Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Rosenberg: Jinsi miaka miwili ya vita vya Ukraine ilivyoibadilisha Urusi
Na Steve Rosenberg
Mhariri wa Taarifa za Urusi
Nilipokuwa nimesimama nikiwatazama Warusi wakiweka mashada ya maua kwa heshima ya kiongozi wa upinzani Alexei Navalny, kijana mmoja alishiriki jinsi alivyopokea kifo cha Bw Navalny gerezani.
"Nimeshtuka," aliniambia, "kama vile miaka miwili iliyopita mnamo Februari 24: wakati vita vilipoanza."
Hii ilinifanya nifikirie juu ya kila kitu ambacho kimetokea nchini Urusi miaka hii miwili iliyopita, tangu Rais Putin aamuru uvamizi kamili wa Ukraine.
Ni orodha ya visa vya umwagaji damu, na misiba.
- Vita vya Urusi vimesababisha vifo na uharibifu kwa Ukraine. Jeshi la Urusi pia limepata hasara kubwa.
- Miji ya Urusi imepigwa kwa makombora na mashambulizi ya droni;
- Mamia ya maelfu ya wanaume wa Kirusi waliandikishwa jeshini;
- Mamluki wa Wagner waliasi na kuandamana kwenda Moscow. Kiongozi wao Yevgeny Prigozhin alifariki baadaye katika ajali ya ndege.
- Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ilitoa waranti ya kukamatwa kwa rais wa Urusi kwa tuhuma za uhalifu wa kivita.
- Sasa mkosoaji mkubwa wa Vladimir Putin amekufa.
- Tarehe 24 Februari 2022 ilikuwa wakati mzuri sana.
Lakini kuangalia nyuma mwelekeo wa vita ulikuwa wazi. Ilikuwa mwaka wa 2014 ambapo Urusi ilikuwa imechukua jimbo la Crimea kutoka Ukraine na kuanza kuingilia kijeshi jimbo la Donbas; Alexei Navalny alikuwa ametiliwa sumu ya kuathiri mfumo wa neva inayojulikana kama Novichok mwaka 2020 na kufungwa jela mwaka wa 2021.
Ukandamizaji wa ndani nchini Urusi ulianza kabla ya uvamizi wa Ukraine, lakini umeongezeka tangu wakati huo.
Kuhusu Vladimir Putin, miaka miwili ya vita hivi anaonekana kujiamini zaidi na kuamua kuwashinda maadui zake nyumbani na nje ya nchi. Anapingana na Marekani , Nato na EU na anavielezea vita vya Urusi nchini Ukraine kama vita dhidi ya Urusi na "magharibi kwa pamoja", vita vitakavyokuwepo kwa maisha yake.
Je, vitaisha lini? Siwezi kutabiri siku zijazo. Ninaweza, hata hivyo, kukumbuka yaliyopita.
Katika kabati langu la nyumbani hivi karibuni nilipata nakala za taarifa zangu fupi kuhusu Urusi za zaidi ya miaka 20 iliyopita: miaka ya mapema ya utawala wa Putin.
"Kulingana na kura ya maoni ya hivi majuzi, asilimia 59 ya Warusi wanaunga mkono wazo la Urusi kujiunga na Umoja wa Ulaya ..." niliandika tarehe 17 Mei 2001.
"Nato na Urusi zinatafuta ushirikiano wa karibu zaidi: ishara kwa pande zote mbili kwamba tishio la kweli la amani ya ulimwengu haliko kati ya kila mmoja..." [20 Novemba 2001] . Kwa hivyo, yote yalienda vibaya wapi? Sio mimi pekee ninayejiuliza.
Kuzisoma , ilikuwa ni kama kusoma kuhusu kitu kipya kabisa.
"Putin niliyekutana naye, nilifanya naye biashara nzuri, na kuanzisha naye Baraza la Nato-Urusi, ni tofauti sana na huyu wa sasa’’ Mkuu wa zamani wa Nato Lord Robertson aliniambia hivi majuzi tulipokutana London.
"Mtu aliyesimama kando yangu Mei 2002, kando yangu, na kusema Ukraine ni taifa huru na ambalo litafanya maamuzi yake kuhusu usalama, sasa ndiye mtu anayesema kwamba [Ukraine] si taifa ."
Bwana Robertson hata anakumbuka Vladimir Putin akitafakari uanachama wa Nato wa Urusi.
"Katika mkutano wangu wa pili na Putin, alisema kwa uwazi: 'Ni lini utaialika Urusi kujiunga na Nato?' Nilisema, 'Hatualiki nchi kujiunga na Nato, zinatuma ombi.' Na akasema, 'Vema, hatutasimama na kundi la nchi ambazo hazina maana.'
