Ayatollah Khamenei: Jinsi kiongozi mkuu wa Iran alivyofanikiwa kuidhibiti Iran kwa 'mkono wa chuma'

    • Author, Sam Woodhouse and BBC News Persian
  • Muda wa kusoma: Dakika 13

Maoni na sera kali za mamlaka za Ayatollah Ali Khamenei zimekuwa na mchango mkubwa nchini Iran kwa karibu miongo minne.

Khamenei, 86, amekuwa kiongozi wa pili mkuu tangu mapinduzi ya 1979 baada ya kifo cha Ruhollah Khomeini mnamo mwaka 1989 na mwenye mamlaka ya juu zaidi nchini humo.

Kama kiongozi mkuu, alikuwa akidhibiti siasa za nchi, jeshi na taasisi za kidini za Iran ikiwa ni pamoja na kutoa mwongozo wa uhusiano wa masuala ya kigeni.

Kabla ya kuchukua wadhifa huo alikua rais wa taifa hilo kwa mihula miwili kuanzia 1981 hadi 1989.

Mamlaka ya ofisi yake yamemfanya Khamenei kuwa na nguvu zote kama mkuu wa nchi na kamanda mkuu wa jeshi, ikiwa ni pamoja na kikosi cha Revolutionary Guards.

Malezi ya kidini

Ali Khamenei alizaliwa Mashhad, jiji la pili kwa ukubwa nchini Iran, mwaka wa 1939.

Baba yake alikuwa kiongozi wa kidini wa Shia, tawi kuu la Kiislamu la Iran.

Khamenei alizungumzia sana utoto wake kama "maskini lakini mcha Mungu", akisema mara kwa mara hakula chochote ila "mkate na zabibu".

Alianza masomo ya dini huko Mashhad, akakaa kwa muda mfupi huko Najaf, Iraqi, kisha akasoma katika chuo cha dini katika mji wa Qom nchini Iran.

Wanachuoni kadhaa walimfundisha, ikiwa ni pamoja na Khomeini, ambaye baadaye alianzisha Jamhuri ya Kiislamu.

Khamenei alijiunga na wakosoaji wa Shah wa Iran, mfalme ambaye hatimaye alipinduliwa na mapinduzi ya mwaka 1979, ambayo mara nyingi hujulikana kama Mapinduzi ya Kiislamu.

Kwa miaka mingi, Khamenei aliishi kwa kujificha au alifungwa gerezani.

Polisi wa siri wa Shah walimkamata mara sita, na alikabiliwa na mateso.

Wakati wa mapinduzi, Khamenei hakuwa mtu maarufu kati ya watu waliokuwa karibu na Ayatollah Khomeini, lakini alijulikana haraka baada ya ghasia hizo.

Alijiunga na Baraza la Mapinduzi lililoongoza mapinduzi, na kuwa baraza la uongozi la muda baada ya kuanguka kwa utawala wa Shah.

Jukumu lake la kwanza la serikali ya Jamhuri ya Kiislamu lilikuwa naibu wa Wizara ya Ulinzi.

Khomeini alimteua kuwa kiongozi wa Sala ya Ijumaa huko Tehran mwaka huo, cheo ambacho alikishikilia rasmi kwa muda mrefu.

Mahubiri ya kisiasa ya Ali Khamenei, yaliyotangazwa nchi nzima, yalimfanya ajulikane ndani ya uongozi mpya.

Jaribio la mauaji

Mnamo mwaka 1981 Juni, Khamenei alinusurika jaribio la mauaji.

Kundi la wapinzani lililipua bomu kwenye mhadhara wake.

Huenda shambulizi hilo liliokoa maisha yake.

Khamenei alikuwa mwanzilishi mwenza na hatimaye kiongozi wa chama cha Islamic Republican, ambacho kilisaidia uongozi wa baada ya mapinduzi kuimarisha mamlaka.

Hata hivyo, alikuwa hospitalini wakati wa shambulizi kubwa la mabomu katika makao makuu ya chama hicho.

Mapafu yake yalichukua miezi kadhaa kupona kutokana na shambulio hilo ambalo lilifanya mkono wake wa kulia kulemaa kabisa.

Baadaye mwaka huo huo, akawa mgombea wa urais wa Iran.

Ayatollah Khomeini alilidhibiti baraza lililoamua nani angesimama, na Ali Khamenei alishinda kwa 97% ya kura.

Hotuba ya kuapishwa ya Khamenei ilikuwa mwongozo wa urais wake, ukishutumu "mkengeuko, uliberali, na wafuasi wa mrengo wa kushoto waliopendelea Marekani".

Vita vya Iran-Iraq

Nchi jirani ya Iraq iliivamia Iran miezi kadhaa kabla ya uchaguzi.

Rais wa Iraq, Saddam Hussein, alihofia mapinduzi ya Iran yangedhoofisha utawala wake.

Kabla ya kuwa rais, mwanzoni mwa vita Khamenei alitumia miezi kadhaa vitani.

