Siku ya Ualbino:Watu wenye ulemavu wa ngozi bado wanapitia changamoto nyingi maishani

ISAAC MWAURA

Chanzo cha picha, ISAAC MWAURA

Muda wa kusoma: Dakika 4

Watu wenye ulamavu wa ngozi bado wanapitia changamoto nyingi maishani licha ya kuwa wamepiga hatua kubwa kuhakikisha kwamba pana usawa na pia wanajihusisha na shughuli za kujenga jamii na nchi .

Katika siku hii ya kuadhimisha ulemavu wa ngozi duniani ,kauli mbiu ni kutambua mchango na ukakamavu wa watu wenye ulamavu wa ngozi kwamba wana uwezo kama watu wengine .

Kuna wengi wanaofahamu safari na changamoto za watu wenye ulamavu wa ngozi lakini simulizi ya Isaac Mwaura- anayeishi na ulemavu huo na amekuwa mstari wa mbele kuyatetea maslahi ya watu wenye hali hiyo sio tu nchini Kenya bali kote barani Afrika .

Mwaura ni mtu wa kwanza mwenye ulemavu wa ngozi kuwa mbunge na seneta nchini Kenya na safari yake ya maisha binafsi inasimulia kile ambacho wengi katika hali yake hupitia lakini ni miongoni mwa wachache waliofika kilele cha matamanio yao hasa katika ulingo wa siasa .

Maelezo ya sauti, World Albinism Day: Babangu alisema hawezi kumlea mtoto ‘anayefanana na nguruwe’

Haijakuwa rahisi

Mwaura ,mzaliwa wa Kiambu nchini Kenya anasema tangia akiwa mdogo alitamani sana kuwa mwanasiasa na ndoto yake hiyo haikuwa rahisi kwasababu ya hali yake ya ualbino.

Hata hivyo ukakamavu wake na sifa zake za uongozi ,anasema zilianza kudhihirika akiwa shuleni .

'Sikupenda kamwe kuona mtu akidhulumiwa,ningechukua hatua ili kuzuia mateso ya mtu yeyote' anasema

Msimamo wake huo kuhusu haki na usawa uliendelea hata alipoanza kazi ya uanaharakati kuwatetea watu walemavu wakati alipoteuliwa kuijunga na bodi ya kitaifa ya watu wenye ulemavu akiwa na umri wa miaka 22 .

iSAAC MWAURA

Chanzo cha picha, iSAAC MWAURA

Hatua hiyo ilimpa nguvu kujiamii kwamba siku moja angeweza kutimiza ndoto yake kuwa mbunge na baadaye aliweza kuteuliwa kuwa mbunge maalum kuwaakilisha watu wenye ulemavu .

Hakukomea hapo kwani baadaye aliteuliwa tena kuwa Seneta kuwaakilisha watu hao katika bunge la seneti na kuwa mtu wa kwanza Kenya mwenye ulemavu wa ngozi kupanda ili kuzishikilia nafasi hizo mbili .

Kwa sasa kuna kesi kortini baada ya chama chake cha Jubilee nchini Kenya kumvua useneta kwa msimamo wake unaokinzana na matakwa ya uongozi wa chama hicho .

Maelezo ya video, Kisiwa cha ukerewe kaskazini magharibi mwa Tanzania ambacho ni kimbilio kwa Albino

Mwaura anasema hatua ya kujaribu kumvua useneta ni mwendelezo wa ubaguzi wa watu kama yeye ambao anasema bado wanaangaliwa kama wanyonge ambao hawafai kuwa na maoni yao huru au misimamo yao binafsi .

' Wajua kuna tatizo kwamba mtu kama mimi mwenye hali hii akipewa nafasi ,basi nafaa kuitikia kila ninachoambiwa-nimechukuliwa kana kwamba nimehurumiwa ilhali uwezo wangu ni kama wa seneta au kiongozi yeyote yule.Hilo ni tatizo ambalo bado watu wenye ulemavu wa ngozi wanapitia kila siku maishani' anasema Mwaura .

Mwaura anasema juhudi zaidi zinahitajika kulinda haki za watu wenye ulemavu wa ngozi kwasababu hatari wanazokabiliwa nazo ni nyingi zikiwemo mauaji ,uuzaji wa sehemu za miili yao,kubaguliwa na hata kutelekezwa na familia zao .

