Jinsi biashara ya ngono inavyowawinda wakimbizi wa Ukraine

Wiki tano baada ya uvamizi wa kikatili wa Urusi nchini Ukraine, embu tafakari jinsi watu walivyokuwa wakiishi kwa hofu huko.
Mabomu, umwagaji damu, kiwewe.
Hakuna shule kwa watoto wako, hakuna huduma za afya kwa wazazi wako, hakuna paa lililokuwa salama juu ya kichwa chako katika sehemu nyingi za nchi.
Je, ungejaribu kukimbia? Waukraine milioni kumi walikimbia makazi yao, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Wengi hutafuta kimbilio katika maeneo mengine ya Ukraine, yanayoaminika kuwa salama zaidi. Lakini zaidi ya watu milioni tatu na nusu wametorokea mpakani.
Hao haswa wakiwa ni wanawake na watoto, kwani wanaume walio na umri wa chini ya miaka 60 walilazimishwa na serikali ya Ukraine kubaki na kupigania nchi yao.
Wakiwa wamehama makazi yao na wamechanganyikiwa, mara nyingi bila kujua waende wapi, wakimbizi wanalazimika kuweka imani yao kwa wageni au watu wasiowafahamu.
Machafuko ya vita sasa yapo nyuma yao, lakini ukweli ni kwamba, hawako salama kabisa nje ya Ukraine pia.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alionya kwenye Twitter kwamba: "Kwa waharibifu na walanguzi wa binadamu, vita vya Ukraine si janga." "Ni fursa - na wanawake na watoto ndio walengwa."
Mashirika ya biashara haramu yanajulikana sana nchini Ukraine na nchi jirani katika wakati wa amani. Ukungu wa vita ni kifuniko kamili cha kuongeza biashara.
Karolina Wierzbińska, mratibu katika Homo Faber, shirika la haki za binadamu lililoko Lublin, aliniambia watoto walikuwa na wasiwasi mkubwa.
Vijana wengi walikuwa wakisafiri nje ya Ukraine bila kusindikizwa, alisema.
Michakato ya usajili ambayo ilikuwa na mvuto nchini Poland na maeneo mengine ya mpakani - hasa mwanzoni mwa vita - ilisababisha watoto kutoweka, na wasijulikane walipo mpaka sasa.
Mimi na wenzangu tulielekea kwenye mpaka wa Poland na Ukraine ili kushuhudia.
Katika kituo cha treni, kinachojulikana sana kwa kusaidia wakimbizi, tulipata shughuli nyingi zikiendelea. Wanawake walioonekana kupigwa na butwaa na watoto waliokuwa wakilia walikuwa wamezunguka pande zote.

Wengi walikuwa wakifarijiwa na kupewa chakula cha moto kutoka kwenye vyungu vya kupikia vya ukubwa wa viwandani na jeshi la watu waliojitolea.
Kufikia sasa, kuna mpangilio mzuri? ingawa sio kikamilifu.
Tulikutana na Margherita Husmanov, mkimbizi wa Ukraine kutoka Kyiv mwenye umri wa miaka 20. Alifika mpakani wiki mbili zilizopita, lakini aliamua kubaki, kusaidia kuwazuia wakimbizi wenzake kuangukia katika mikono isiyofaa.
Nilimuuliza ikiwa anahisi hatari. Alijibu "Ndiyo," "Hiyo ndiyo sababu nina wasiwasi juu ya usalama wao.
"Wanawake na watoto wanakuja hapa kutoka kwenye vita vya kutisha. Hawazungumzi lugha ya Poland wala Kiingereza. Hawajui kinachoendelea na wanaamini kile anachoambiwa na mtu yeyote.
"Mtu yeyote anaweza kufika kwenye kituo hiki, siku ya kwanza nilipojitolea tuliona wanaume watatu kutoka Italia, walikuwa wakitafuta wanawake warembo wa kuwauza kwenye biashara ya ngono.
"Niliita polisi na ikawa nilikuwa sahihi. Hali ni kutisha."

