Barwan Salum: Nimekuwa mfano hai katika taifa langu

m

Chanzo cha picha, Barwani

    • Author, Esther Namuhisa
    • Nafasi, BBC Swahili

Tanzania ni taifa ambalo katika miaka ya hivi karibuni lilikumbwa na mauaji makubwa ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) haswa kipindi cha uchaguzi kilipokuwa kinakaribia.

Licha ya matukio hayo mwaka 2010, historia iliandikwa na bwana Barwan Salum baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Lindi, kusini mwa Tanzania.

Barwan amekuwa mbunge pekee albino kuchaguliwa na wananchi nchini Tanzania na hata Afrika Mashariki.

Miaka miwili kabla ya kuchaguliwa kwake, mwaka 2008, rais wa Tanzania wa wakati huo Jakaya Kikwete alimteua mbunge wa kwanza albino Al-Shymaa Kway-Geer wakati nchi jirani ya Malawi, imeshuhudia uteuzi wa albino wa kwanza kuwa mbunge Novemba 4, mwaka huu.

Vilevile , Issac Mwaura ni mtu wa kwanza mwenye ulemavu wa ngozi kuwahi kuwa seneta nchini Kenya.

Kampeni nyingi zilizofanyika Tanzania dhidi ya watu wenye ualbino , zimeweza kubadili mitazamo ya wengi.

Zamani, jamii hii ya watu wenye ulemavu wa ngozi waliitwa 'zeruzeru' lakini miaka ya hivi karibuni jina hilo halitumiki sana katika jamii, na hasa katika majukwaa ya umma.

n

Chanzo cha picha, Barwani

Kwa jinsi hali ilivyokuwa ya kutisha kwa watu wenye ualbino nchini Tanzania, halikuwa jambo la kawaida kwa mtu mwenye ualbino kujitokeza hadharani kwenye majukwaa huku akijua fika watu wa aina yake wanasakwa.

Mauji ya albino yalishamiri huku kukiwa na imani potofu kwa baadhi ya watu wakiamini kuwa wakipata viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi watapata utajiri.

Barwan anautaja ushindi wake kuwa wa watu wote wenye ualbino. " Nimekuwa mfano hai katika taifa langu kuwa albino aliyeweza kuongoza na hata tunajivunia kuwa tumeweza kuwa na waziri ambaye sasa ni balozi, huu ni ushindi mkubwa kwetu,"Baruani anaeleza.

M

"Wakati ule mimi nazaliwa, ukizaliwa mlemavu waliona kama laana hivi, watu wengi hawakutuchukulia kama watu wa kawaida kutokana na ngozi zetu, lakini sasa watu wana elimu ya kibaolojia kuhusu sisi, nilipokuwa nasoma wanafunzi wenzangu walikuwa wakinitenga hawakutaka kushirikiana na mimi.

Zamani , Wengi waliamini mwisho wa maisha ya albino ni miaka 20 mpaka 25 ,Lakini pia wazazi na walezi hawakuwa na uwezo mkubwa wa kututunza hasa adui yetu mkubwa sana ni mwanga wa jua ambao unaathiri sana ngozi zetu." Barwan anasimulia.

Kuna umuhimu gani kwa yeye kuwa kiongozi

M

Chanzo cha picha, CUF

Barwani anasema kulikuwa na umuhimu wa yeye kuwa kiongozi wa kisiasa kwa wakati ule , kwa kuwa nafasi ya watu wenye ulemavu katika chama kimoja haikuwepo hivyo mara baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 fursa iliongezeka.

Aliwania nafasi ya ubunge mara tatu ambapo mwaka 2000 na mwaka 2005 hakufanikiwa na kufanikiwa ushindi mwaka 2010.

"Nilikuwa mbunge wa kwanza sio Tanzania tu hata Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla kupata ubunge kwa kuchaguliwa na wananchi wenyewe katika sanduku la wapiga kura.

Niljiona ninao uwezo wa kuwa mbunge, hotuba zangu ziliwavutia watu wengi, niliona nisiishie kwenye mikutano ya kisiasa nikaona kuna haja sasa ya kwenda katika bunge na kutunga sheria ili kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanapata haki zao.

Wakati anapata nafasi hiyo walemavu walikuwa watu wa daraja la chini zaidi katika kupata elimu ya kutosha, kupata ajira za maofisini, watu walikuwa wanauliza je tukimpa kazi anaweza?

Lakini niliweza kufungua milango kwa namna moja au nyingine", Barwani anaeleza.

Je alikuwa hana hofu ya maisha yake?

Taarifa zilivyozidi kumiminika juu ya ongezeko la mauaji ya albino ilibidi serikali impatie ulinzi wa karibu kwa ajili ya usalama wake.

"Watu wangu wa karibu walikuwa wanapata shida kujua usalama wangu upo vipi lakini pia ilifika mahali uongozi wa serikali uliokuwa karibu ilikuwa ni lazima waangalie usalama wangu uko vipi kwa kuwa hakukuwa na utulivu wala amani ya kutosha wakati wote kulikuwa na wasiwasi."

Je kuwa albino, kulichangia ushindi wake?

Barwani

Chanzo cha picha, Barwani Salum

"Watu wengi walistaajabu na kuona kama siwezi na nilikuwa na upinzani mkubwa sana hasa kwenye chama kinachotawala wakatumia hiyo nafasi kuwaambia kuwa huyu hawezi kwamba haijawai tokea hata mara moja na nyie watu wa hili jimbo hamna watu wanaoweza kwenda bungeni zaidi ya huyu yalikuwa maswali ya uchochezi ambayo watawala walikuwa wanawaambia wapiga kura kwamba mimi sipaswi kushika nafasi hiyo bora watafute mtu mwingine yoyote sio mimi.

Vyama vya watu wenye ulemavu vilishirikiana nami kuwaondoa watu mashaka ambayo wananchi walikuwa nayo.

Hata hivyo Barwani anasema wakati ule kulikuwa kuna hitaji la mtu mwenye asili ya ualbino kuepo bungeni ili kuweza kueleza changamoto zao badala ya kusemewa na watu wengine.

Maelezo ya sauti, World Albinism Day: Babangu alisema hawezi kumlea mtoto ‘anayefanana na nguruwe’

Furaha ya ushindi

Ilikuwa furaha isiyo na kifani, watu wa jimbo langu la Lindi , wengi walikuja toka maeneo mbalimbali duniani kuja kuangalia ni watu wa namna gani wakati watu wenye ulemavu wa ngozi wanauwawa, wanakatwa viungo lakini watu wake wameamua kumchagua mtu wa aina ile ile na kumpeleka katika jumba la kutunga sheria iliwastaajabisha watu wengi na watu wa Lindi walionekana majasiri hivyo hii sio furaha yangu mimi tu hata wananchi wa Lindi walijawa na furaha.

Walemavu wengi walikuwa hawathubutu walikuwa hawawezi na hata vyama vyao vilikuwa haviwezi kufanya hivyo kuwapeleka mbele lakini kuingia kwangu kwenye siasa na kuwa mbunge kulifungua mlango kwa watu wengi kuja kugombea lakini kwa bahati mbaya mpaka leo bado hakuna mlemavu wa ngozi katika Afrika amevunja rekodi hii ya kwangu.