Kuachwa na baba yake

Jambo ambalo linampa jaka moyo hadi leo ni kwamba alipokuwa na umri wa miaka minne ,baba yake alimtoroka mama yake kwa sababu alisema hakutaka kumlea Mwaura kwa sababu ya hali yake ya ngozi .Anasema babake alikataa kuendelea kumpa malezi akidai kwamba 'hakutaka kumlea mtoto aliyefanana na nguruwe'.

Mwaura anasema huu ndio uliokuwa mwanzo wa kasumba ya kuonekana tofauti au kudhalilishwa na kwa namna fulani ni jambo ambalo limempa msukumo wa kutaka kuwasaidia watu wengine waliozaliwa na ualbino .

ISAAC MWAURA

Chanzo cha picha, iSAAC MWAURA

'Hatujawahi kukutana na baba yangu.. nimejaribu kumsamehe baba yangu ,kuna pengo ambalo siwezi kuliziba .Kila mtoto anafaa kulelewa na wazazi wake wote na watoto wengi wenye ulemavu wa ngozi wamelelewa na mama zao pekee' anasema Mwaura .

Mwaura anaishauri jamii kubadiisha dhana kwamba watu wenye ulemavu wa ngozi wana udhaifu fulani wa kutoweza kuafikia ama kutekeleza majukumu kama watu wengine .

Anasema kando na sababu ambazo ni za wazi ,watu wenye hali hiyo wana uwezo wa kunawiri katika majukumu mbalimbali na hata kazi ambazo watu wakawaida wanazifanya .

Maelezo ya video, Joanné Dion: Watu weusi wanafikiri nina hadhi ya kizungu

' Watu wanafikiri kwamba watu wenye hali hii hawajiwezi kwasababu ya hilo na ukijitokeza kwa ukakamavu kufanya jambo wanasema basi ....wewe si mlemavu'

' Iwapo utazaa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi basi hakikisha kwamba unahusika na maisha yake na usimuache' .

Wasichana wetu ni warembo na pia wanaweza kuwa wake za watu... tuondoe kasumba kwamba hawawezi' anasema Mwaura.

Ruka X ujumbe
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe

Seneta huyo ambaye pia ni baba wa mtoto wa kiume anasema masaibu aliyopitia akiwa mtoto yamemfanya kutaka kuwa baba anayehusika pakubwa na maisha ya mwanae ili kuepuka kabisa kumfanya mtoto wake kupata pengo ambalo yeye alilipitia baada ya kuachwa na baba yake .

Anasema 'Ningependa sana kukutana na baba yangu kwa sababu wakati mwingine unaskia kwamba yupo.. mara aliaga dunia lakini maisha yanaendelea..'

Anatoa ushauri kwa wanaume ambao labda watapata watoto albino- 'Hata kama hutaishi na mama yake mtoto wako ambaye ni albino basi kuwa katika maisha yake...watu wenye ulemavu wa ngozi wanakosa kupata wapenzi , hakuna anayetaka kuwaoa na wanakumbwa na changamoto za kukosa ajira pamoja na tishio la mauaji'

Kuna matumaini

'Tumepiga hatua kubwa .Mwanzoni hata hakukuwa na siku ya watu wenye ulemavu wa ngozi na tumepigania siku hii tangia mwaka wa 2006 na 2007.

Hata kupata uakilishi bungeni imekuwa ni mapambano ya muda mrefu' anasema Mwaura .

Mwaura anasema safari ya watu wenye ulemavu wa ngozi imekuwa ndefu na sasa kibarua kipo mikononi mwao .'Mpiganie nafasi za kazi na onyesheni vipaji vyenu bila uwoga' anasema.

iSAAC MWAURA

Chanzo cha picha, iSAAC MWAURA

Ameongeza kuwa hapo awali haikuwa rahisi kumuona mtu mwenye ulemavu wa ngozi katika baadhi ya nafasi za kazi lakini sasa kunao wanaohudumu kama maafisa wa magereza na wengine hata wapo katika taaluma kubwa kuihudumia jamii .

'Hakuna aliyeweza kujua kwamba mtu albino anaweza kushika bunduki ,sasa kuna ambao wapo katika shirika la vijana wa kujenga taifa ,NYS'

'Jitokezeni kwa sababu asiyekuwepo na lake halipo'