Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Mtanzania anakula mchele kwa pua' -Mtaalamu wa mchele
- Author, Esther Namuhisa
- Nafasi, BBC Swahili
Ni kawaida mteja anapotaka kununua manukato, lazima anuse hata kama ni perfume ambayo huwa anainunua kila mara.
Nchini Tanzania akina mama wengi wanapokwenda sokoni au dukani kununua mchele, lazima waunuse ndio wataridhika kuwa "huu ndio mchele mzuri".
Dr. Zackaria Kanyeka, mtaalamu wa mchele kutoka Kyela, yeye anasema mchele wa Mbeya umepata umaarufu mkubwa kutokana na tabia ya walaji kupenda harufu na ladha ya mchele huo.
Anasema yeye alizaliwa na kusoma katika ardhi ya mpunga, eneo ambalo nchi nzima inafahamu kuwa kuna mchele mzuri.
"Nimeanza kulima mpunga nikiwa nina miaka 6 , mpunga ndio umenilea na kusababisha nipate elimu mpaka ya PHD.
Wakati nasoma elimu ya juu, ulaya…nilikuwa nawaambia wazungu kuwa wao hawali mchele, wanakula mkate hivyo anajua jamii yake inapenda nini?
Elimu yake ya juu yote amesomea mpunga, na kufanyia miradi ya mpunga."
Anasema ameweza kuzalisha mbegu mbalimbali za mpunga.
"Kitu ambacho nilikuwa ninakiangalia sana, ni ule mchele ambao wanaupenda kwa kula na ambao unazaa sana bila kudhurika na wadudu.
Kabla mama hajanunua mchele lazima aunuse, kabla hajanunua atachukua mchele na kusogeza kwenye pua kabla hajaamua ni upi anunue.
Taifa zima linajua kuwa mchele wa Kyela unafahamika nchi nzima kuwa ndio mchele mzuri.
"Mtanzania anakula mchele kwa pua"...Licha ya kwamba mchele una majina mengi lakini wateja wanachozingatia zaidi ni mchele kunukia vizuri.
Gharama ya mchele kuwa juu, inazingatia mchele kunukia pia. Hata maskini anajua kizuri kikoje, ndio maana mchele wa Mbeya umepata umaarufu mkubwa.
Mchele ambao tunautambua kama mpunga ukiwa shambani na wali baada ya kupikwa, huwa una majina tofautitofauti.
Utasikia 'Kula na bwana' hiyo ni aina ya mchele ambao ukipika wali wake lazima majirani wajiulize.
Ni mchele mtamu ambao unapendwa kupikwa maeneo ya pwani, Dar es Salaam na Tanga.
Huwa hauzai kwa wingi ingawa unastahilimi mabadiliko ya hali ya hewa.
Dr. Kanyeka anasema mlaji wa mchele wa Afrika Mashariki anataka kula ubwabwa au mchele ambao ni mzuri, wenye kunukia, mrefu , wenye kung'ara.
"Ukiuangalia unang'aa, mbegu ndefu, nyembamba zenye urefu wa katikati au nene, ambao haukatiki yani ulionyooka.
Haina kitu cheupe ndani, wali ukipikwa unabaki laini hata ukilala na kuliwa kesho yake bado unakuwa laini.
Hivyo , ikiwa mnunuaji wa mchele anataka mchele unukie, mkulima anataka faida pia .
Ingawa kuna mpunga ambao unanukia, na ukiupika unakuwa bokoboko lakini kuna mchele ambao ukipika unakuwa unaachana na huu ndio wataalamu wanautaka, ila kuna mchele pia ambao ukiupika unakaa kama makande.
Huu mchele akina mama wengi huwa wanauita mdundiko.
Na akina mama huwa wanaulizia mchele wa Mbeya wanapofika sokoni kwa sababu ya mchele huo kunukia.
Unaweza kusikia sukari , kilombelo, super, mwarabu na majina mengine mengi ya mchele.
Dr.Kanyeka anasema wanapozalisha mbegu za mpunga , huwa wanafanya utafiti kwa kuwapa watu mbalimbali kama 20 au zaidi na wao ndio watachagua mchele huo kama mzuri au la.
"Huwa tunaupika mchele bila kuweka chumvi, mafuta wala nazi wanaula..Mchele utakaofaulu kwa asilimia 80 ndio unapelekwa kwa wakulimwa.
Mimi nikitafuna mchele najua aina gani ya mbegu ,"Prof.Kanyeka ameeleza.
Zamani., mchele ulikuwa unaonekana kuwa chakula cha kifahari na waafrika walikuwa wanaonekana wanakula ugali huku mchele ukiwa ni wa watu wenye kada ya juu.
Hata shuleni mchele haukuwa chakula kinachopikwa.
Mchele ni rahisi sana kuupika kuliko Ugali. Na sasa kuna mabadiliko mengi katika hili.
Kwa sasa asilimia 60 ya watanzania wanakula wali, uchumi unakua kwa sasa na watu wanahama kutoka vyakula vya asili na kuingia kwenye mchele.
Awali wali ulikuwa unaliwa wakati wa sikukuu kama krismasi au iddi au mwaka mpya.
Ukisikia nyumba imepika mchele ujue ni sikukuu ya jambo Fulani.
Kadiri muda unavyoenda na kipato kinaongezeka na kunakuwa na muingiliano, kumekuwa na mabadilko, Mpaka miaka ya 1970, watanzania walikuwa kilo 14 za mchele kwa mwaka, miaka ya 90; kilo 21.5 kwa mwaka na miaka 2000 kila mtanzania anakula kilo 24 kwa mwaka.
Bilashaka mpaka sasa imefikia kilo 27 kwa mwaka.
Mpunga ni chakula ambacho kililetwa kutoka Asia na wale waliokuwa wanafanya biashara za utumwa.
Mchele ulilimwa zaidi na watu waliotoka Asia.
Mkulima wa kwanza wa mchele nchini Tanzania mnamo 1868 alikuwa mwarabu, aliitwa Nasibu Najumo na mkulima wa kwanza usangu ni Tip Tibu… na Tabora ulipelekwa na mwarabu.
Mpunga unauzwa kwa bei ya juu kuliko mahindi na umepata umaarufu zaidi na uhitaji.
Na mahitaji yataongezeka kwasababu ni chakula na zao la biashara.
Kwa Afrika mashariki na kati,Tanzania inaongoza kwa ukanda huu ukiondoa Madagascar.
Tuna hekta asilimia 42, na kuzalisha asilimia 62 ya unaozalishwa ukanda wote ukiondoa Madagasca., zinazofuata ni Msumbiji, kongo na Uganda.
Dr. Kanyeka amemaliza kwa kusema , Serikali ingewekeza katika mchele ingeongeza mapato kwa kuwa kuna wenzetu hawajajitosheleza katika hili.
Sehemu tuliopo ni eneo zuri sana katika kilimo cha mchele, kuna mataifa mengi yametuzunguka ambayo hayana mpunga wa kutosha.
Umaarufu wa mpunga unaongezeka kila siku kwasababu ni zao la biashara.
Unabadilisha maisha ya watu sana.