Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jamii ya Batwa Uganda:Waliondolewa msituni ili kuwaokoa sokwe
- Author, Patience Atuhaire
- Nafasi, BBC News, Uganda
Wakiwa wameondolewa katika makazi yao ya asili ya msitu miongo mitatu iliyopita katika harakati za kuhifadhi wanyamapori, watu wengi wa Batwa nchini Uganda wanahisi kusalitiwa.
Ukiwa unatembea katika hifadhi ya Kitaifa ya Msitu wa Bwindi, utasikia nyimbo ambazo jamii ya Batwa huimba zinapaswa kuwa za kusherehekea, lakini zinasikika za huzuni sasa.
Wanasifia mavuno mazuri ya asali, lakini hakuna mavuno kwani Wabata hawaruhusiwi tena kukusanya asali, au kitu kingine chochote katika msitu huu.
Badala yake, watu hawa wa kiasili huchukua vikundi vya watalii wanaolipa katika maeneo ya mababu zao na kufanya maonesho ya namna walivyokuwa wakiishi hapo awali.
Mdundo unaochezwa kwenye funguo za chuma za piano, inayojulikana kama "ichyembe", tunapofikia mkusanyiko wa makazi yao dakika 30 tu kufikia kwenye msituni.
"Hili lingekuwa kaburi, ambapo tungewasiliana na babu zetu," Eric Tumuhairwe, kiongozi wa kikundi, anaelezea akionyesha mahali nyuma ya nyumba.
"Wanaume walipotaka kwenda kuwinda walichukua nyama au asali kama sadaka, waliwinda nguruwe-mwitu na aina kadhaa za swala. Wake zao walisherehekea uwindaji mwingi, walipika na kucheza. Lakini hatupati vyakula vya aina hii tena."
Bw Tumuhairwe, ambaye ana umri wa miaka 50 hivi, anakumbuka vizuri maisha kabla ya watu wake kuondolewa.
Kwa karne nyingi waliishi mbali na misitu ya maeneo ya milimani kwenye mpaka wa Uganda, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakiwa wawindaji.
Lakini katika miaka ya 1990, Wabatwa wa Uganda walifukuzwa kutoka kwenye misitu ya Bwindi, Mgahinga na Echuya kusini-magharibi mwa nchi hivyo maeneo hayo yaligeuka kuwa mbuga za wanyama, haswa kwa ajili ya ulinzi wa sokwe adimu wa milimani.
Bw Tumuhairwe anatueleza kuhusu mila za Batwa, ikiwa ni pamoja na uchumba katika eneo ambalo zamani lilikuwa uwanja ambapo vijana wa kiume na wa kike walikuwa wakijumuika na kufurahi.
"Kijana anayetaka kuoa alilazimika kumtega kindi.
"Huwa mnyama ana kasi , kwa hivyo aliweka mtego eneo ambalo alikuwa amelala kwenye shimo la mti.
Anamkamata wakati anaamka na kujaribu kukimbia. Ilibidi amlete hai, vinginevyo hakuwa na mke kwa ajili yake. " anakumbuka kwa kucheka.
Tunapanda juu ya milima ya msituni iliyofunikwa na ukungu, hadi kwenye pango ambalo kuna jumuiya iliyozoea kukusanyika kwa ajili ya ibada.
"Nataka kurejea jinsi tulivyoishi... Kila kitu tulichohitaji, msitu ulitolewa: nyama, matunda, na madawa," anasema Bw Tumuhairwe.
Baada ya kuondolewa, baadhi ya familia za Batwa zilipewa mashamba na serikali. Lakini kwa vile hawakujua jinsi ya kulima, ardhi iliuzwa na wengi walitawanyika katika eneo lote, wakinusurika kwa hisani kutoka kwa majirani na mashirika yasiyo ya serikali.
"Baadhi ya majirani walitudharau, wakituita watu wa msituni," anakumbuka Aida Kehuuzo, ambaye ana umri wa miaka 80 hivi na mwanamke pekee katika kundi la wasafiri.
Ushindi mahakamani
Wakiwa chini ya watu 7,000 nchini Uganda, Wabatwa wengi wamehamia maeneo ya mijini, kama Kisoro, ambayo iko karibu na misitu.
Pembezoni mwa mjini , familia hizi ziko kwenye maeneo ya umma wakiwa wamejijengea nyumba zao kwa maboski na maturubahi.