Margherita anasema maafisa wa eneo hilo wamejipanga zaidi sasa.
Polisi wanashika doria kituoni mara kwa mara. Watu (haswa wanaume, tunaambiwa) walio kwenye maeneo yenye vishawishi, ni waliopo katika wiki kadhaa za kwanza za kuwasili kwa wakimbizi, wametoweka kwa kiasi kikubwa.
Lakini kama tunavyojua kutoka kwa vyanzo kadhaa, watu wengine wenye nia mbaya sasa wanajifanya kama watu wa kujitolea waliovaa mavazi ya watu wakujitolea.
Elena Moskvitina alizungumza kwenye Facebook ili kutoa elimu. Sasa yuko Denmark akiwa salama, kwa hivyo tulizungumza kwa muda mrefu kupitia Skype, hali ambayo alipitia.
Yeye na watoto wake walivuka hadi nchi jirani ya Rumania kutoka Ukraine iliyokumbwa na vita.
Walikuwa wakitafuta lifti mbali na mpaka.
Alichoeleza kuwa wafanyakazi bandia wa kujitolea katika kituo cha wakimbizi waliuliza alikokuwa akiishi.
Walifika baadaye mchana na kumwambia kwa ukali kwamba Uswizi ndio mahali pazuri pa kwenda na kwamba wangempa lifti huko, gari likiwa limejaa wanawake wengine.
Elena aliniambia wanaume walimtazama yeye na binti yake "kwa upole". Binti yake alifadhaika.
Wakamwomba awaoneshe mwanae aliyekuwa kwenye chumba kingine.
Walimtazama juu na chini, alisema. Kisha wakasisitiza asafiri na hakuna mtu mwingine isipokuwa wao, na walikasirika alipoomba kuona vitambulisho vyao.
Ili kuwakimbia wanaume hao kutoka kwa familia yake, Yelena aliahidi kukutana nao wakati wanawake wengine walipokuwa kwenye gari lao. Lakini walipotoka tu, aliniambia, akawashika watoto wake na kukimbia.

Elżbieta Jarmulska, mjasiriamali ambaye ni mchangamfu kutoka Poland, ndiye mwanzilishi wa Mpango wa Women Take The Wheel. Lengo lake, anasema, ni kuwapa wakimbizi wa Kiukreni "usafiri wa usalama".
"Wanawake hao wamepitia mambo mengi tayari, wakitembea au kuendesha gari kwenye eneo la vita na kisha wanakabiliwa na hofu na unyonyaji hapa? Sina namna ya kuelezea maumivu yao," anasema.
Kufikia sasa, ameajiri zaidi ya "wanawake 650 wa Poland, kama anavyowaelezea, wakiendesha gari hadi mpaka wa Poland na Ukraine, ili kuwapa wakimbizi usafiri salama.
Ninaandamana na Elżbieta, anayejulikana zaidi kama Ela, hadi kituo cha wakimbizi ambapo anasisitiza kuonesha kitambulisho chake na uthibitisho wa makazi yake kwa maafisa, kabla hajauliza kama kuna mtu anataka lifti hadi Warsaw.
Gari lake lilikuwa limejaa kwa muda mfupi. Abiria: mkimbizi Nadia na watoto wake watatu.
Ela aliiweka familia hiyo katika gari lake lililojaa vitu, akiwapa watoto wadogo maji, chokoleti na tembe za maumivu wa mwendo ikiwa wangehitaji.

Nadia, wakati huohuo, aliniambia juu ya safari yake ya hatari kutoka Ukraine katika mji wa Kharkiv.
Sasa huko Poland, alifarijika sana, alisema, kuwa na dereva wa kike.
Alikuwa amesikia juu ya hatari za usafirishaji haramu wa binadamu na unyonyaji kwenye redio ya Kiukreni. Lakini aliamua kusafiri tu .
Nyumba yake ilikuwa imepigwa makombora, alisema. Hatari za vita zilikuwa kubwa zaidi.
Ela ina maslahi ya wakimbizi moyoni. Lakini kuacha mpaka salama haimaanishi kuwa hatari imekwisha kwao.
Wengi tuliozungumza nao walitarajia kurudi nyumbani punde tu ghasia hizo zitakapoisha. Lakini kwa siku zijazo, majuma, hata miezi, wanahitaji mahali pa kulala, kula, kupeleka watoto wao shuleni, na pia kazi.
Mahitaji hayo huwafanya wakimbizi kuwa hatarini.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameidhinisha kwa kauli moja hatua ya kufungua soko la ajira, shule na upatikanaji wa huduma za afya kwa watu wa Ukraine, lakini kama mashirika ya kutetea haki za binadamu yanavyoonyesha, wakimbizi wanahitaji msaada ili kusajiliwa na kufahamishwa haki zao.
Mmoja wa wafanyakazi wa kujitolea niliokutana nao kwenye mpaka wa Poland na Ukraine aliniambia kwamba unapokuwa chini na nje, huna urafiki na unahitaji pesa, unaweza kuishia kufanya mambo ambayo hujawahi kufikiria.
Mwanamke huyu alishawishiwa kufanya ukahaba alipokuwa mdogo. Na hiyo, anasema, ni sehemu kubwa ya sababu anasaidia wakimbizi wa Ukraine sasa.
"Nataka kuwalinda. Ili kuwaonya," aliniambia. Aliniuliza nisitangaze jina lake. Tangu wakati huo amebadilisha maisha yake na hataki watoto wake wajue kuhusu maisha yake ya zamani.
Mengi zaidi
- YA MSINGI:Marekani haina mipango ya kuuondoa utawala wa Urusi, asema Blinken
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
- SILAHA:Mzozo wa Ukraine:Makombora ya stinger na silaha nyingine kali zinazotumiwa Ukraine













