Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jinsi Varenicline, inavyosaidia kuacha kuvuta sigara, ina madhara gani?
Dawa itakayokusaidia kuacha kuvuta sigara. Hivyo ndivyo wizara ya afya nchini Uingereza inavyoielezea varenicline, dawa ambayo sasa itatolewa bure nchini humo ili kuwasaidia watu kuacha uvutaji wa sigara.
Varenicline, pia huitwa Chantix au Champix katika mataifa mengine, ni tembe ambayo humezwa kila siku katika kipindi cha miezi michache kulingana na maelekezo ya kitaalamu.
Kwa mujibu wa mamlaka za afya ni mbinu yenye ufanisi zaidi inayopatikana sasa ya kusaidia kuacha kuvuta sigara, ikitajwa kuwa na matokeo mazuri ikilinganishwa na jojo zenye nikotini.
Si dawa mpya. Katika baadhi ya mataifa ilikuwa kimbilio la kwanza katika kuacha uvutaji sigara,lakini ghafla iliondolewa sokoni mwaka 2021 baada ya Pfizer,baadara iliyozalisha,kusitisha uuzaji wake ulimwenguni.
Kampuni hiyo ya dawa ilifikia hatua hiyo kutokana na kuwepo kwa kile ilichosema ni "viwango visivyokubalika" vya kemikali inayosababisha saratani.
Mwaka mmoja baadaye, mwaka wa 2022, dawa nyingine sawa na varenicline, bupropion, kutoka GSK, pia iliondolewa kwenye soko kutokana na wasiwasi kama huo.
Vidonge hivyo viwili ambavyo vilipaswa kuleta mabadiliko makubwa katika kusaidia kupambana na saratani ya mapafu vinaweza kusababisha saratani.
Ulimwengu umeishiwa na dawa za kusaidia kuacha kuvuta sigara, na kutoa mbinu a mbadala pekee ya matibabu ya utumiaji wa nikotini, ambayo ni pamoja na nicotine patches, tembe na jojo.
Lakini sasa varenicline inapatikana tena duniani kote katika toleo ambalo mamlaka inaeleza kuwa "lililoboreshwa" na limeidhinishwa katika nchi kadhaa kuwa salama.
Hufanyaje kazi?
Tofauti na patches za nikotini au gum, varenicline haina nikotini na haifanyi tabia.
Inafanya kazi kwa kupunguza matamanio ya nikotini na kuzuia hali ya kuvutiwa na sigara kutokea kwenye ubongo, huku ikisaidia kupunguza dalili kama vile kuwashwa au kukosa usingizi.
Dawa hiyo kawaida huanza kufanya kazi ndani ya wiki moja baada ya kuanza kutumia na inapaswa kutumiwa kwa wiki 12 hadi 24 chini ya usimamizi wa kitabibu.
Mamlaka inapendekeza kutumia dawa hiyo pamoja na tiba saidizi au ushauri nasaha.
Kwa njia hii, kwa mujibu wa huduma ya afya ya Uingereza, inaweza kusaidia mtu mmoja kati ya wanne kuacha kuvuta sigara.
Utafiti uliofanywa nchini Uingereza na Chuo Kikuu cha London uligundua kuwa dawa hiyo ikitumiwa kwa njia hii inaweza kusaidia zaidi ya watu 85,000 kuacha kuvuta sigara kila mwaka ambapo katika nchi hii inaweza kuzuia karibu vifo 9,500 vinavyohusishwa na uvutaji sigara katika miaka mitano ijayo.
Kulingana na Vituo vya Udhibiti wa Magonjwa vya Marekani (CDC), varenicline inaweza kuwa chaguo zuri hasa kwa watu ambao hapo awali wamejaribu matibabu mengine ya kuacha kuvuta sigara bila mafanikio.
Madhara
Kama ilivyo kwa dawa nyinginezo, varenicline zina madhara,kwahiyo mamlaka imependekeza dawa hizi kutumika chini ya usimamizi wa kitabibu.
Vituo vya usimamizi wa magonjwa CDC vimeorodhesha yafuatayo;
• Kichefuchefu au kutapika (ndiyo sababu inashauriwa kuimeza pamoja na chakula au glasi ya maji).
• Matatizo ya usingizi, kama kukosa usingizi na ndoto za maruwe ruwe
• Matatizo ya tumbo, kama vile kuvimbiwa au kujaa gesi tumboni.
• Mabadiliko ya hisia au tabia.
Dawa hizi husababisha madhara ya figo na haishauriwi kutumiwa na wajawazito,au wanawake wanaonyonyesha,au mtu yeyote mwenye umri wa chini ya miaka 18.
'Dawa inayookoa maisha'
Barani ulaya,mamlaka za afya inaweza kurejesha tena varenicline sokoni.
Kuachana na uvutaji wa sigara si tu changamoto kwa wavutaji bali hata kwa watoa huduma za afya duniani.
Kwa mujibu wa watafiti nchini Hispania 30% pekee ya wanaotaka kuacha,wanaweza kupata huduma wezeshi,na 65% wanaojaribu wakiishia njiani ndani ya miezi mitatu tu.
Uvutaji wa sigara unaongoza kwa kuchangia maradhi na vifo vinayoweza kuepukika.
Uingereza kulikuwa na wagonjwa wapatao 400,000 waliosajiliwa maradhi yatokanayo na uvutaji wa sigara mwaka 2023.
Na kila mwaka wizara ya afya inatumia takribani dola za Marekani bilioni 3.2 kwa ajili ya kutibu matatizo ya kiafya yanayotokana na uvutaji sigara.
Mamlaka za afya zinaamini kwamba dawa hiyo inaweza kusababisha "mabadiliko makubwa" kwa watu wanaotaka kuacha kuvuta sigara na kwa huduma za afya duniani kote.
Profesa Nick Hopkinson, profesa wa dawa za mfumo wa upumuaji katika Chuo cha Imperial London, alisema varenicline ndiyo "dawa yenye ufanisi zaidi katika kusaidia kuacha kuvuta sigara".
Kutopatikana katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni kumesababisha changamoto kubwa na kuongeza: "Tunajua kwamba kuacha sigara ni jambo bora zaidi ambalo mvutaji sigara anaweza kufanya ili kuboresha afya yake na afya ya wale wanaomzunguka; hasa watoto na vijana'.
"Watu wana uwezekano mkubwa wa kuacha sigara kwa mafanikio ikiwa wanapata usaidizi wa kisaikolojia na dawa ili kupunguza kutamani kuvuta sigara na kusaidia kuvunja utegemezi wao kwa tumbaku."
Na anasisitiza kwamba dawa hiyo inaweza kuwa "muhimu sana" kwa wale ambao hawajafanikiwa kuacha kuvuta sigara kwa kutumia dawa nyingine kama vile jojo zenye nikotini kama ilivyokuwa ikifahamika hapo awali.
Imetafsiriwa na Martha Saranga na kuhaririwa na Ambia Hirsi