Jumuiya hiyo ipo pembezoni.
Jitihada za kufanya mahojiano nao ziliambulia patupu, kwani wengi wanahisi kunyonywa na wanasiasa na mashirika na wanachukia watu wasio jamii yao.
"Unakuja hapa kupiga picha na kuziuza. Tunapata faida gani? Sitazungumza nawe usiponilipa," anafoka mwanamke mmoja.
Mwaka 2011, kikundi cha Batwa wakiungwa mkono na mashiŕika yasiyo ya kiseŕikali (NGOs), waliipeleka seŕikali ya Uganda mahakamani kutokana na kufukuzwa kwao- na mwishoni mwa mwaka jana, mahakama ya kikatiba iliamua kuwaunga mkono.
Ilisema jamii imetendewa unyama na kuamuru "fidia ya haki" ilipwe ndani ya miezi 12, lakini serikali inakusudia kukata rufaa.
Baadhi ya Wabatwa, kama Allen Musabyi, wamezoea na kuanza kilimo.
Lakini ardhi ambayo yeye na wengine wachache wanatayarisha kwa ajili ya zao la viazi limekodishwa - linalipwa kwa shirika la misaada la Umoja wa Maendeleo ya Batwa nchini Uganda (UOBDU).
"Kama huna ardhi, huwezi kuendelea, huwezi kuwapeleka watoto shule, huwezi kula.
"Lakini kama ningepewa fursa ya kurudi msituni, ningekimbilia huko," anakiri.
'Wanyama wanathaminiwa zaidi'
Alice Nyamihanda, ambaye anafanya kazi UOBDU na ni mmoja wa wahitimu wachache wa chuo kikuu cha Batwa, anasema jamii inapaswa kupigania usawa.
"Nataka Wabatwa wenzangu wawe kama watu wengine," anasema - na sio kushindia chakula kutoka kwa mapipa ya taka kama ilivyo kawaida huko Kisoro.
"Wanyama wanahudumiwa vizuri kuliko Wabatwa, kwa sababu watalii wakija wanalipa pesa, serikali inatumia pesa hizo, na Wabatwa wanabaki wanateseka."
Wanyama anaowazungumzia ni sokwe wa milimani. Serikali inatoza hadi $700 (£530) ili kufuatilia sokwe.
Juhudi za uhifadhi zimesababisha idadi ya sokwe wa milimani nchini Uganda kuongezeka hadi 459, na zaidi ya 1,000 duniani kote, kumaanisha kwamba hawajaorodheshwa tena kama walio hatarini kutoweka.
Lakini Bi Nyamihanda anashangaa iwapo kunaweza kuwa na njia endelevu zaidi ya kulinda wanyamapori pamoja na haki za jamii ya Batwa.
Mamlaka ya Wanyamapori ya Uganda inasema kuwa inafanya hivi kwa kuwaruhusu Wabatwa kupeleka watalii msituni na sehemu ya tano ya mapato yanayokusanywa kutoka katika mbuga hiyo huenda kwa vijiji vya karibu kupitia serikali ya mtaa.
Kulingana na Sam Mwandha, mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya Wanyamapori Uganda, anasema wananchi - ikiwa ni pamoja na Batwa - wanaweza kuja na mapendekezo ya kufadhiliwa kwa kutumia pesa hizi.
"Wakati jamii ya Wabatwa ikiondolewa msituni, makosa kadhaa yalifanyika. Lakini madai ya kutomiliki ardhi, kutowaruhusu kuwa na utamaduni wao, ni potofu na sio sahihi.
"Tunawaambia, 'Waenda shule wakasome', lakini [pia] tunasema, 'Usisahau utamaduni wako, unaweza kuutumia kupata pesa.'
Bado Wabatwa wanataka mahali pa kuita nyumbani na kutambuliwa kama watu wa kiasili walio hatarini kutoweka ili wawe na ulinzi bora chini ya sheria za kimataifa.
Huku msituni, Bw Tumuhairwe anakiri kwamba elimu na ukulima umekuwa wa manufaa kwa baadhi ya Wabatwa - ingawa anaongeza kuwa hali bado ngumu:
"Lakini unapokuja kufikiria, hilo pia ni kufuta sisi ni nani, tulitoka wapi."