenda Uingereza mwaka jana.
"Wauguzi wetu wote wa wagonjwa mahututi, wauguzi wetu wazoefu, wamekwenda. Kwa hivyo tunaishia kutokuwa na chochote - hatuna wafanyikazi wenye uzoefu wa kufanya nao kazi. Hata kama serikali itaajiri, lazima tupitie uchungu wa kuwafunza wauguzi tena."
Kliniki ndogo pia huathiriwa na uhamaji wa wafanyikazi kwa sababu hata muuguzi mmoja akitoka katika kituo kidogo cha afya inaweza kuwa na athari kubwa.
Katika Kliniki ya Afya ya Ewim huko Cape Coast, muuguzi mmoja ameondoka katika idara yao ndogo ya dharura na mwingine ameondoka katika kitengo cha wagonjwa wa nje. Wauguzi wote wawili walikuwa na uzoefu na walikuwa wamepata kazi nchini Uingereza.
Daktari mkuu huko, Dk Justice Arthur, alisema athari ni kubwa.
"Wacha tuchukue huduma kama vile chanjo ya watoto. Ikiwa tutapoteza wauguzi wa afya ya umma, basi watoto ambao wanapaswa kuchanjwa hawatapata chanjo yao na tutapata watoto kufa," aliambia BBC.
Alisema wagonjwa waliokomaa pia watakufa iwapo hakutakuwa na wauguzi wa kutosha wa kuwahudumia baada ya upasuaji.
Wauguzi wengi ambao timu ya BBC ilizungumza nao walitaka kuondoka Ghana kutokana na ukweli kwamba wangeweza kupata mapato zaidi kwingineko.
Katika kituo cha huduma za afya cha Kwaso karibu na jiji la Kumasi, Mercy Asare Afriyie alieleza kuwa alikuwa na matumaini ya kupata kazi nchini Uingereza hivi karibuni.
"Uhamisho wa wauguzi hautakoma kwa sababu ya hali duni za huduma. Mshahara wetu si kitu cha kuandika nyumbani na katika wiki mbili unautumia. Ni kutoka mkono hadi mdomo."
Wauguzi wa Ghana waliambia BBC kwamba nchini Uingereza wanaweza kupokea zaidi ya mara saba ya wanayopokea nchini Ghana.
Perpetual Ofori-Ampofo kutoka Chama cha Wauguzi na Wakunga cha Ghana alisema mfumo wa afya wa nchi yake unahitaji msaada zaidi.
"Ukiangalia idadi, basi sio maadili kwa Uingereza kuajiri kutoka Ghana kwa sababu idadi ya wauguzi wa kitaalamu ikilinganishwa na wauguzi wanaofunzwa au wauguzi wasaidizi ni tatizo kwetu," alisema.
Lakini aliongeza kuwa haikuwezekana kuwazuia wauguzi kuondoka kwani uhamiaji ni haki na kwamba serikali ya Ghana ilihitaji kufanya zaidi kuwashawishi kubaki. Wizara ya afya katika mji mkuu, Accra, ilikataa kutoa maoni.
Ghana iko kwenye orodha ya Shirika la Afya Ulimwenguni ya nchi 55 zilizo hatarini, ambazo zina idadi ndogo ya wauguzi kwa kila mtu ikilinganishwa na idadi ya watu. Orodha hiyo - iliyopewa jina na wengine kama "orodha nyekundu" - imeundwa ili kuzuia uandikishaji wa utaratibu katika nchi hizi.
Hivi majuzi serikali ya Uingereza ilitoa pauni milioni 15 ($18.6m) kwa Ghana, Nigeria na Kenya ili kusaidia kuongeza nguvu kazi zao za afya.
Lakini nchi hiyo inajulikana kuwa inaangazia kupata mkataba rasmi na Ghana ambapo inaweza kuwa na uwezo wa kuajiri kwa vitendo zaidi kwa ajili ya kuipa serikali ya huko kiasi cha fedha kwa kila muuguzi.
Tayari ina makubaliano sawa na hayo na Nepal.
Lakini Bw Catton wa ICN alihoji kama inatosha.
Aliiambia BBC kwamba anaamini kuwa mikataba kama hiyo "inajaribu kuunda hali ya heshima ya kimaadili badala ya kuakisi gharama halisi kwa nchi ambazo zinapoteza wauguzi wao".
Mkurugenzi wa Wafanyakazi wa Afya wa WHO, Jim Campbell, alieleza BBC kwamba Brexit imekuwa sababu ya Uingereza kugeukia nchi za Afrika kwa wauguzi kujaza nafasi za NHS.
"Soko la ajira lina ushindani mkubwa duniani kote na, baada ya kufunga soko la ajira linalowezekana kutoka kwa uhuru wa Ulaya wa kutembea, tunachoona ni matokeo ya hilo katika suala la kuvutia watu kutoka Jumuiya ya Madola na mamlaka zingine."