Afcon Cameroon 2022:Michuano ya soka katika kivuli cha uasi

Kundi linalotarajia kuwa la wanasoka, wakitoka jasho na kuangaza katika harakati zao kwenye joto la alasiri, buti zao zikinyunyiza vumbi kidogo wanapokimbia.

Wanacheza umbali wa kutupa jiwe mbali na mawimbi ya kustaajabisha ya Bahari ya Atlantiki, na kwenye kivuli cha kilele cha pembe tatu cha Mlima Cameroon.

Wamefurahishwa na mji wao wa Limbe kuwa mwenyeji wa mechi za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon). Mashindano ya kimataifa ya kandanda ya bara hilo yanaanza Jumapili.

"Ni furaha kubwa kwetu sisi Wacameroon. Itakuwa furaha kuwakaribisha watu kutoka mataifa mengine kwa ajili ya mashindano haya makubwa," anasema Erik.

Frederick, ambaye anacheza kama golikipa katika moja ya timu bora huko Limbe, anasema hawezi kusubiri kuona nyota wa Ligi Kuu kama vile Mohamed Salah wa Misri na Sadio Mane wa Senegal.

Mpaka sasa ameweza kuangalia kwenye runinga tu.

"Labda ningezungumza nao, niwasalimie. Ningefurahi sana."

Limbe ndio jiji pekee nchini Cameroon ambako wanazungumza lugha ya Kiingereza na ndio michuano ya soka ya Afrika yatafanyika.

Kwa takriban miaka mitano, Cameroon imesambaratishwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Cameroon ilitawaliwa na Wafaransa na Waingereza, na urithi huo wa kikoloni uliacha mgawanyiko wa lugha.

Kwa miongo kadhaa baada ya kupata uhuru kutoka kwa Waingereza walilalamika kuwa wametengwa, huku mamlaka ya kisiasa na kiuchumi yakiwa mikononi mwa walio wengi wanaozungumza Kifaransa.

Mwaka 2016 wanasheria na walimu waliongoza vuguvugu la maandamano ya amani kwa upande wa wale wanaozungumza lugha ya Kiingereza Cameroon. Wengi walikamatwa na kuwekwa ndani kwa miezi michache eneo hilo lilikuwa kwenye vita.

'Kuzimu ya duniani'

Hakuna anayejua haswa ni watu wangapi walikufa, ingawa vikundi vinavyotaka kujitenga na vikosi vya serikali vimeshutumiwa kwa ukatili.

Zaidi ya watu milioni moja wamelazimika kukimbia makazi yao.

"Ilikuwa kama kuzimu ya duniani," anasema Akame Kingsly Ngolle, ambaye alikuwa ana shule huko Munyenge - kaskazini mwa Limbe - lakini alilazimika kukimbia wakati risasi zilipokuwa zikipigwa.

"Kama mtu binafsi kila kitu nilichokuwa nacho kiliteketezwa, nyumba yangu na kila kitu kingine."

Walimu wengi na wanafunzi walifika Limbe pia, na shule inaendesha shughuli zake tena, ingawa katika majengo ya kukodi.

Kuta za mbao kwenye ghorofa ya chini ya jengo la ghorofa tatu huifanya kujisikia kama suluhisho la muda.

Walimu hao wanapaswa kukabiliana na matatizo mengi, ikiwa ni pamoja na wanafunzi ambao wamekosa masomo kwa miaka mingi.

Hakuna mtu anayeenda shule - au hufanya chochote - hata Jumatatu.

Limbe inageuzwa kuwa kile kinachojulikana hapa kama "mji wa mizimu" wakati huo, kwa sababu ya vitisho vya vikundi vinavyotaka kujitenga kushambulia mtu yeyote anayekwenda kazini au shuleni.

Kwingineko katika mkoa huo shule zimeshambuliwa, wanafunzi na walimu kuuawa.

Hiyo sio yote.

Augustine Akwa anafurahi kupata mahali salama huko Limbe, lakini anasema yeye na wanafunzi wengine wengi waliohamishwa wanatatizika kutafuta riziki:

"Kununua vitabu ni vigumu, hata kupata chakula cha kutosha. Haya ndiyo magumu tunayokabiliana nayo."

