Mwanafunzi Mtanzania nchini Israel: 'Mabadiliko ya zamu yaliniokoa, lakini marafiki zangu ni mateka wa Hamas'

Na Priya Sippy

BBC News

"Iwapo singekuwa shambani asubuhi hiyo, ningekuwa mmoja wa waliotekwa," Ezekiel Kitiku aliambia BBC kutoka kusini mwa Israel.

Wenzake wawili - Joshua Loitu Mollel na Clemence Felix Mtenga - walikuwa miongoni mwa zaidi ya watu 230 waliochukuliwa mateka katika Ukanda wa Gaza, ambao uko chini ya udhibiti wa Hamas, uliopigwa marufuku kama kundi la kigaidi nchini Uingereza na nchi nyingine.

Wanafunzi hao watatu walikuwa wametua Israel mwezi Septemba, wakiwa na hamu ya kuanza kazi yao kama wataalamu wa kilimo kwa muda wa miezi 11 ijayo.

Tangu kuwasili kwao, Ezekiel Kitiku na Bw Mtenga walikuwa wakiishi Kibbutz Nir Oz na kufanya kazi katika shamba la maziwa nyakati za mchana. Rafiki yao Bw Mollel alikuwa anakaa na kufanya kazi umbali wa kilomita 30 (maili 18) huko Kibbutz Nahal Oz. Kibbutz zote mbili zina idadi ya watu mia kadhaa na ziko karibu sana na Gaza.

"Wiki hiyo ratiba mpya ilitayarishwa na jina langu likatajwa kufanya kazi za usiku, lakini Clemence alisalia zamu za mchana," Bw Kitiku aliambia BBC. Bw Mollel alikuwa zamu za mchana katika shamba tofauti.

Mwendo wa saa saba usiku mnamo tarehe 7 Oktoba, Bw Kitiku anasema aliondoka gizani kwa baiskeli yake na akapanda dakika tano hadi shambani kuanza zamu yake.

Alitumia muda wote asubuhi hiyo kukamua ng’ombe na kutekeleza majukumu mengine ya ufugaji. Kufikia saa kumi na mbili , jua lilipoanza kuchomoza, alikuwa akichunga ng'ombe ndani ya zizi.

Dakika thelathini baadaye alisikia mlipuko mkubwa. Hapo ndipo Hamas walipoanza kurusha makombora kutoka Gaza.

“Niliposikia kelele hizo, nikakumbuka tuliambiwa kwamba tukisikia sauti ya risasi au mabomu twende kwenye makazi, hivyo ndivyo nilivyofanya.

"Niliogopa sana. Ilikuwa mara yangu ya kwanza kusikia kelele kama hii."

Alipokuwa akielekea kwenye makao hayo, aliona moshi mwingi na miali ya rangi ya chungwa ikifuka kutoka karibu na kibbutz yake, hivyo mara moja akawasiliana na marafiki zake wote wawili.

"Waliniambia kuwa kulikuwa na roketi nyingi sana zinazokuja kutoka Gaza - na kwamba walikuwa wakienda kwenye makazi pia."

Hata hivyo, bila kujua, wanamgambo wa Hamas walikuwa tayari wameanza kuvamia kibbutzi mbili ambapo marafiki zake walikuwa.

Saa chache baadaye, aligundua kuwa jumbe za WhatsApp na meseji zake hazikuwa zikitumwa tena kwa simu zao.

"Nilidhani labda simu zao hazikuwa na chaji. Ujumbe wa mwisho niliowatumia ulikuwa - 'Mko salama?'

Wala hawakujibu. Hii ilikuwa karibu saa nne . Hajasikia kutoka kwao tangu wakati huo.

Huku makombora yakirushwa siku nzima, Bw Kitiku alilazimika kubaki shambani, akijaribu kulala ndani ya makao hayo.

Asubuhi iliyofuata mambo yalipoonekana kuwa shwari kidogo na akitaka kujua nini kimewasibu marafiki zake, alimwomba meneja wake amrudishe kwenye kibbutz yake. Hapo aliweza kuona kwamba wanajeshi kutoka Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) walikuwa wametumwa.

"Kwenye lango la kibbutz kulikuwa na askari wengi wa IDF. Walinizuia kuingia na kuniambia nitalazimika kurudi kukaa kwenye shamba hilo kwa sababu lilikuwa salama zaidi."

Alibaki kwenye makazi shambani na watu wengine wawili kwa siku nyingine mbili - na chakula kidogo - na usiku mwingine akiwa peke yake.

Mwishowe IDF ilisema hangeweza kurudi kwenye kibbutz yake na wanajeshi walimsindikiza hadi eneo jingine karibu kilomita 30 kaskazini mwa Gaza.

Alipotoka shambani, alishtushwa na alichokiona nje ya geti.

"Mifumo ya maji ilikuwa imepigwa kwa mabomu, na maji yalikuwa yakitiririka kila mahali. Niliona maiti mitaani.

"Hofu ya kile kilichotokea kwa marafiki zangu ilianza kuongezeka."

Wanaume hao watatu walikuwa wamekutana katika kitovu cha uchumi cha Tanzania cha Dar es Salaam kupitia masomo yao ya kilimo miezi michache kabla ya kusafiri hadi Israel.

Haikuwa hadi wiki tatu baada ya shambulio la Hamas ambapo Bw Kitiku aligundua kilichowapata marafiki zake.

Wizara ya mambo ya nje ya Israel ilitangaza katika taarifa yake siku ya Jumapili kuwa wanazuiliwa mateka huko Gaza.

Anasema anashukuru kujua kwamba wote wawili wako hai, lakini bado ana wasi wasi kuhusu hali zao. Pia anawajua wanafunzi wengine kwenye programu yao ambao wamechukuliwa mateka, akiwemo mmoja kutoka Thailand.

Mbali na wale waliowachukua mateka, watu wenye silaha wa Hamas waliwaua takriban watu 1,400 tarehe 7 Oktoba, wengi wao walikuwa wakiishi kibbutzim.

Tangu wakati huo, Israel imefanya mashambulizi ya anga kwenye Ukanda wa Gaza. Wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas inasema takriban watu 9,000 wameuawa.

Bw Kitiku anasema ana wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wa marafiki zake wanaozuiliwa katika Ukanda wa Gaza.

"Kuna mashambulizi mengi ya mabomu na watu wana huduma chache za kijamii. Ninajaribu kujiweka katika viatu vyao, lakini siwezi kufikiria kile wanachopitia."

Anasema utambuzi wa jinsi alivyokaribia kunaswa katika shambulio hilo bado ni mzito akilini mwake.

“Siku chache za kwanza kisaikolojia sikuwa sawa, najaribu kujilazimisha kukabiliana na hali hiyo.

"Iwapo singekuwa shambani asubuhi hiyo, ningekuwa mmoja wa waliotekwa."

Sasa anafanya kazi katika shamba tofauti.

"Mamlaka nchini Israel walituambia tuko salama na tunaweza kuendelea na mafunzo yetu hapa," anasema.

Yeye na wanafunzi wengine wa kutoka Tanzania - kunakadiriwa kuwa na Watanzania 260 nchini Israel - wamepewa usaidizi na ubalozi wao kurejea nyumbani iwapo wanataka kufanya hivyo, anasema.

"Lakini ninawezaje kufikiria kurudi nyumbani wakati sijui hali ya marafiki zangu wawili huko Gaza?"

Mengi zaidi kuhusu mzozo wa Israel na Palestina