Uganda Coalition for Forces of Change : Kundi la waasi lililokiri 'kupindua serikali'

- Author, Isaac Mumena
- Nafasi, BBC Uganda
Polisi wa Uganda wanasema kundi jipya la waasi linalojulikana kwa jina la Uganda Coalition for Forces of Change limeundwa nchini Uganda na kwamba hadi sasa wamewauwa maafisa 4 wa polisi na kuiba bunduki nne.
Operesheni iliyoendeshwa jana imefanikisha kukamatwa kwa washukiwa nane na kupatikana kwa bunduki mbili katika wilaya ya Kasanda kilometer 102 magharibi ya Jiji la Kampala.
Msemaji wa Polisi Fred Enanga anasema kuwa kundi hilo limekiri kuwa dhamira yao ni kupindua Serikali.
Hata hivyo anasema uchunguzi unaendelea ili kujua waanzilishi halisi wa kundi hilo jipya la waasi ni akina nani.

Chanzo cha picha, ISLAMIC STATE PROPAGANDA
"Hadi sasa tumewakamata washukiwa 8 ambao ni wanachama wa kundi jipya la waasi linalojulikana kama Muungano wa vikosi vya Uganda kwa ajili ya mabadiliko.
Katika mashambulizi waliyofanya, maafisa wanne wa polisi waliuawa na bunduki zao kuchukuliwa.
Wamekiri kuwa mashambulizi dhidi ya polisi ni mkakati wa kupata bunduki na kulidhoofisha jeshi la polisi ambalo linaonekana kuwa kikwazo cha azma yao ya kubadilisha Serikali.
Tumefanikiwa kupata bunduki 2 na risasi 22.
Tutafanya uchunguzi mpana zaidi ili kujua ni viongozi gani wako nyuma ya kundi hili jipya na vitendo vyao vya uvunjaji sheria"