Haijamzuia kuendelea na masomo yake, na ana ndoto ya kuwa mhandisi wa petroli ili aweze kuhudumia familia yake.

Nilipata azimio kama hilo la kuboresha maisha yao katika watu wengi waliohama niliokutana nao huko Limbe.

Mfano mwingine ni Ringnyu Lovetta Ngala aliyeanzisha huduma ya kusafisha neema ya Mungu, ili kuwapa watu waliohamishwa makazi yao kama vile kazi yake ya kusafisha, kufua nguo, kupalilia, kilimo na huduma nyingine.

Katika mwezi mzuri, watu wanaweza kupata zaidi ya $40 (£30) - si nyingi, pengine, lakini za kutosha kulipa ada na kulipa kodi ya nyumba.

Wengi wanatumaini kuwa Afcon inaweza kuleta mabadiliko kidogo kutokana na mihangaiko yao ya kila siku.

Sio tu wale waliohamishwa na mzozo wa Anglophone ambao wanahisi athari zake.

Katika fukwe za hoteli ya Sema - jengo kuu kuu lililo kando ya bahari, na uwanja wa mpira wa vikapu na mpira wa wavu majini - wamelazimika kuachisha kazi 80% ya wafanyikazi wao katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na janga la Covid.

Afcon inaweza kuleta wadau na mashabiki wengi hotelini na kuongeza soko , lakini nini kitatokea baada ya michuano hiyo?

Na pia kuna swali la kama ni hatari kuwa na michezo huko Limbe.

Wanaojitenga hawataki mashindano hayo yafanyike hapa, na wametishia kuyavuruga.

Usalama ulioimarishwa

Afisa mkuu, Engamba Emmanuel Ledoux, anakiri kuwa bomu lililipuka wiki iliyopita - ingawa hakuna mtu aliyejeruhiwa - lakini anasema mamlaka itaweka timu na mashabiki salama kabisa wakati wa mashindano.

Kama sehemu ya juhudi hizo, askari wenye silaha nzito - wameonekana wakishika doria katika mitaa ya Limbe.

Felix Agbor Balla, mwanasheria na mwanaharakati wa haki za binadamu, ambaye alikuwa mmoja wa sauti maarufu dhidi ya kutengwa katika awamu ya amani ya mapambano, anaamini kuwa serikali na wanaotaka kujitenga wanakosa mbinu.

Anasema wanaotaka kujitenga wanapaswa kutangaza kusitisha mapigano katika mashindano hayo, na serikali inapaswa kuwaachilia wafungwa, akiwemo kiongozi anayetaka kujitenga Ayuk Tabe.

Kufikia sasa inaonekana dalili ndogo ya hilo kutokea - na dalili ndogo kwamba pande hizo mbili zinaaminiana vya kutosha kushiriki katika aina ya mijadala yenye maana inayohitajika kumaliza mzozo huo.

Wanaharakati kama Esther Njomo Omam wanasisitiza kwamba wakati wanaume wanapigana ni wanawake na watoto wanaoteseka zaidi.

Mamlaka zinatumani Afcon inaweza kuleta watu pamoja, na hata wale wanaoishuku serikali kuu wanaweza kwenda uwanja wa Limbe kuwaona nyota wa soka barani humo.

Itachukua mengi zaidi ya hayo, ingawa, kuponya majeraha ya miaka michache iliyopita.

Urithi wa kipekee wa kikoloni nchini Cameroon

• Ilitawaliwa na Ujerumani mwaka 1884

• Wanajeshi wa Uingereza na Ufaransa waliwalazimisha Wajerumani kuondoka mwaka wa 1916

• Cameroon imegawanywa miaka mitatu baadaye - 80% inaenda kwa Wafaransa na 20% kwa Waingereza

• Cameroon inayomilikiwa na Ufaransa ilikuwa huru mwaka 1960

• Baada ya kura ya maoni ya 1961, eneo la Uingereza liligawanywa.

Kusini mwa Cameroon walipiga kura kujiunga na Cameroon, huku Cameroon Kaskazini wakijiunga na Nigeria inayozungumza Kiingereza.