Bwana Robertson alisema hafikirii kwamba Putin alitaka kweli kuomba uanachama wa Nato.
"Alitaka uwasilishwe kwake, kwa sababu nadhani kila wakati alifikiria - na anazidi kufikiria - kwamba Urusi ni taifa kubwa katika ulimwengu na inahitaji heshima ambayo Muungano wa Soviet ulikuwa nayo," aliniambia.
"Kamwe hangeweza kufaa ndani ya muungano wa mataifa sawa, wote wakiwa wameketi kwenye meza wakijadiliana na kujadili maslahi ya sera ya pamoja."
Kuongezeka kwa kiburi’
Bwana Robertson anadokeza kwamba Muungano wa Usovieti uliwahi kutambuliwa kama mamlaka kuu ya pili duniani, lakini Urusi haiwezi kutoa madai yoyote katika mwelekeo huo leo.
"Nafikiri namna hiyo ilikula utu [wa Putin]. Kuchanganya hilo na udhaifu , wakati mwingine, wa Magharibi na kwa njia nyingi uchochezi ambao alikabiliana nao, pamoja na ubinafsi wake unaokua. Nadhani hiyo ilimbadilisha mtu ambaye alitaka kushirikiana na Nato katika mtu ambaye sasa anaona Nato kama tishio kubwa."
Moscow inaona mambo kwa njia tofauti. Maafisa wa Urusi wanadai kuwa upanuzi wa Nato kuelekea mashariki ndio ulidhoofisha usalama wa Ulaya na kusababisha vita. Wanaishutumu Nato kwa kuvunja ahadi kwa Kremlin, ambayo inadaiwa ilikufa katika siku za Muungano wa Usovieti -USSR, kwamba muungano huo hautakubali nchi zilizokuwa kwenye mzunguko wa Moscow.
"Hakika hapakuwa na chochote kilichoandikwa kwenye karatasi," Bwana Robertson ananiambia. "Hapakuwa na chochote kilichokubaliwa, hapakuwa na mkataba wa athari hiyo.
Lakini ni Vladmir Putin mwenyewe aliyetia saini Azimio la Roma tarehe 28 Mei 2002. Kipande hicho hicho cha karatasi nilichotia saini, ambacho kiliweka kanuni za msingi za uadilifu na kutoingilia nchi nyingine. Alitia saini hiyo. Hawezi kumlaumu mtu mwingine yeyote."
Makumbusho ya vita vya Solnechnogorsk ni kumbukumbu ya Warusi waliouawa katika "operesheni maalum ya kijeshi"
Katika mji wa Solnechnogorsk, maili 40 kutoka Moscow, miaka miwili ya mwisho ya historia ya Urusi inaonyeshwa kwenye bustani.
Ninaona mchoro wa unaounga mkono kikundi cha mamluki cha Wagner.
Kuna maua katika kumbukumbu ya Alexei Navalny.
Na kuna sanamu kubwa ya watu wawili wa ndani, askari Warusi , waliouawa katika Ukraine. Waliochorwa kando ni wanafunzi wa kijeshi wa Jeshi la Vijana akiwasalimia.
Katikati ya mji, katika kumbukumbu ya wale waliouawa katika Vita vya Pili vya Dunia na vita vya Usovieti nchini Afghanistan, sehemu mpya imeongezwa:
"Kwa askari waliouawa katika operesheni maalum ya kijeshi." Majina arobaini na sita yamechorwa kwenye jiwe.
Nakutana na Lidiya Petrovna, akipita na mjukuu wake, na namuuliza jinsi maisha yalivyobadilika katika miaka miwili.
"Viwanda vyetu sasa vinatengeneza vitu tulivyokuwa tukinunua nje ya nchi. Hiyo ni nzuri," Lidiya anasema. "Lakini nina huzuni kwa vijana, kwa kila mtu, ambaye ameuawa. Hakika hatuhitaji vita na Magharibi. Watu wetu hawajaona chochote isipokuwa vita, vita, vita maisha yao yote."
Ninapozungumza na Marina, anawasifu wanajeshi wa Urusi ambao anasema "wanafanya wajibu wao" nchini Ukraine. Kisha anamtazama mtoto wake Andrei mwenye umri wa miaka 17.
"Lakini kama mama nina hofu kwamba mwanangu ataitwa kupigana. Nataka amani haraka iwezekanavyo, ili tusiogope kitakachotokea kesho."
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Ambia Hirsi