Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, Tanzania inalibeba soka la Afrika Mashariki?
- Author, Rashid Abdallah
- Nafasi, BBC Swahili
Timu ya taifa ya Tanzania imejinyakulia tiketi ya kushiriki mashindano makubwa zaidi ya mpira barani Afrika - Afcon. Miaka kadhaa imepita tangu ishiriki mara yake ya pili 2019. Miongo minne imekatika tangu ishiriki kwa mara ya kwanza 1980.
Mafanikio haya yanawaacha nyuma wanachama wakongwe wa Jumuiya ya Afrika Mashariki - Kenya na Uganda. Mataifa hayo hayajafanikiwa kukata tiketi ya kwenda magharibi mwa Afrika katika taifa la pembezoni mwa bahari ya Atlantic - Ivory Coast.
Mara ya mwisho Kenya kwenda Afcon ni 2019 - yalipofanyika Afrika Kaskazini nchini Egypt. Uganda nayo ilishiriki mwaka huo huo. Licha ya kuifunga Nigeria katika mchezo wa mwisho, lakini pointi zake hazikumvuusha kusonga mbele mara hii.
Je, kufuzu kwa Tanzania kunatosha kuwa kielelezo kwamba sasa wanalibeba soka la Afrika Mashariki? Takwimu zinasemaje? Na historia inajibu nini juu ya swali hilo?
Soka la Timu za Taifa
Tuzitazame takwimu za sasa za Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), imeiweka Tanzania katika nafasi ya 124. Timu nyingine za Afrika Mashariki, Kenya nafasi ya 105, DR Congo 69, Burundi 140, Rwanda 139, Uganda 92 na Sudan Kusini 186.
Miongoni mwa timu hizo ni DR Congo pekee wakati nchi hiyo ikijuulikana kama Zaire, iliposhiriki kombe la dunia mwaka 1974, na likawa ndilo taifa la kwanza kutoka Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kushiriki kombe hilo.
DR Congo ilitolewa bila kufunga goli hata moja katika hatua ya awali kwa kufungwa mechi zote tatu, ilipokutana na miamba ya soka ikiwemo Brazil. Toka wakati huo hakuna taifa mwanachama wa Afika Mashariki amefuzu kuingia mashindano hayo.
Ukitaja kombe la Dunia, nchi ya Nigeria, Misri, Algeria, Cameroon, Senegal, Ghana ndio huingia katika mashindano hayo mara nyingi miongoni mwa timu za Afrika. Upande wa Afrika Mashariki bado kiza kimetanda.
Katika ushiriki wa mashindano ya kombe la Afrika tangu kuanza kwake, Kenya imeshiriki mara sita mara yao ya kwanza ni 1972. Uganda saba mara ya mwanzo ni 1962. Burundi mara moja 2019. Rwanda mara moja 2004. Sudan Kusini haijawahi kwenda Afcon na juhudi zao za kwenda 2024 zinazidi kudidimia.
Nchi nyingine ambazo zimefuzu katika mashindano yajayo, huko Ivory Coast - 2024; ni DR Congo mara 19 na hii ya sasa itakuwa 20. Tanzania mara tatu ikijumuisha mara hii. Mwanzo walifuzu 1980, kisha 2019 .
DR Congo imeshinda kombe la Afrika mara mbili – 1968 iliizidi nguvu Ghana katika fainali iliyofanyika Ethiopia. Ushindi wao wa mara ya pili ni 1974 iliitwanga Zambia katika fainali iliyochezwa Misri.
Mashindano makongwe yanayojumuisha nchi za Afrika Mashariki na Kati, yaliyoasisiwa na Kenya, Zanzibar, Tanzania Uganda na Somalia ya CECAFA; nchi ya Uganda ndio imechukua makombe mara nyingi ikifuatiwa na Kenya.
Kwa kuzitazama takwimu hizi zote, soka la Tanzania kwa upande wa timu ya taifa haliwezi kuwa kinara mbele ya majirani zake. Mafanikio ya timu ya taifa bado ni madogo mno katika mashindano hayo yote.
Vilevile uwakilishi wa wachezaji wenye uraia wa Tanzania katika ligi kubwa kama zile za Ulaya, ni wa kutafuta kwa tochi. Hali hiyo haipishani na mataifa jirani. Kinyume chake mataifa ya Afrika ya Magharibi na Afrika Kaskazini yanafanya vyema katika eneo hilo.
Leo mataifa mengi Afrika Magharibi na Kaskazini, yamejaza wachezaji wenye majina makubwa kwenye soka la Ulaya kama Mohamed Salah, Mohamed Elneny (Misri), Sadio Mane na Edouard Mendy (Senegal), Partey (Ghana), Hakim Ziyech na Achraf Hakimi (Morocco), Riyah Mahrez (Algeria), Wilfred Ndidi, Kelechi Ihenacho na Victor Moses (Nigeria). Kukitaja kwa uchache kizazi cha sasa.
Soka la klabu
Tukigeukia soka la vilabu. Hili ni eneo pekee ambalo Tanzania inatazamwa kama kinara miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki. Ligi yake inazidi kupiga hatua kwa kasi kubwa.
Taarifa ya Shirikisho la kimataifa la historia na takwimu za mpira wa miguu (IFFHS), iliitangaza ligi yaTanzania bara kuwa ya tano kwa ubora barani Afrika mwaka 2022. Ikiwa imepanda kutoka nafasi ya 10.
Kimataifa ilipanda kutoka nafasi ya 62 hadi 39. Kwa Afrika iko nyuma ya ligi ya Misri, Algeria, Morocco na Sudan. Kwa kuzingatia takwimu hizi hii ni ligi bora Afrika Mashariki.
Akieleza mafanikio ya timu ya Simba, afisa habari wa timu hiyo Ahmed Ally, aliandika katika ukurasa wake wa Twitter mwezi Julai mwaka huu: Simba Sports Club imepanda viwango vya ubora wa Shirikisho la Mpira Afrika (CAF) kutoka nafasi ya 9 hadi nafasi ya 7.
Timu ya Yanga nayo imefanya vyema hivi karibuni. Mwaka huu imefanikiwa kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Pamoja na kwamba imekosa ubingwa - imeshika nafasi ya pili katika mashindano hayo kubwa ya vilabu Afrika baada ya Ligi ya Mabingwa.
Uwekezaji na udhamini umezidi kuongezeka katika ligi ya Tanzania bara. Umaarufu wa ligi umezidi kukuwa kwa sababu ya kupata bahati ya mechi zake kuoneshwa katika runinga. Manunuzi ya wachezaji kutoka nje ya Tanzania yamezidi kupanda.
Naam, Tanzania inalibeba soka la Afrika Mashariki katika upande wa ligi yake. Lakini haifanyi vizuri kwa upande wa timu taifa. Badala yake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, inaonekana kuwa na historia inayotazamika angalau ya timu yake ya taifa.