Wabunge waidhinisha mtu wa kwanza wa jinsia mbili kufanya kazi ya serikali Kenya, hii inatuma ujumbe gani?

Bunge la Kenya siku ya Jumanne liliweka historia kwa kumuidhinisha mtu wa kwanza mwenye jinsia tofauti kushika nafasi ya juu katika Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu nchini humo.

Dkt Dennis Nyongesa Wamalwa alikiri kuwa na jinsia tofauti aliidhinishwa na wabunge na kumfanya kuwa mtu wa kwanza wa jinsia ya tatu kushika wadhifa wa juu wa umma.

Idhini yake pia inatuma ujumbe wa azimio la nchi kutambua watu wa jinsia ya tatu.

Mhadhiri huyo wa chuo kikuu aliisimulia kamati ya uchunguzi inayoongozwa na Mbunge wa Kangema Muturi Kigano jinsi ambavyo amekabiliwa na ukiukaji wa haki za binadamu kutokana na jinsia yake.

Watu wenye jinsia tofauti ni watu waliozaliwa wakiwa na jinsi zote mbili yaani ya kiume na kike.

Kulingana na sensa ya watu ya mwaka 2019, kuna watu wa jinsia mbili 1,524 wanaotafsiri kuwa asilimia 0.003 ya idadi ya watu.

"Mteule alisema kuwa maono yake ni kuendeleza utamaduni wa kuheshimu haki za binadamu kwa watu wote na kwamba atafanya kazi ili kutekeleza mapendekezo ya kikosi kazi juu ya watu wa jinsia tofauti na ujumuishaji katika mtaala ili kujenga uelewa," ikisoma sehemu ya Sheria na Haki, Ripoti ya Kamati ya Masuala ya Kisheria.

Unaweza pia kusoma:

Nyongesa ni miongoni mwa viongozi wengine wanne walipendekezwa na Rais Uhuru Kenyatta katika KNCHR.

Wanne hao ni Roseline Doreen Adhiambo Odhiambo - Odede (mwenyekiti), Prof Marion Wanjiku Mutugi, Dkt Raymond Plal Sangsang Nyeris na Bi Sara Talaso Bonaya.

Odede aliyekuwa makamu mwenyekiti katika Tume ya Majaji na Hakimu iliyoacha kazi ya Uchunguzi huku Bonaya akiwa mjane wa aliyekuwa waziri wa Baraza la Mawaziri Bonaya Godana.

Katika kupitisha wateule hao, wabunge waliipongeza kamati hiyo kwa kufanya uangalizi na kuhakikisha maslahi ya wachache yanazingatiwa.

Mbunge wa Dagoretti Kusini John Kiarie alisema uteuzi wa Nyongesa ni wa kipekee na udhibitisho kwamba nchi imejitolea kutambua watu wa jinsia ya tatu.

"Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii, mtu aliyekiri kuwa na jinsia tofauti atateuliwa katika tume huru ya kitaifa," Kiarie alisema.

"Kuna kelele zinazoongezeka za kutambuliwa kwa jinsia ya tatu kwa jina la watu wa jinsia tofauti."

"Nyongesa pamoja na kuwa na elimu nzuri pia anawakilisha wachache," Mbunge wa Rarieda Otiende Amolo alisema.

Mbunge wa Homa Bay Opondo Kaluma alisema kuteuliwa kwa Nyongesa ni utambuzi wa kijasiri wa jinsia ya tatu nchini.

"Huyu atakuwa mtu wa kwanza kujiunga na wakala wa serikali wa kiwango hicho," Kaluma alisema.

Wabunge siku ya Jumanne waliidhinisha wateule hao kuwezesha uteuzi wao rasmi na Rais Uhuru Kenyatta.