Katika miaka minane ya vita, mamia ya maelfu walipoteza maisha pande zote mbili.

Katika kipindi cha mzozo huo, Iraq ilitumia silaha za kemikali dhidi ya vijiji vya mpakani vya Iran na kushambulia miji ya mbali ikiwemo Tehran kwa makombora.

Vita hivyo vilifanya Khamenei kuendelea kutoiamini Marekani, ambayo iliunga mkono Iraq.

Kiongozi Mkuu

Mnamo mwaka 1989, Ayatollah Khomeini alikufa, na Baraza la Wataalamu wa Uongozi likamchagua Khamenei kuwa mrithi wake.

Kiongozi huyu mkuu mpya alionekana na wengine kuwa na rekodi dhaifu katika masomo ya kidini.

"Mimi ni mtu mwenye makosa na mapungufu mengi, na kwa kweli ni mwalimu wa kidini mwenye elimu kidogo sana," alikiri katika hotuba yake ya kwanza ofisini.

"Hata hivyo, nimepewa jukumu na nitatumia uwezo wangu wote na imani yangu yote kwa Mwenyezi kuweza kubeba jukumu hili zito."

Kwa kukosa heshima kwa viongozi wakuu wa kidini na umaarufu wa Khomeini, Khamenei aliishi kwa tahadhari.

Lakini baadaye alianzisha mitandao ya waliomtii katika mahakama, polisi, vyombo vya habari, viongozi wa kidini, bunge, kikosi cha Revolutionary Guards na vyombo vya kijasusi.

Karim Sadjadpour, mwenzake katika Shirika la Carnegie kwa ajili ya Amani ya Kimataifa mjini Washington, aliiambia BBC News kwamba uwezo wa Khamenei unategemea "kundi lililoshikamana la viongozi wa kidini wenye msimamo mkali na vikosi vya Ulinzi vya Revolutionary".

Vyombo vya habari vya serikali ya Irani vilimuonyesha kama aliyeishi kwa shida huko Tehran na mke wake, watoto na wajukuu.

Alizuia maandamano

Hadi kifo chake, Khamenei ameshutumiwa kikandamiza upinzani.

Mnamo mwaka 1999, alisitisha maandamano ya wanafunzi.

Muongo mmoja baadaye, walioandamana kupinga uchaguzi wakidai kuwa uliibiwa walinyunyiziwa pilipili, kupigwa na kufyatuliwa risasi.

Mnamo mwaka wa 2019, kuongezeka kwa bei ya mafuta kulisababisha maandamano ya barabarani, na mamlaka ikaminya mtandao.

Shirika la Amnesty International linasema polisi waliwafyatulia risasi waandamanaji hadi kufa.

Wanawake wanaofanya kampeni dhidi ya uvaaji hijab waliteswa na kuwekwa katika kizuizi cha faragha.

Mwanasheria mmoja wa kike wa haki za binadamu alihukumiwa kifungo cha miaka 38 jela na kuchapwa viboko 148.

Mnamo mwaka 2022, alikumbana na changamoto kubwa kufuatia kifo cha Mahsa Amini akiwa chini ya ulinzi - mwanamke wa Kikurdi mwenye umri wa miaka 22 alikamatwa kwa kukataa kuvaa hijabu.

Shirika la Habari la Wanaharakati wa Kutetea Haki za Kibinadamu la Iran (HRANA) lenye makao yake makuu nchini Marekani limesema lilipokea majina ya zaidi ya watu 400 waliouawa katika maandamano yaliyofuata.

Katika msimu wa baridi wa 2025-26, kulitokea mfululizo wa maandamano ya mitaani nchini Iran, yaliyosababishwa na kuzorota kwa uchumi.

Mamlaka zilianzisha kamata kamata ya watu. Khamenei alikiri kuwa maelfu ya watu waliuawa, lakini aliwashutumu maadui kwa kuandaa ghasia.

"Wale wanaohusishwa na Israel na Marekani walisababisha uharibifu mkubwa na kuua maelfu ya watu kadhaa," alisema na kuongeza kuwa walichochea machafuko. "Walifanya uhalifu na kosa kubwa," Khamenei alisema.

Shirika la HRANA limesema serikali ilivyojibu ilijumuisha "utumiaji nguvu kwa kukusudia kuua".

Iliripoti kwamba zaidi ya watu 7,000 waliuawa, wengi wao wakiwa waandamanaji, na zaidi ya watu 200 kati ya wale waliokufa walikuwa "wajeshi na vikosi vya serikali".

Marufuku ya chanjo ya Corona

Uchunguzi wa mwaka 2022 uliofanywa na BBC News Persian ulikadiria kuwa ugonjwa wa corona uliua watu 300,000 nchini Iran wakati wa janga hilo - zaidi ya mara mbili ya idadi rasmi ya vifo wakati huo.

Bila kutoa ushahidi, Khamenei alidai, "Inasemekana kwamba sehemu moja ya virusi hivi imeundwa mahsusi kwa ajili ya Iran, kwa kutumia maarifa ya maumbile ya Kiirani".

Wakati usambazaji wa chanjo ulimwenguni ulipoanza - ukiongozwa na kampuni za dawa za Marekani na Ulaya - alipiga marufuku uagizaji wa chanjo za Marekani na Uingereza.

Ripoti za baadaye zilisema yeye binafsi alidungwa moja ya chanjo kadhaa zilizotengenezwa na Irani.

Kupinga Marekani

Muda mfupi baada ya mapinduzi ya mwaka 1979, wanafunzi wa chuo kikuu watiifu kwa Khomeini waliukalia ubalozi wa Marekani, wakiwachukua mateka wanadiplomasia na wafanyakazi katika maandamano ya Marekani.

Utekaji nyara huo ulidumu kwa siku 444 na ulisaidia kuweka msimamo dhidi ya Marekani na Magharibi kama sera rasmi ya serikali.

Baada ya mashambulizi ya Septemba 11 nchini Marekani, Rais Bush aliitaja Iran katika kile alichodai ni 'Taifa lenye kufadhili ugaidi'.

Iran iliunga mkono Hezbollah - kundi la Shia lenye silaha huko Lebanon - kama mshirika wake katika mzozo ambao umesalia kidogo tu uendelee na kuwa wa kudumu na Israeli.

Khamenei aliikosoa Marekani, lakini sera zake hazikuidhinisha wala kuzikabili Marekani moja kwa moja.

Mpango wa Nyuklia

Khamenei alizitaja silaha za nyuklia kuwa si za Kiislamu na mwaka 2003 alitoa fatwa (tafsiri ya sheria za Kiislamu) dhidi ya kuzitengeneza.

Hata hivyo, Israel na nchi za Magharibi ziliamini kwamba, wakati Mahmoud Ahmadinejad alikuwa rais, Iran ilikuwa na nishati ya nyuklia na mipango ya kisasa ya makombora kama kitu cha kuficha uwezo wa silaha za nyuklia.

Vikwazo vilivyofuata vilifanya Iran kuwa nchi masikini.

Mnamo mwaka wa 2015, Iran, Marekani, Uingereza, Ufaransa, Uchina, Urusi na Ujerumani zilifikia makubaliano ya kuzuia urutubishaji wa madini ya Urani nchini Iran.

Hata hivyo, Donald Trump alijiondoa wakati wa urais wake wa kwanza wa Marekani akiuita mkataba huo "uongo mkubwa kwamba utawala wa mauaji ulitamani mpango wa amani wa nishati ya nyuklia."

Iran ilisisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ulikuwa wa amani, na kwamba Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki limethibitisha ushirikiano wake.

Rais wa zamani wa Marekani Barrack Obama, ambaye alitia saini mkataba huo, aliandika mkataba huo "unafanya kazi".

Ufaransa, Ujerumani na Uingereza zilisema "zinajutia" uamuzi wa Marekani.

Wakati urais wa kwanza wa Trump ukikaribia, Marekani ilimuua afisa mkuu wa kikosi cha Revolutionary Guard Qasem Soleimani. Khamenei aliapa kulipiza kisasi, akijiweka karibu na Urusi na Uchina.

Mnamo mwaka wa 2025, Israel ilichukua hatua za kijeshi dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran, na kuwauwa wanasayansi, wanajeshi na maafisa wa ngazi za juu, ikiwa ni pamoja na kutekeleza mashambulizi yanayoongezeka katika maeneo ya makazi.

Iran ililipiza kisasi kwa kurusha makombora dhidi ya Israel.

Marekani ilipojiunga na mashambulizi ya Israel, Khamenei aliapa kutojisalimisha, lakini alionekana dhaifu.

Tarehe 28 Februari 2026, Marekani na Israel kwa pamoja zilianzisha mashambulizi ya anga dhidi ya Iran. Trump alihalalisha mashambulizi hayo, akisema Iran "kamwe haiwezi kuwa na silaha ya nyuklia".

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alisema hatua hiyo ni kuondoa 'tishio lililopo' linalosababishwa na Iran.

Israel ilisema Iran ilianzisha mashambulizi ya kulipiza kisasi huko, huku milipuko ikitokea katika mataifa kadhaa ya Ghuba.

Khamenei ametawala siasa za Iran, akionyesha udhibiti na mara nyingi kulitokea ukatili kwa waliokuwa madarakani.

Wakati fulani, Kiongozi Mkuu alijidhihirisha kuwa karibu juu ya siasa - akidharau ugomvi kati ya wanamageuzi na wahafidhina.

Lakini mara chache Ayatollah Khamenei aliruhusu upinzani kwa sera ambazo alikataa kuendeleza.

Maisha ya Iran yanatawaliwa na sheria alizoziweka. Ni wachache sana wanaoweza kusema ni mabadiliko gani yatarajiwe.

Imetafsiriwa na Asha Juma na kuhaririwa na Ambia Hirsi